MAMBA ANYAKUA MTOTO WA MIAKA 12 AKIOGELEA...

Mtoto wa kiume wa miaka 12 ameburutwa na mamba ambaye alitoweka kwenye maji akiwa na mtoto huyo kinywani mwake jana katika tukio la pili la kutisha ndani ya kipindi cha wiki mbili kwenye Ukanda wa Kaskazini wa Tropiki nchini Australia.
Ingawa timu ya polisi na walenga shabaha waliendelea na msako kumtafuta kijana huyo jana binafsi wanahofia kwamba mtoto huyo yuko nje ya uwezekano wa kupatiwa msaada.
Chini ya wiki mbili zilizopita, binti wa miaka saba aliuawa na mamba katika Ukanda huo wa Kaskazini, katika kile kinachoaminika kuwa mabaki yake kukutwa ndani ya mnyama huyo ambaye baadaye alipigwa risasi katika eneo binti huyo alipotoweka.
Katika tukio la hivi karibuni, mtoto huyo wa kiume, anayeaminika kutokea Aboriginal karibu na Port Bradshwa, maili 400 mashariki mwa Darwin, alishambuliwa na mamba wakati akiogelea na kundi la watu katika wangwa tulivu.
"Ripoti za awali zinadai watu wazima katika kundi hilo walijaribu kumwokoa mtoto huyo kwa kumchoma mishale mnyama huyo, lakini mamba huyo akamkokota mtoto na kumpeleka kwenye kina kirefu," alisema mkuu wa polisi Michael White.
Alisema maofisa kutoka kituo cha polisi cha Aboriginal walibaki eneo la tukio hadi giza na wangeendelea na msako wa mtoto huyo mapema alfajiri inayofuata.
White alisema janga hilo kwa mara nyingine limeangazia hatari iliyoko katika kuogelea kwenye maji kaskazini mwa Australia.
Tukio la jana lilikuwa kumbukumbu ya siku moja mapema Novemba pale binti wa miaka saba aliponaswa na mamba wa majichumvi maili 210 mashariki mwa Darwin, mji mkuu wa Ukanda wa  Kaskazini.
Polisi waliondesha msako walifanikiwa kumpiga risasi na kumuua mamba mwenye urefu wa futi 10 na uchunguzi wa mnyama huyo ulibaini vile vilivyoaminika kuwa mabaki ya mtoto ndani ya tumbo lake.
Mamba wa majichumvi, ambao wanaweza kufikia hadi urefu wa futi 25 na uzito wa zaidi ya tani moja, ni wengi mno katika Ukanda wa Kaskazini na alama za tahadhari zimewekwa karibu na maji zikionya wageni kukaa mbali na maji.
Mamba wanalindwa katika Ukanda wa Kaskazini na idadi yao imekuwa ikiongezeka kwa kasi kubwa, na kusababisha mashambulio kadhaa kwa binadamu.

No comments: