WABUNGE WATAKA MAFISADI WOTE WANYONGWE...

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wameelezea kukerwa kwao na vitendo vya ufisadi miongoni mwa viongozi na watumishi wa umma na kutaka Katiba ijayo itamke kuwa, adhabu yao iwe ni kunyongwa.
Aidha, wamechachamalia uchaguzi mdogo, wakitaka usiwepo kwa kuwa una gharama kubwa na hivyo kuibebesha Serikali mzigo, huku wengine wakiendelea kulia na kitendo cha Mawaziri kuwa wabunge, wakitaka mawaziri wasitokane na wabunge, lengo likiwa kuongeza uwajibikaji.
Waliyasema hayo jana mjini hapa mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Waziri Mkuu wa zamani Jaji Joseph Warioba.
Mbali ya masuala hayo, wabunge hao pia walieleza kutofurahishwa na mfumo wa sasa wa kuwapo kwa wabunge wa Viti Maalumu, baadhi wakitaka vifutwe na wengine wakishauri wapewe nafasi ya kuanzia majimboni, lakini kwa kushindanishwa na wanawake wa vyama vingine.
Suala la umri wa Rais nalo lilichukua nafasi, wengine wakitaka umri wa kugombea uanzie miaka 35, badala ya 40 ya sasa.
Akichangia suala la ufisadi, Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi) alisema viongozi mafisadi wanastahili kunyongwa kwa kuwa nao ni wauaji na hawajui haki za binadamu, hivyo hawana sababu za kulindwa na Katiba kwa kizingizio cha haki za binadamu.
“Nashauri viongozi wa aina hii ni wauaji, wahujumu uchumi na watu wasiofaa katika jamii, hawa wanyongwe. Tusishabikie haki za binadamu wakati wenyewe hawajui haki, jiulize mtu anayepewa fedha za kununua dawa au maji ili zisaidie wengi katika jamii, anapokula fedha hizo si anataka kuua na kutesa raia wema? Kama anafanya hivi kwa nini naye asinyongwe?” alihoji.
Aidha, mchangiaji mwingine, Nyambari Nangwine ambaye ni Mbunge wa Tarime kwa tiketi ya CCM, alitaka mafisadi na watoa rushwa wanyongwe kwa kuwa ni hatari kwa umoja na mshikamano wa wananchi, kwa kuwa wanatengeneza makundi katika jamii.
Aidha, baadhi ya wabunge wamechachamalia uchaguzi mdogo, wakisema hauna maana kwa kuwa unaibebesha Serikali gharama kubwa.
Miongoni mwa waliotoa maoni hayo ni mwanasiasa mkongwe, Kapteni John Chiligati, Mbunge wa Manyoni Mashariki wa tiketi ya CCM aliyesema haamini kama uchaguzi mdogo una umuhimu wowote kulinganisha na gharama kubwa za kufanya aina hiyo ya uchaguzi.
Wengine waliosema hayo  ni Murtaza Mangungu wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, Mwigulu Nchemba wa Iramba Mashariki ambaye pia ni Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM-Taifa.
“Katika Katiba mpya, nashauri kuwe na Serikali mbili kama ilivyo sasa, kuwe na wagombea wawili mmoja wa kike na mwingine wa kiume, ikitokea mmoja amefariki dunia au tatizo jingine lolote, basi mwingine aendelee kuwawakilisha wananchi na pasifanyike uchaguzi mdogo, kwani ni
gharama,” alisema.
Aidha, alisema mfumo huo utasaidia kutengeneza uwiano mzuri wa idadi ya wanawake na wanaume bungeni, huku akishauri Katiba pia itoe nafasi ya mwanamke kushika moja ya nyadhifa tatu za juu Serikali. Nafasi hizo ni Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu.
Mbali ya kukataa uchaguzi mdogo, kwa asilimia kubwa wabunge walikataa Viti Maalumu, wakiwemo mfumo wa sasa hauwapi heshima, hivyo kutaka wapewe majimbo ili wapigiwe kura na wananchi, ikiwa ni nafasi maalumu itakayoshindanisha wanawake, achilia mbali ile itakayowaniwa na wabunge wanaume majimboni.
Kuhusiana na umri wa kugombea Rais, idadi kubwa walipendekeza uanzie miaka 35, kwa kuwa katika umri huo wengi wanakuwa wameshaiva kiutendaji na pia wanakuwa na nguvu za kuwatumikia wananchi.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy (CCM) alisema umri wa miaka 35 ni sahihi na usizidi miaka 55, akisema taifa linahitaji wagombea wenye nguvu, na si wenye umri mkubwa ambao kila kukicha hupelekwa nje kwa matibabu au uchunguzi wa afya.
Alitaka pia Katiba iwabane waliostaafu utumishi wa umma, akisema wasiruhusiwe kugombea ubunge au udiwani akisema wengi wamegeuza sehemu ya ajira, ilhali walishalipwa mafao yao, lakini wanakimbilia bungeni ambako huishia kusinzia.
Aidha, alipendekeza ukomo wa ubunge au udiwani uwe wa mihula miwili ya miaka mitano mitano.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangallah (CCM), Mbunge wa Viti Maalumu, Leticia Nyerere (CCM), Agripina Buyogera wa Kasulu Vijijini (NCCR- Mageuzi), Dk. Pudenciana Kikwembe wa Viti Maalumu-CCM, nao walipendekeza umri wa kuwania urais uwe miaka 35.
Licha ya wengi kutaka wabunge wasiwe Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa, walisema pia kwamba sasa ni wakati mwafaka wa kuachana na mawaziri ambao ni wabunge, na badala yake wateuliwe kutoka nje ya mfumo huo, kama ambavyo wametaka majaji nao wasiteuliwe na Rais, bali wapiti mchujo maalumu utakaowashirikisha wananchi na baadhi wapitishwe na Bunge.
Mmoja wa wachangiaji hao, Deogratius Ntukamazina, Mbunge wa Ngara kwa tiketi ya CCM alisema kama wabunge watakaopata uwaziri, Katiba iwatake ama kujiuzulu au kukataa.
“Hii itasaidia uwajibikaji kwa mawaziri. Huyu wakati mwingine tunaoneakana haya hata kama tunaona mambo hayaendi vizuri,” alisema na kutaka Majaji nao washindanishwe kuwania nafasi hizo, badala ya kuteuliwa na Rais, huku akishauri kuwe na mabunge mawili, likiwamo la Seneti litakalowashirisha viongozi wastaafu, lengo likiwa kuchota busara na uzoefu wao wa uongozi.
Kuhusiana na suala la elimu, alishauri wabunge wawe na elimu ya kuanzia shahada ya kwanza na madiwani wasiwe na elimu ya chini ya kidato cha nne.
Suala la Zanzibar kutaka mafuta yaondolewe katika suala la Muungano, nalo liliibuka, na baadhi ya wanasiasa wakongwe, Steven Wassira na Chiligati wakitaka Katiba ibariki kuwa yatakapopatikana, yawe mali ya Zanzibar ili kupunguza malalamiko juu ya masuala ya muungano.
Aidha, wabunge kadhaa waliridhia muundo wa sasa wa Muungano uendelee, wengine wakitaka Serikali tatu, kama ilivyo kwa Esther Bulaya, Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya CCM na Mbunge wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa (CUF) ambako kwa kiasi fulani walionekana kutofautiana na misimamo ya vyama vyao, mathalani CCM ni muumini wa Serikali mbili, muundo uliopo sasa wa Muungano.

No comments: