LOWASSA ATAKA KATIBA ITAFSIRI RUSHWA...

Edward Lowassa.
Katiba mpya imetakiwa iwe na kifungu maalumu kitakachofafanua rushwa ni nini kwenye uchaguzi.
Lakini pia ieleze ni matumizi gani mgombea hawezi kuyakwepa katika kampeni zake, mathalani kukusanya wapiga kura kwenda kupiga kura, ikieleza gharama hizo atazibeba nani.
Hayo ni miongoni mwa mapendekezo ya Waziri Mkuu wa zamani, Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa aliyoyatoa mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dar es Salaam jana.
“Katika sehemu nyingi nchini, mwananchi kama hana fedha hawezi kugombea nafasi za uongozi. Katiba mpya iwe na ibara inayofafanua ni kiasi gani cha fedha ambacho mgombea anaruhusiwa kutumia katika kampeni,” alisema Lowassa.
Alisema kama hilo halitawezekana, basi uwepo mfumo ambao chama ndicho kitapigiwa kura badala ya mtu; vyama viwe ndivyo vinaingia kwenye uchaguzi kuwania majimbo na si wanachama.
“Huko kila mtu atakuwa anapigania chama chake kupata kura nyingi ili wapate viti vingi zaidi, pengine hii itasaidia kuondoa kikwazo cha mtu kuwa na uwezo wa kifedha ndipo aweze kuwania uongozi,” alisema Lowassa ambaye amekuwa akidaiwa kuwa na uwezo mkubwa kifedha.
Alipendekeza pia kuhusu elimu akisema angependa kipengele cha elimu ya sekondari kiwe kwenye Katiba ambayo itatamka wazi kuwa elimu hiyo ni bure.
“Nchi yetu bado ina idadi kubwa ya watu masikini. Uwezo wao wa kipato ni mdogo. Naamini kabisa Serikali inaweza kugharimia elimu ya sekondari, ikawa bure,” alisema na kuongeza kuwa hatua hiyo  itatoa nafasi ya kujenga Taifa lijalo lenye idadi kubwa ya vijana watakaokuwa wamepata elimu ya sekondari.
“Wabunge wenzangu bila shaka wanalijua hili. Ukweli katika majimbo yetu wazazi wamekuwa wakishindwa kulipia karo za shule kwa  watoto wao. Wabunge tumekuwa tukibeba mzigo huo japo kidogo. Kwa hiyo, kifungu cha elimu bure kwa sekondari, kiwe kwenye Katiba,” alisisitiza.
Kuhusu ardhi, Lowassa alisema Katiba ya sasa inawapa nguvu zaidi wakulima na kusahau wafugaji ambao wanaonekana kuwa wakimbizi nchini mwao, wakitangatanga kutafuta malisho ya mifugo yao.
“Kwa mwanadamu, kunyang'anywa haki ya kutumia ardhi ya nchi aliyozaliwa ni sawa na kunyang'anywa haki ya uraia wake,” alisema na kuongeza kwamba wafugaji wanapohamahama,  ardhi waliyokuwa wanaimiliki imekuwa ikimilikishwa watu wengine; wakulima au wawekezaji.
Alisema angependa Katiba hii mpya impe mfugaji haki katika suala la ardhi ambapo ardhi ya wafugaji italindwa na ifafanuliwe kikatiba. “Kuwe na mgawanyo wa asilimia 50 kati ya mfugaji na mkulima,” alisema.
Pia alizungumzia adhabu ya kifo alibainisha, kwamba ibara ya 14 ya Katiba ya sasa ya mwaka 1977 inazungumzia tu uhai ikitamka kiujumla tu kuwa kila mtu ana haki ya kuishi na uhai wake kulindwa.
“Lakini haki hiyo inanyang'anywa na kifungu namba 196 cha sheria ya kanuni za adhabu sura ya 16, inayotamka adhabu ya kifo kwa kosa la mauaji ya kukusudia. Adhabu hiyo hiyo pia hutolewa kwa kosa la uhaini. Sasa mapendekezo yangu ni kuwa na ibara inayotamka wazi kuwa hakutakuwa na adhabu ya kifo nchini kwa kosa la kukusudia au uhaini,” alisema.
Mapema aliisifu Katiba ya sasa akisema ni nzuri, imeliongoza Taifa katika umoja na mshikamano kwa muda wote huo. “Lakini,  kutokana na hali ya dunia ya sasa,  ni vema kuwapo Katiba mpya ili kuendana na hali halisi,” alisema.

No comments: