MWANAFUNZI ALIYEBAKWA NA WAHUNI SABA AFARIKI DUNIA...

KUSHOTO: Gari maalumu likisubiri kuchukua mwili wa mwanafunzi huyo kwenye Hospitali ya Mount Elizabeth, nchini Singapore. KULIA: Madaktari wakiondoa mwili wa mwanafunzi huyo tayari kwa maandalizi ya kuusafirisha kwenda India.
Binti ambaye alibakwa na kundi la wahuni na kupigwa vibaya ndani ya basi katika tukio ambalo halikuishitua India pekee, bali dunia nzima, amefariki dunia juzi usiku katika hospitali moja nchini Singapore.
Binti huyo mwenye miaka 23 alikuwa katika hali mbaya tangu baada ya tukio hilo akisumbuliwa na viungo vyake kadhaa kushindwa kufanya kazi na mshituko wa moyo, na licha ya juhudi za madaktari bingwa katika Hospitali ya Mount Elizabeth, juzi usiku akapoteza maisha yake.
Mateso yake ya kutisha yamewaamsha Wahindi kudai ulinzi mkubwa kwa wanawake dhidi ya matukio ya ubakaji ambayo yanaathiri maelfu kati yao kila siku, huku maandamano makubwa yakiendelea kuikumba nchi hiyo.
Tofauti na mateso ya kutisha aliyopitia katika mikono ya wabakaji wake, 'alifariki bila purukushani' huku familia yake na maofisa wa Ubalozi wa India wakiwa kando yake," alisema Dk Kevin Loh, Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Mount Elizabeth ambako alikuwa akipatiwa matibabu tangu Alhamisi iliyopita.
"Timu ya madaktari wa Hospitali ya Mount Elizabeth, manesi na wafanyakazi wanaungana na familia yake katika kuomboleza kuondokewa naye," alisema katika taarifa.
Alisema mwanamke huyo aliendelea kuwa katika hali mbaya tangu Alhamisi wakati alipoletwa kwa ndege Singapore kutoka India.
Licha ya juhudi za timu ya madaktari bingwa wanane wa Hospitali ya Mount Elizabeth kuimarisha afya yake, hali yake iliendelea kuzorota katika siku hizi mbili. Alikuwa akisumbuliwa na viungo vingi kushindwa kufanya kazi kutokana na majeraha makubwa mwilini mwake na kwenye ubongo. Alikuwa na ujasiri katika kupambana na hali hiyo kwa kipindi kirefu dhidi ya mabaya yote lakini kiwewe mwilini mwake kilitawala kwa yeye kuweza kukishinda."
Balozi wa India, T.C.A. Raghanvan aliwaeleza waandishi kwamba uwiano wa majeraha aliyokuwanayo yaliashiria 'zaidi kifo' na mwishoni 'yalithibitisha hayadhibitiki.'
Alisema mipango inafanywa kuweza kurejesha mwili wake India.
Yeye na rafiki yake wa kiume walikuwa wakisafiri kwenye basi la abiria Desemba 16 jioni ndipo waliposhambuliwa na wanaume sita ambao walimbaka na kuwapiga wote wawili, kuwavua nguo wote uchi wa mnyama na kuwatupa kando ya barabara.
Tukio hilo limekuja wakati mwathirika mwingine wa ubakaji nchini India anasemekana kujiua baada ya polisi kuchukua siku 14 kufungua kesi na siku 30 zaidi kuweza kuwakamata watuhumiwa.
Mapema jana madaktari waliripoti kwamba mwanafunzi huyo mwathirika wa ubakaji alikuwa tayari 'akipambana dhidi ya mabaya kufuatia ugonjwa wa moyo, mapafu na athari za uti wa mgongo na majeraha kwenye ubongo."
Lakini Ijumaa jioni, hali ya binti huyo 'ilibadilika na kuwa mbaya' na nuru yake ikaanza kudorora kutokana na viashiria vya viungo kadhaa kushindwa kufanya kazi, alisema Dk Kevin Loh.
Hii ni licha ya madaktari kupigania maisha yake ikiwamo kumwekea vifaa bandia vya kusaidia kupumua, dawa za maumivu na pia vichocheo vya kudhibiti uwezo wa mwili wake kupambana na maambukizi," alisema, na kuongeza kwamba wanafamilia wake walikuwa kando yake.
Polisi wamewakamata watu sita kuhusiana na shambulio hilo na kwamba wako mikononi mwa polisi.
Serikali ya India imechukua hatua kufuatia siku kadhaa za ghasia kupinga shambulio hilo kwa kuahidi kuweka hadharani picha, majina na anwani za wabakaji watakaotiwa hatiani.

No comments: