BI HARUSI AANGUKA DIRISHANI NA KUFA WAKATI WA FUNGATE...

KUSHOTO: Abbie Emmett. KULIA: Sean Emmett.
Bi harusi mwenye miaka 27 kutoka Uingereza anaaminika kuanguka na kufa kutoka kwenye chumba cha hoteli wakati akiwa kwenye fungate mjini Dubai.
Abbie Emmett alifariki siku chache tu baada ya kuwasili katika Umoja wa Falme za Kiarabu akiwa na mumewe Sean, mwenye miaka 43, baba wa watoto watatu aliyetengana na mkewe, baada ya harusi yao iliyofanyika Afrika Kusini.
Polisi mjini Dubai walikuwa wakichunguza kilichotokea baada ya Abbie, ambaye ni binti wa kasisi, aliripotiwa kuwa ameanguka kutoka dirishani kwenye hoteli hiyo Jumanne iliyopita.
Alikuwa akichangia ghorofa mjini Addlestone, Surrey, na mwendesha pikipiki wa kulipwa wa mbio za Grand Prix, Sean, na alisemekana kuwa amefunga naye ndoa takribani wiki mbili zilizopita mjini Cape Town.
Jirani yao Nicole Turvey mwenye miaka 27, alilieleza gazeti la Sunday Mirror: "Najihisi mnyonge. Ni msichana mdogo sana, umri sawa na wangu. Inasikitisha kwa kila mmoja. Hakika alikuwa akihitaji kupata watoto."
Rafiki mwingine, ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema 'hakuweza kuamini' kilichotokea na kumsifia Abbie kama 'mtu mwenye upendo'.
Msemaji wa mambo ya Nje alieleza: "Tumepokea taarifa ya kifo cha raia wa Uingereza mjini Dubai mnamo Februari 19.
Tunatoa msaada wa kibalozi kwa familia katika wakati huu mgumu."
Sean kwa sasa amestaafu mbio hizo lakini bado ni mkufunzi binafsi na amekuwa mshindi wa mbio 19 za pikipiki na pia kushiriki zaidi ya mashindano 50 ya MotoGP katika kipindi chake.

No comments: