KESI YA RAIS WA CHAMA CHA MADAKTARI YAPIGWA KALENDA...

Dk Namala Mkopi.
Kesi ya kudharau amri ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi inayomkabili Rais wa Chama cha Madaktari nchini (MALT), Dk. Namala Mkopi imeahirishwa hadi Januari 23 mwakani itakapoendelea kusikilizwa.
Hakimu Hellen Liwa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, aliahirisha kesi hiyo hadi mwakani watakapoendelea kusikiliza ushahidi wa upande wa mashitaka.
Dk Mkopi anakabiliwa na mashitaka mawili ya kudharau amri ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi iliyowataka madaktari waliogoma nchi nzima wasitishe mgomo, na shitaka jingine ni kuwashawishi madaktari wagome.
Akisomewa maelezo ya awali Septemba mwaka huu ilidaiwa kuwa, Juni mwaka huu  madaktari wanaofanya kazi katika hospitali za serikali waliingia kwenye mgomo dhidi ya mwajiri wao ambaye ni serikali na mgomo huo uliandaliwa na MAT ambapo madaktari waligoma kuwahudumia wagonjwa.
Wakili Tumaini Kweka alidai kuwa wakati mgomo huo ukiendelea serikali ilipeleka maombi Mahakama Kuu Diveshini ya Kazi kuomba mahakama hiyo itoe amri ya kuzuia mgomo huo usiendelee hadi mgogoro baina ya Mat na Serikali ulifunguliwa katika Tume ya Usuluhishi wa Migogoro (CMA) utakapomalizika.
Aidha Kweka alidai kuwa Juni 22 mwaka huu, Mahakama Kuu ilitoa amri ya kuwataka madaktari waliogoma nchi nzima wasitishe mgomo na mahakama hiyo ikampa nakala ya amri hiyo Dk Mkopi  Juni 25 mwaka huu, lakini waliendeleza mgomo.
Juni 26 mwaka huu, Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ilitoa amri nyingine kwa MAT iliyokuwa ikikitaka chama hicho kutekeleza kwa vitendo amri ya mahakama iliyotolewa Juni 22 mwaka huu ambayo ilimtaka Dk. Mkopi kwenda kwenye vyombo vya habari kuwatangazia madaktari wote waliogoma wasitishe mgomo huo; lakini alidharau amri hizo mbili za mahakama.
Hata hivyo, Dk Mkopi alidai kuwa madaktari hawakugoma kuwatibia wagonjwa na kwamba si kweli kuwa alidharau amri ya mahakama iliyomtaka aende kwenye vyombo vya habari kuwatangazia madaktari waache kugoma.

No comments: