MAPYA ZAIDI YAIBUKA MGOGORO WA KANISA LA KKKT...

Hoteli ya Corridor Springs ya Arusha inayomilikiwa na KKKT.
Katika kuhakikisha linapata kiini cha madeni makubwa yanayotishia kupigwa mnada kwa mali za Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Kanisa hilo limechukua uamuzi wa kumfukuza kazi Meneja wa Hoteli ya Corridor Springs inayomilikiwa na Dayosisi hiyo, John Njoroge, imefahamika.
Hata hivyo, hatua hiyo imedaiwa ni sawa na `danganya’ toto, ikielezwa siri nzito imejificha.
Mbali ya kumtimua Meneja huyo ambaye imebainika kuwa alikuwa raia wa nchi jirani ya Kenya, wachungaji wa kanisa hilo walio mstari wa mbele kutaka Bodi ya Hoteli hiyo iwajibike kwa ubadhirifu na uzembe, imeelezwa nao wameanza `kushughulikiwa’ kwa kulimwa barua za kujieleza.
Uchunguzi umebaini kuwa, mmoja wa wachungaji, Kiongozi wa Usharika wa Ngateu katika Jimbo la Arusha Magharibi, Philemon Mollel, ameandikiwa barua ya kuwa na “tabia mbaya katika huduma ya kichungaji”, lakini ikidaiwa sababu kubwa ni kuwa na msimamo wa kuitaka Bodi ya Hoteli hiyo kuwajibika.
Katika nakala ya barua ya Desemba 17, mwaka huu iliyoandikwa Mollel na Katibu Mkuu wa Dayosisi hiyo, Israel ole Karyongi pamoja na mambo mengine, inamtuhumu Mchungaji Mollel kuwa na tabia mbaya mbele ya waumini ya kuwadharau na kuwakashifu viongozi wa Kanisa, akiwamo Askofu Thomas Laizer.   
Hata hivyo, Mchungaji Mollel alipinga madai hayo akisema kuwa chanzo cha barua hiyo ni msimamo wake wa kutaka ukweli juu ya madeni ya mali za Dayosisi hiyo uwekwe hadharani na wahusika wawajibishwe.
“Niliweka wazi msimamo wangu katika kikao tulichofanya Desemba 15, mwaka huu kwamba Bodi lazima iwajibike kwa haya yote na kuwataka wenzangu (wachungaji na wakuu wa majimbo) tusitafune maneno kwa sababu ukweli uko wazi na dhahiri,” alisisitiza Mchungaji Mollel na kuongeza:
“Niliwaambia wajumbe wazi kwamba msitufanye wajinga mbele ya washirika na hiyo ndiyo sababu ya kuandikiwa barua hii na nitaweka kila kitu hadharani kesho (Jumapili),” alisema.
Kuhusu Njoroge, habari kutoka ndani ya hoteli hiyo zinasema kuwa alitimuliwa kazi wiki mbili zilizopita kutokana na shinikizo la wachungaji wa kanisa hilo kufuatia hali mbaya ya kifedha ya hoteli hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Hoteli hiyo, Israel ole Karyongi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Dayosisi hiyo, alithibitisha kutimuliwa kwa Meneja huyo akidai kuwa ni hatua ya kupisha uchunguzi ili kubaini ukweli wa ubadhirifu wa hoteli hiyo na mambo mengine.
“Ni kweli Meneja ametimuliwa ili kupisha uchunguzi wa kina ufanyike kujua ukweli wa hali halisi na sasa timu ya wakaguzi inaendelea na kazi ya kupitia mahesabu ya hoteli,” alithibitisha Karyongi.
Hata hivyo, habari za ndani za hoteli hiyo na Dayosisi zinasema, hatua ya kufukuzwa kwa meneja huyo ni janja ya viongozi waandamizi wa Dayosisi ambao inasemekana walishirikiana naye kuifilisi hoteli hiyo.
Uchunguzi unaonesha kuwa Njoroge amefichwa nchini Dubai na viongozi hao waandamizi wa Dayosisi (majina yamehifadhiwa kwa sasa) ili wasiumbuke kutokana na sakata hilo.
“Huyu bwana hivi tunapozungumza hata kwao Kenya hapatikani na baadhi ya jamaa zake wanasema kuwa yupo Dubai akisubiri hatima ya ukaguzi huo,” alisema rafiki wa karibu wa Njoroge ambaye alikataa kutaja jina lake.
Inasemekana hata mali alizokuwa akimiliki Njoroge ikiwamo Klabu ya usiku inayoitwa Brazil iliyokuwa maeneo ya Nanenane Njiro, ameiuza kabla ya kuondoka nchini kinyemela.
Pamoja na mambo mengine, Njoroge anadaiwa kushindwa kusimamia uendeshaji wa hoteli hiyo kiasi cha kushindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi wa hoteli na kodi mbalimbali za Serikali kwa miezi tisa.
Kutokana na hilo, kumekuwa na hali ya kukabana koo ndani ya Kanisa, yakitakiwa maelezo ya kina kuhusu kiini cha mali za kanisa kukaribia kuwekwa rehani kwa sababu ya madeni katika miradi inayojiendesha.
Mgawanyiko huo umetokana na upande mmoja kutaka Bodi ya Hoteli ya Corridor Springs chini ya Uenyekiti wa Katibu wa Dayosisi, Israel ole Karyongi, kuwajibika huku upande mwingine ukipinga hoja hiyo.
Hoteli hiyo inayomilikiwa na Dayosisi hiyo iko hatarini kupigwa mnada baada ya kushindwa kulipa marejesho ya mkopo uliochukuliwa kutoka benki moja ya biashara ili kuijenga mwaka 2006.
Hali ya hewa ndani ya Dayosisi imechafuka tangu waumini wake walipotakiwa kuchangia Sh 20,000 kila mmoja, ili kulipa deni la benki hiyo ya biashara kabla ya Desemba 31, mwaka huu ili kunusuru mali za Dayosisi hiyo ikiwamo Hoteli ya Corridor Springs na Hospitali ya Rufaa ya Selian zisipigwe mnada.
Chanzo cha mgogoro huo ni maagizo mawili tofauti ya kuwataka waumini hao wachangie kunusuru mali za Dayosisi hiyo yaliyotolewa ndani ya mwezi mmoja uliopita.
Katika maagizo ya kwanza yaliyotolewa kwa wakuu wa majimbo wa Dayosisi katika kikao kilichoketi Novemba 27, mwaka huu, ilielezwa kuwa deni lilikuwa Sh milioni 680.
Habari za uhakika zilisema kuwa kikao hicho kiliamua kila jimbo lichangie fedha kwa kadiri ya uwezo wa waumini wake na kila moja lilipangiwa kiasi wanachotakiwa kuchanga ili kuokoa mali za Dayosisi. Kwa mfano, Jimbo la Arusha Magharibi lilitakiwa kuchangia Sh milioni 300 kabla ya mwishoni mwa Machi mwakani.
Vyanzo vya habari vilisema kuwa maagizo hayo yalitolewa kwa wakuu wa majimbo sita yanayounda Dayosisi hiyo ya Kaskazini Kati.
Hata hivyo, wakati maagizo hayo yakitekelezwa, Desemba 9, mwaka huu Makao Makuu ya Dayosisi ilitoa waraka wa kutaka kila muumini kuchangia Sh 20,000 kama kiwango cha chini kabla ya Desemba 31, mwaka huu.
Hata hivyo, Karyongi hivi karibuni alilieleza gazeti hili kuwa deni hilo si Sh bilioni 11 kama inavyodaiwa bali ni Sh bilioni moja, ingawa waraka wa kuwataka waumini zaidi ya 600,000 kuchangia Sh 20,000 kila mmoja, wangepata Sh bilioni 12.

1 comment:

Anonymous said...

Kwahiyo kwa sasa mmelipa?