MAMA WA BINTI ALIYEBAKWA NA WAHUNI SABA AANGUKA GHAFLA...

Jeneza lenye mwili wa binti aliyebakwa na wahuni likiwa ndani ya gari mara baada ya kuwasili mjini Delhi.
Mama wa binti wa India ambaye alibakwa na kundi la wahuni amekimbizwa hospitali jana baada ya kuanguka wakati mwili wa binti yake ulipokuwa ukichomwa moto.
Pia imefahamika kwamba mwanafunzi huyo wa tiba ya viungo mwenye miaka 23 alipanga kufunga ndoa na rafiki yake wa kiume, ambaye alijeruhiwa katika shambulio hilo, kwa mujibu wa majirani zake.
Mwili wa msichana huyo ulichomwa moto mapema jana baada ya ndege iliyokodiwa na Serikali ya India kurejesha mwili wake mjini Delhi kutoka hospitalini nchini Singapore ambako alifariki juzi wakati akipatiwa matibabu kufuatia majeraha makubwa aliyopata.
Mateso yake ya kutisha yamewaamsha raia wa India kutaka ulinzi mkubwa kwa wanake kutokana na vitendo vya ubakaji kupitia maandamano makubwa, uwashaji mishumaa na kupinga mitaani wakiwa na mabango na vizuizi barabarani.
Msichana huyo na rafiki yake wa kiume walikuwa wakitazama filamu ya The Life of Pi jioni katika jengo la sinema lililoko wilaya ya Saket mjini New Delhi ndipo waliposhambuliwa kwenye basi wakiwa njiani kurejea nyumbani Desemba 16, mwaka huu.
"Walishafanya maandalizi yote ya harusi na walikuwa wamepanga kufanya sherehe ya harusi mjini Delhi," jirani aliieleza NDTV.
"Tunafahamu kwamba alikuwa aolewe mwezi Februari," alisema. "Majirani wote wameshitushwa na kilichotokea."
Sherehe za siri jana zilifanyika zikiambatana huku Polisi wa kuzuia ghasia nchini India wakiweka ulinzi nje ya jengo la kuchomea miili mjini New Delhi.
Wakihofia maandamano miongoni mwa wananchi wenye hasira, eneo na muda wa kuchoma mwili haukuwekwa wazi, lakini ilifanyika mapema baada ya mwili kuwasili kutoka Singapore kwenye ndege maalumu ya Air-India.
Mama yake aliyechanganyikiwa alianguka na kupelekwa Hospitali ya Safdarjung baada ya mwili wa binti yake kuondolewa.
Waziri Mkuu Manmohan Singh na Sonia Gandhi, wakuu wa chama tawala cha Congress, walikuwa uwanja wa ndege kupokea mwili na kukutana na wanafamilia wa muathirika ambao pia waliwasili katika ndege hiyo.
Baada ya mwili kuwasili uwanja wa ndege, ulipelekwa kwenye nyumba ya binti huyo mjini New Delhi kwa taratibu za kidini kabla ya kusindikiwa na polisi hadi sehemu ya kuchomea mwili.
Ulinzi ulikuwa mkali, huku kukiwa hakuna ruhusa kwa wananchi au vyombo vya habari kuingia kwenye eneo la kuchomea mwili.
Taarifa kuhusu utambulisho wa binti huyo havikutolewa hadharani kwa usalama wa familia yake.
Wazazi wake waliuza sehemu ya ardhi jirani yao na pia ardhi kwenye kijiji chao huko wilaya ya Ballia iliyoko mashariki mwa Uttar Pradesh kugharimia elimu ya binti yao.
"Sasa kaka yake mkubwa, ambaye anajiandaa kwa mitihani ya uhandisi, hana matumaini ya kuendelea na masomo yake. Familia jiyo ilitegemea mafafikio ya binti huyo katika fani yake ili kuwanasua kutoka kwenye umaskini wao," jirani aliyejitambulisha kwa jina la Vimla aliieleza IANS.
Watuhumiwa sita waliokamatwa wanakabiliwa na adhabu ya kifo endapo watapatikana na hatia.

No comments: