DISCO TOTO MARUFUKU DAR KRISMASI, MWAKA MPYA...

Watoto wakisakata muziki katika moja ya sikukuu kubwa za kitaifa kwenye ukumbi wa Msasani, Dar es Salaam.
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imejipanga kuhakikisha usalama wa kutosha unakuwepo katika msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, ili kukabiliana na uhalifu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema licha ya kuhakikisha ulinzi huo, pia haitaruhusiwa  disko toto kutokana na sababu za kiusalama kwani kumbi nyingi hazifai kwa mazingira ya watoto.
Aliwataka wazazi kutowaruhusu watoto wao kwenda kwenye madisko kwani kumbi nyingi hazina usalama mzuri na watoto hujaa na kusababisha kukosekana kwa hewa kulingana na kumbi zenyewe zilivyo.
“Tunataka kuhakikisha wananchi wanasherekea sikukuu hizi kwa amani na utulivu, kwani kwa uzoefu unaonesha mara nyingi kipindi hiki watu wenye nia ovu hujiandaa kufanya uhalifu,” alisema Kova.
Alisema wamejipanga kufanya doria katika maeneo mbalimbali ikiwemo sehemu za ibada, kumbi za starehe na maeneo yote ya jijini hapa.  Pia kuwawekea usimamizi watoto wao  wanapoenda ufukweni au kuwaacha nyumbani peke yao.
Alisema watafanya doria kwa kutumia magari, pikipiki, mbwa, farasi na kutumia vyombo vya kitaalamu kugundua viashiria vya uhalifu na watatumia boti kufanya doria kwenye fukwe za bahari pamoja na kufanya doria ya anga.
Kova amewataka askari wa Usalama Barabarani kutopokea rushwa kwa madereva na hasa wale wanaovunja sheria za Usalama Barabarani na kuwanyang’anya leseni madereva wa pikipiki watakaopakia watu wengi maarufu kama ‘mshikaki’.
“Wananchi wawe sehemu ya ulinzi wa mali zao na wasisite kutoa taarifa  wanapoona vitendo vya uhalifu au hata viashiria vya uhalifu, ili usalama uwepo kwa wananchi,” alisema Kova.

No comments: