BANDARI SASA KUKATWA MISHAHARA KUFIDIA UPOTEVU MALI ZA WATEJA...

Dk Harrison Mwakyembe.
Baada ya kuwang’oa vigogo wa bandarini kwa ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka, sasa Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, amewageukia wafanyakazi.
Dk Mwakyembe ameagiza wafanyakazi watakaohusika na upotevu wa mali za wateja wote kuanzia mwezi ujao, walipe fidia ya mali hizo, kupitia mishahara na posho zao.
Akizungumza juzi mbele ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Dk Mwakyembe alisema ili kupunguza wizi mdogo na udokozi bandarini, wateja  watakaopotelewa na vifaa vyao bandarini, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), itawajibika kufidia.
Fidia hiyo kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, itatokana na    bajeti ya TPA na pengo la bajeti hiyo, litazibwa  kwa kuwakata mishahara na posho wafanyakazi wote waliokuwepo kwenye eneo la tukio wakati udokozi ukitokea. 
Katika taarifa yake hiyo ambayo gazeti hili linayo, Dk Mwakyembe, alisema kutokana na hatua ambazo Wizara hiyo imechukua dhidi ya vitendo vya ubadhirifu kwa baadhi ya viongozi wa mamlaka hiyo, tayari mafanikio yameanza kupatikana katika kipindi cha muda mfupi.
“Kuanzia Mei, mwaka jana hadi leo (juzi) hakuna kontena lililodaiwa kuibwa au kupotea. Hata hivyo udokozi kwenye mizigo pamoja na magari, bado unaendelea na mchezo huu tutaukomesha.
“Kuanzia mwezi ujao wateja watakaopotelewa na vifaa watalipwa fidia na wahusika kukatwa mishahara na posho zao,” alisema.
Alisema ufanisi wa upakuaji mizigo ambao umekuwa tatizo kwa miaka mingi bandarini hapo, umerejea kwa kasi ambapo muda wa kusubiri meli tangu inapoingia nchini mpaka inaondoka, umepungua kutoka siku 21 hadi siku 14 na sasa ni siku saba tu.
“Tayari nchi za Rwanda, Burundi na Uganda zimetuma mawaziri wake wa Uchukuzi nchini kuelezea utayari wao sasa kutumia Bandari ya Dar es Salaam,” alisema Dk Mwakyembe.
Alisema eneo la mapato, nalo lina mafanikio kwani kuanzia Septemba mwaka jana, mapato yamepanda kutoka wastani wa Sh bilioni 28 kwa mwezi, hadi Sh bilioni 38 Septemba mwaka jana na hadi kufikia Desemba mwaka jana, mapato hayo yalifikia Sh bilioni 50.
Dk Mwakyembe alisema pamoja na mafanikio hayo, pia Bandari hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo TPA kukabiliwa na malalamiko ya udokozi uliokithiri kwenye mizigo ya watu.
Alitoa mfano wa magari na upotevu wa makontena 32 na kuongeza kuwa asilimia 56.8 ya makontena yanayopotea bandarini hapo ni ya  DRC.
Alisema Chama cha Wafanyabiashara wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), waliiandikia Wizara ya Uchukuzi barua za malalamiko kuhusu wizi huo wa makontena hasa ya vitenge, khanga, maziwa ya kopo na nyembe na kueleza nia yao ya kususia bandari ya Tanzania.
Aidha katika kukabiliana na changamoto hiyo pamoja na ile ya Bandari hiyo kuwa na ufanisi duni, aliunda Kamati ndogo ya uchunguzi ya watu saba kubaini chanzo cha matatizo hayo iliyoongozwa na Wakili mzoefu wa Mahakama Kuu, Berbard Mbakileki na kamati hiyo ilimaliza muda wake Oktoba mwaka jana.
Alisema baada ya taarifa ya Kamati, alianza kuwaondoa wajumbe wote wa Bodi ya TPA na kuteua wapya ambayo baadaye ilikutana na Mamlaka ya Nidhamu kusikiliza tuhuma na utetezi kwa kila aliyetuhumiwa.
“Matokeo yake Bodi hiyo mpya iliwatia hatiani watumishi na viongozi wa TPA watano ambao ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Ephraim Mgawe, Naibu Mkurugenzi Mkuu Huduma, Hamadi Koshuma na Naibu Mkurugenzi Mkuu Miundombinu Julius Mfuko,” alisema.
Wengine ni Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam Cassian Ngamilo na Meneja wa Kitengo cha Mafuta Tumaini Massaro ambao wote baada ya kubainika kuwa na makosa mbalimbali, ikiwemo ubadhirifu na ufanisi duni, walifukuzwa kazi juzi.

No comments: