JINSI MEDALI ZILIVYOMWOKOA MO FARAH NA UGAIDI MAREKANI...

Mwanariadha Mo Farah akionesha medali zake za Olimpiki.
Shujaa wa Olimpiki nchini Uingereza, Mo Farah amebainisha jinsi alivyohojiwa na maofisa wa mpakani nchini Marekani wakimtilia mashaka kwamba ni gaidi.
Mshindi huyo wa medali mbili za dhahabu, ambaye pia ametunukiwa tuzo ya CBE katika orodha ya watunukiwa wa Mwaka Mpya, alisema aliburutwa mbele ya walinzi wakati akiingia nchini humo kwa ajili ya mapumziko ya Krismasi mwaka huu.
Mkimbiaji huyo mwenye miaka 29 alilieleza gazeti la The Sun kwamba walinzi wa mpakani walimuuliza maswali kwa sababu ya 'asili yake kutoka Somalia'.
Mwanariadha huyo alilazimika pia kuonesha medali zake za Olimpiki katika juhudi za kuthibitisha yeye ni nani hasa.
Katika ziara yake iliyopita nchini humo, Farah alibainisha kwamba alitakiwa kuondoka kabla ya kupokea barua ikieleza kwamba 'alikuwa chini ya uchunguzi wa tishio la ugaidi'.
Farah alihamia Uingereza akiwa na baba yake mzaliwa wa Uingereza wakati alipokuwa na umri wa miaka minane tu.
Alisema kwamba alikamatwa na walinzi wa mpakani wakati akitembelea Portland, Oregon, akiwa na familia yake katika mapumziko ya Krismasi.
Mwanariadha huyo alisema: "Siwezi kuamini. Sababu ya asili yangu ya Kisomali nimekuwa nikikamatwa kila mara ninapokuja kwenye Ofisi za Forodha za Marekani."
Farah alisema alilazimika kuishia 'kuonesha medali zake' kuthibitisha yeye ni nani, ambapo mara kwa mara amekuwa akizibeba kwenye mizigo yake.
Farah, ambaye ushindi wake katika mbio za mita 5,000 na 10,000 umetoa matukio mawili ya kusisimua katika michezo iliyofanyika London mwaka 2012, amekuwa akifanya mazoezi nchini Marekani.
Baada ya kushindwa kufuzu kwa michezo ya Olimpiki mwaka 2008, alimhamishia mke wake, Tania na bintiye Rihanna mjini Portland kufanya kazi na kocha mkongwe Alberto Salazar katika makao makuu ya Nike.
Lakini mkimbiaji huyo alisema kwamba siku za nyuma alishakumbana na matatizo na maofisa wa mpakani.
Akidhani kwamba wadhamini wake Nike walishatatua viza yake ya ukaazi, Farah 'alilazimika kuondoka' Marekani huku akiwa anatumia viza ya kitalii.
Alisema: "Tulienda Toronto kukaa kwa siku chache, na kisha kurejea tena.
Lakini wakati tulipokuwa huko tulipata barua ikitueleza kwamba tuko chini ya uchunguzi kama tishio la ugaidi na tunatakiwa kuondoka kwa siku nyingine 90."
Farah amedai kwamba kocha wake Mmarekani alikuwa na 'rafiki yake anayefanya kazi FBI' ambaye alikuwa 'shabiki mkubwa'. Kwa mujibu wa mkimbiaji huyo, suala hilo 'limepatiwa ufumbuzi'.

No comments: