FAMILIA YA NYERERE YAMKANA MTUHUMIWA WA MAUAJI...

Familia ya Joseph Nyerere, imemkana mtuhumiwa wa kesi ya mauaji, aliyejitambulisha kwa jina la Makongoro Joseph Nyerere.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na mmoja wa wanafamilia hao, Nuru Nyerere,   kwa niaba ya familia hiyo, ilisema hadi kifo cha baba yao, Joseph  mwaka 1994 hawakuwa na taarifa zozote za ndugu yao anayeitwa Makongoro Joseph Nyerere.
“Hadi baba anafariki dunia, hatukuambiwa kama tuna ndugu anayeitwa Makongoro Joseph Kizurira Nyerere …watoto wote wa mzee Joseph tunafahamiana, lakini kwa huyu ndiyo kwanza tunaambiwa kuwa ni ndugu yetu.
“Tunauhakikishia umma kwamba hadi kifo cha baba yetu hatukuambiwa juu ya kuwapo kwa ndugu mwenye jina hilo; hii ina maana kwamba hatumtambui,” alisema Nuru.
Naye mtoto mwingine wa Joseph, Matare, alisema: “Tangu kutangazwa kwa habari hizi tumepata simu nyingi za pole. Tunashangaa kwa sababu huyu mtu hatukuwahi kuambiwa kuwa ni ndugu yetu na wala yeye mwenyewe hakuwahi kuja kwetu kujitambulisha kama ni mmoja wa watoto wa mzee Joseph.”
Matare alisema amesema kwa mshituko kwenye magazeti ya juzi na katika mitandao ya jamii, kuwa kuna mtu anayejiita Makongoro Joseph Nyerere.
“Huyu hatumtambui kwa uhusiano, taarifa wala sura. Watoto wote wa marehemu Joseph Nyerere wanafahamika, hakuna mtoto wa marehemu mwenye jina hilo,” alisema.
Juzi, Makongoro ambaye ni mfanyabiashara, mkazi wa Dar es Salaam, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka ya mauaji ya mfanyabiashara mwenzake, Onesphory Kitoli.
Mshitakiwa huyo anatarajiwa kuunganishwa katika kesi hiyo na mtuhumiwa mwingine mfanyabiashara maarufu, Marijani Abubakari, maarufu kama Papaa Msofe (50) na kesi hiyo itatajwa Februari 20, mwaka huu.
Wakili wa Serikali, Charles Anindo, alimsomea Makongoro mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Agnes Mchome, alidai kuwa Novemba 6, 2011 huko Magomeni Mapipa, Makongoro alimuua kwa makusudi Kitoli kinyume na kifungu cha 196 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.
Anindo alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na aliomba Mahakama iahirishe kesi hiyo hadi Februari 20, mwaka huu, ambako Makongoro ataunganishwa na Papaa Msofe kwenye mashitaka hayo.
Mshitakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

No comments: