WAUMINI KANISA LA KKKT WAMGEUZIA KIBAO ASKOFU LAIZER...

Askofu Thomas Laizer.
Katika hali inayoonekana Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya   Kaskazini Kati kuparanganyika, sasa waumini wa Jimbo la Arusha Magharibi ndani   ya Dayosisi hiyo wametishia kujitenga iwapo masharti yao hayatatekelezwa. 
Masharti hayo ni pamoja na kuwataka viongozi waandamizi wa Dayosisi hiyo, akiwamo   Askofu Thomas Laizer na Katibu Mkuu wa Dayosisi, Israel Karyongi kujiuzulu   kutokana na tuhuma za ufisadi wanazozielekeza kwao.
Sambamba na viongozi hao kuachia nyadhifa zao, waumini hao pia wanataka Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Ngateu katika jimbo hilo, Philemon Mollel, arejeshewe   uchungaji wake mara moja bila masharti yoyote.
Mchungaji Mollel ambaye amekuwa mstari wa mbele kutetea na kupigania mali za Dayosisi hiyo, amefukuzwa kazi na kuvuliwa uchungaji ndani ya kanisa hilo.
Hatua  ya kuwataka viongozi hao waandamizi wa Dayosisi kujiuzulu na kurejeshewa   uchungaji wake Mchungaji Mollel ilifikiwa juzi katika kikao cha viongozi wa sharika   mbalimbali za Jimbo la Arusha Magharibi pamoja na wazee waliokutana jijini hapa kujadili mustakabali wa Dayosisi hiyo.
Mmoja wa viongozi wa jimbo hilo ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini, alithibitisha kuwapo kwa tamko hilo akisema kuwa wachungaji waliohudhuria kikao hicho wapo tayari kujitenga na Dayosisi ya Kaskazini Kati endapo uamuzi wao hautafanyiwa kazi.
‘’Hali ni tete wala tusijidanganye, waumini hawaelewi kinachoendelea na kinachofuata ni  sisi kujitenga na Dayosisi kwa kuwa ufisadi, udikteta na ufujaji ovyo wa mali  za Dayosisi unazidi kuongezeka kila kukicha,’’ alisema na kuongeza:
‘’Watu wanapigania wahusika katika kufuja mali za kanisa wawajibishwe lakini wengine wachache wanawaunga mkono kwa maslahi yao huku wengine wakitolewa kafara... Kamwe  hatutakubali haya yafanyike kanisani.”
Juhudi za kumpata Askofu Laizer na Katibu Mkuu wa Dayosisi, Karyongi hazikuzaa matunda, kwani simu zao ziliita bila kupokewa na hata walipotumiwa ujumbe wa simu uliotaka ufafanuzi juu ya hatua hiyo ya waumini, hakukuwa na majibu.
Hata hivyo, Mkuu wa  Jimbo la Arusha Magharibi, Mchungaji Godwin Lekashu, alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa hatua hiyo alisema: “Mimi kama Kiongozi wa Jimbo sina taarifa rasmi ya kikao hicho, na kama kingekuwa rasmi ningekuwa na taarifa na hata maamuzi yake ningeyafahamu.”
“Kwa ufafanuzi zaidi ningekushauri uwasiliane na msaidizi wa Askofu ambaye ndiye msemaji wa Dayosisi ya Kaskazini Kati,” alisisitiza Mchungaji Lekashu ambaye inaelezwa kwamba ni mfuasi mkubwa wa Katibu Mkuu wa Dayosisi hiyo.
Wiki mbili zilizopita Bodi ya Dayosisi hiyo chini ya Uenyekiti wa Israel Ole   Karyongi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa KKKT, ilimtimua kazi meneja wa hoteli ya   Corridor Springs inayomilikiwa na Dayosisi hiyo, John Njoroge kwa ubadhirifu wa   fedha za hoteli hiyo. 
Hata hivyo, Ole Karyongi naye katika kikao cha Desemba 15 mwaka huu  kilichohudhuriwa na wachungaji na wakuu majimbo walimtaka Mwenyekiti huyo  kuwajibika kwa kujiuzulu kwa kushindwa kusimamia vizuri mali za Dayosisi  hiyo.
Kasheshe ya yote haya imetokana Dayosisi hiyo kudaiwa deni la Sh bilioni 11 na moja  ya benki kubwa hapa nchini.
Dayosisi hiyo imeshapewa muda wa kufikia Desemba 31 mwaka huu iwe imelipa deni hilo, vinginevyo mali za kanisa zitakamatwa na kupigwa mnada kufidia deni hilo, ikiwemo hoteli hiyo.
Habari zilisema kuwa uongozi wa Dayosisi uliweka hospitali ya rufaa ya Seliani  inayomilikiwa na kanisa kuwa dhamana.
Taarifa zilisema kuwa iwapo deni hilo halitalipwa ndani ya muda huo huenda hospitali  hiyo ikapigwa mnada, hatua ambayo inapingwa vikali na waumini wa kanisa hilo.

No comments: