ANDREW CHENGE ATAKA MGOMBEA BINAFSI WA URAIS...

Andrew Chenge.

Aliyekuwa Waziri wa Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge ametaka Katiba ijayo iruhusu mgombea binafsi, lakini itungwe sheria ya kumdhibiti.
Chenge ambaye ni mbunge wa Bariadi Magharibi ameongeza kuwa mgombea huyo lazima adhibitiwe katika masuala mbalimbali yakiwamo ya dini na mengineyo.
Akitoa mapendekezo yake jana mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema iwapo sasa mgombea wa chama cha siasa ana sheria na taratibu zinazomdhibiti lazima binafsi naye adhibitiwe.
Chenge pia alipendekeza Rais asipunguzwe madaraka isipokuwa katika kuteua watendaji uwepo uthibitisho.
Akizungumzia kumpunguzia madaraka Rais alisema kuna miundo miwili ya utawala ya Waziri Mkuu kuwa mtendaji au Rais kuwa mtendaji lakini nchini Rais ni mtendaji   lakini anasaidiwa na tume mbalimbali hivyo la msingi labda katika uteuzi akishateua watu wathibitishwe.
Akizungumzia maadili alipendekeza Sekretarieti ya Maadili ya umma iwe tume ya kikatiba ili iwe na meno kwa kuwa na viongozi weledi na wenye uzoefu.
Alisema hata kama tume hiyo haitakuwa na meno ya kuwafikisha mahakamani viongozi watakaokiuka maadili wawe na uwezo wa kufikisha kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili wachukuliwe hatua.
Hivyo alitaka Tume iwe na uwezo kwa kupatiwa rasilimali za kutosha na watendaji wenye weledi katika kusimamia maadili yakiwamo  ya rushwa. Hata hivyo alisema Chenge alisema katika Katiba haiwezekani kuzungumzia rushwa bali ni kujenga misingi itakayosaidia kuidhibiti kwa kutungwa sheria.

No comments: