RC AAMURU POLISI KUKAMATA WAKOROFI MSIKITINI MWANZA...

Mhandisi Evarist Ndikilo.
Mgogoro wa umiliki wa Msikiti wa Masjidi Hidaya Kitangiri kati ya Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) na uongozi wa sasa wa msikiti huo, umefika kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo ambaye ametishia kuruhusu polisi kukamata yeyote atakayeleta vurugu na kumfikisha katika vyombo vya sheria.
Akizungumza jana katika kikao cha usuluhishi kilichokutanisha pande mbili zinazogombania umiliki wa msikiti huo, Ndikilo aliagiza yeyote atakayeleta vurugu, akamatwe.
“Kuna taarifa kuwa kuna vikundi vya watu vinavyotaka kuhatarisha amani, RPC nakupatia muda wa wiki moja kuhakikisha katika kipindi hiki ambacho mambo haya yanazungumzwa, hakuna tishio la amani na muwakamate wale wote watakaoonekana kuchochea vurugu kwenye msikiti huo,” alisema Ndikilo.
Alionya kuwa hatawavumilia watu wenye nia ya kuharibu amani kwa kisingizio cha mgongo wa imani za dini.
Katika mgogoro huo, uongozi wa Bakwata Mkoa unadai kuwa Msikiti huo ni mali yao na wana vielelezo vya kuumiliki  kuanzia mwaka 1984.
Lakini uongozi wa sasa wa Msikiti huo kupitia kwa Imamu wake, Juma Athuman, nao wanasema kuwa walianza kuumiliki Msikiti huo kuanzia mwaka huo huo.
Kwa mujibu wa Imamu Athumani, mgogoro huo ulianza baada ya uongozi wa Bakwata Mkoa wa Mwanza kusema wao ndio wenye haki ya kumiliki Msikiti huo, jambo ambalo alidai sio la kweli.
“Msikiti ule umenikuta nimeshazaliwa pale na haujawahi kumilikiwa na Bakwata, awali sisi ndio tuliotafuta kiwanja kutoka Jiji Block ‘B’ Na. 185, tukaanza kujenga msingi na baadaye tukapata mfadhili aliyetusaidia kuujenga,” alisema Imamu Athumani. 
Kutokana na kutoelewana, pande hizo mbili zilipeleka malalamiko yao kwa Mkuu wa Mkoa aliyeitisha kikao cha usuluhishi kati ya wawakilishi kutoka Bakwata Mkoa wa Mwanza na uongozi wa sasa wa Msikiti.
Katika kikao hicho, uongozi wa Msikiti uliwakilishwa na baadhi ya waumini wa Msikiti huo wakiongozwa na Imamu  Athumani na mmoja wa Kiongozi mwingine wa Msikiti huo, Ibrahim Selemani na Bakwata waliwakilishwa na Katibu wa Bakwata Mkoa, Mohamedi Balla.
Baada ya mazungumzo, Ndikilo aliwaasa wawakilishi hao kutumia njia za kidiplomasia kutatua mgogoro huo na kufafanua kuwa kwa mujibu wa sheria za nchi, Serikali haipaswi kutoa suluhisho la migogoro ya kidini, ambao alisema ulipaswa ushughulikiwe na waumini wao wenyewe na viongozi wao.
“Mimi kama Serikali majibu ya mgogoro huu ni nani aumiliki Msikiti huo wa Masijidi Hidaya Kitangiri yako mikononi mwenu maana nyie mnafahamu mambo ya imani zenu kwa kina, lakini mkishindwa kupata suluhu, Serikali ina vyombo vyake na vitalazimika kuja hata bila ya kuitwa,” alisema.
Kutokana na mazungumzo hayo, pande zote mbili ziliafiki kupata muda zaidi wa kuzungumza ili kufikia hatma ya usuluhishi wa mgogoro huo kabla ya kwenda kwenye vyombo vya kisheria.

No comments: