Mfungwa aliyekuwa mikononi mwa askari Magereza, ametoroka na kulazimika kukimbia uchi wa mnyama mitaani, baada ya kuvua sare za wafungwa, ili kuficha utambulisho wake.
Mashuhuda wa tukio hilo, walilieleza gazeti hili jana kwamba mfungwa huyo baada ya kufanikiwa kuwatoroka askari Magereza na kuvua sare, alijikuta akilazimika kutafuta mahali pa kujificha.
Hata hivyo, mashuhuda walisema karibu kila nyumba alikokimbilia, wenyeji walimfukuza kwa hofu kuwa ni mwendawazimu.
“Bahati haikuwa yake kwa kuwa kila nyumba alikokimbilia kujificha walimfukuza, hakuwa na la kufanya ila kukimbia mitaani akiwa uchi.
“Lakini alipovuka tu uwanja wa ndege katika kitongoji cha Edeni alikuwa tayari amechoka, alianguka na kuzingirwa na umati mkubwa wa wananchi hadi askari Magereza walipofika,” alisema mmoja wa mashuhuda.
Wakati akitafuta mahali pa kujisetiri, baadhi ya watu waliomshuhudia walidhani ni kichaa na wengine walimpigia yowe la mwizi huku wakimtupia mawe na fimbo hadi walipobaini kuwa si mwizi.
Mmoja wa mashuhuda hao alidai kuwa kutokana na kipigo hicho, mfungwa huyo alilazimika kuwasihi wananchi wasimpige wala wasimuue kwa kuwa yeye ni mfungwa aliyekuwa akisaka fursa ya kuwa huru kwa njia ya mkato.
“Kwanza tulidhani ni mwizi lakini alitusihi tusimuue kwani alikuwa ni mfungwa tu akijaribu kutoroka ili awe huru ndipo tulipoacha kumpiga…kwa kweli mtu huyu alidhamiria kutoroka lakini kwa staili hii ya kukimbia uchi imetustaajabisha wengi,” alisema shuhuda mwingine.
Baada ya kuacha kumpiga, wananchi hao waliendelea kumzingira mpaka askari Magereza walipofika ambapo inadaiwa baadhi walimpiga huku wakisikika kudai kuwa
watampatia kipigo zaidi watakapomfikisha gerezani huku baadhi ya wananchi wakimuonea huruma na kuomba askari hao wasimpige.
Mkuu wa Gereza la Sumbawanga, SSP Mndolo alikiri kutoroka kwa mfungwa huyo, lakini hakuwa tayari kutoa maelezo zaidi.
“Sio kweli kuwa askari wetu walishiriki kumpiga mfungwa huyo, sio kweli kabisa,” alikanusha na kudai kuwa mfungwa huyo kwa sasa ni mzima wa afya.
Alipoelezwa kuhusu mashuhuda, Kamanda Mndolo ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake la pili, alisema ikithibitika kuwa walimpiga watamchukulia hatua kali za kinidhamu.
“Ninavyozungumza nawe mfungwa huyo ni mzima wa afya na ikithibitishwa kuwa askari wetu walimpiga basi tunao utaratibu, kwanza hawaruhusiwi kujichukulia sheria mikononi, hilo ni kosa watachukuliwa hatua kali za kinidhamu,” alisema Kamanda Mndolo.
No comments:
Post a Comment