KESI YA MSANII LULU YATINGA RASMI MAHAKAMA KUU...

Msanii Lulu akisindikizwa mahakamani kusikiliza mashitaka yake ya mauaji.
Kesi ya mauaji ya kutokukusudia inayomkabili msanii wa Filamu nchini, Elizabeth Michael `Lulu’, imepokelewa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kusajiliwa kwa namba 125 ya mwaka 2012.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana mahakamani hapo, kesi hiyo imepokelewa kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na inasubiri kupangiwa Jaji na tarehe ya kuanza kusikilizwa.
Awali Lulu alikuwa akikabiliwa na mashitaka ya kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba, kwa kukusudia lakini baada ya upande wa mashitaka kukamilisha upelelezi alibadilishiwa mashitaka na kuwa kuua bila kukusudia.
Kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu  Augustina Mmbando, katika hatua za awali na Lulu hakuruhusiwa kujibu mashitaka yanayomkabili kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Kwa mujibu wa sheria, kutokana na Lulu kushitakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia, anaweza kupata dhamana.
Desemba 21 mwaka huu, Lulu alisomewa maelezo ya kesi na ushahidi utakaotumika na upande wa mashitaka katika kesi hiyo, ambapo Wakili wa Serikali Shedrack Kimaro alidai kuwa watakuwa na mashahidi tisa, ushahidi wa nyaraka, ripoti ya uchunguzi wa hospitali na ramani ya eneo la tukio.
Baadhi ya mashahidi watakaotoa ushahidi ni pamoja na mdogo wa marehemu, Seth Bosco, Sofia Kassim, Daktari wa marehemu aitwaye Pancras Kageigwa, Morris Semkwao na Esther Zephania ambaye ni askari Polisi wa kituo cha Oysterbay, Kinondoni.
Katika kesi hiyo, inadaiwa kuwa Aprili 7, mwaka huu nyumbani kwa Kanumba, Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam, Lulu alimuua bila kukusudia msanii huyo nyota wa filamu nchini.

No comments: