BABU WA MIAKA 80 ALIWA NA MAMBA AKIOGA ZIWA VICTORIA...

Watu wawili wamekufa wilayani Bunda, mkoani Mara akiwemo mzee mmoja mwenye umri wa miaka 80 kuliwa na mamba wakati akioga ziwani, na mwingine amekufa maji katika Ziwa Victoria.
Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Igundu, Deus Kuliga, tukio la kwanza lilitokea juzi majira ya saa 5 asubuhi katika kisiwa cha Bwenyi, kilichoko ndani ya Ziwa Victoria eneo la kijiji cha Mchigondo, kata ya Igundu wilayani Bunda.
Katika tukio hilo, mzee mmoja Ujiya Geryo (80), mkazi wa kijiji cha Mchigondo aliliwa na mamba wakati akiwa anaoga ziwani.
“Wakati mzee huyo akioga ziwani ghafla mnyama huyo alitokea na kumkamata na kisha akazama naye kwenye kina kirefu cha maji” alisema.
Kuliga alisema kuwa wakati mzee huyo akioga ghafula mamba huyo alitokea na kumkamata na kisha akatokomea naye kwenye kina kirefu cha maji, ambapo juzi wananchi walifanikiwa kupata mabaki ya mwili wake ambayo ni mkono mmoja wa kushoto.
Aidha, alisema kuwa tukio la pili limetokea juzi katika kisiwa cha Bwenyi, ambapo mvuvi mmoja alikufa maji na wengeine watatu wakanusurika, baada ya mtumbwi wao ambao haukuwa na namba za usajiri kuzama baada ya kupigwa dhoruba ndani ya Ziwa Victoria.
Alimtaja mvuvi aliyekufa maji ambaye mwili wake tayari umepatikana kuwa ni Celestine Alphonce, mkazi wa kijiji cha Sikiro, wilayani hapa na kwamba wavuvi wengine watatu walinusurika baada ya kuogelea hadi nchi kavu.
Kuliga aliwataja wavuvi walionusurika kifo kuwa ni pamoja na Mapambo Maendeleo (18), Christopher Nyanja (20) na Frank Jifuna (21), ambao wote ni wakazi wa kijiji cha Sikiro wilayani hapa.
Ofisa Mtendaji alisema kuwa matukio yote mawili yameripotiwa katika kituo kidogo cha polisi Kibara, ambapo pia mganga mkuu wa zahanati ya kata ya Igundu, Maico Karoje, alithibitisha vifo hivyo, ikiwa ni pamoja na kufanyia uchunguzi miili ya marehemu.

No comments: