SHEKHE PONDA NA SHEKHE FARID WARUDISHWA RUMANDE...

Shekhe Ponda Issa Ponda akiwa mahakamani Kisutu.
Hati maalumu za wakurugenzi wa mashitaka Zanzibar na Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania, zimeendelea kuwaweka rumande Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar, Shekhe Farid Hadi Ahmed na Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Shekhe Ponda Issa Ponda.
Jana katika Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe Zanzibar, masharti ya dhamana ya Shekhe Farid na washitakiwa wenzake katika kesi ya uchochezi na kufanya fujo inayowakabili, yalitolewa na Hakimu Ame Msaraka Pinja.
Hata hivyo, kama angeyatimiza, hati maalumu ya Mkurugenzi wa Mashtaka  Zanzibar kupinga dhamana ya Shekhe Farid na wenzake katika kesi nyingine inayomkabili katika Mahakama Kuu ya Vuga, ilitosha kumrudisha rumande.
Katika masharti yaliyotangazwa jana na Hakimu Pinja, Shekhe Farid na wenzake walitakiwa kuwasilisha mahakamani Sh milioni moja taslimu kwa kila mmoja pamoja na kuwa wadhamini watatu ambao ni watumishi wa Serikali kwa kila mmoja na wawasilishe barua za kutambulishwa na waajiri wao na vivuli vya vitambulisho vyao vya kazi.
Pia wadhamini hao kila mmoja alitakiwa kuweka dhamana ya Sh milioni moja, kuwasilisha barua kutoka kwa Sheha wa Shehiya anayoishi na kivuli cha vitambulisho vya ukazi na kwa wenye hati za kusafiria pia wawasilishe vivuli vya hati hizo.
Washitakiwa wengine wanaokabiliwa na mashitaka hayo pamoja na Shekhe Farid ni pamoja na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uamsho, Shekhe Mselem Ali Mselem, Mussa Juma Issa, Azan Khalid Hamdani, Khamis Ali Suleiman na Hassan Bakari Suleiman.
Mbali na hati maalumu ya Mkurugenzi wa Mashtaka  Zanzibar kupinga dhamana zao katika kesi nyingine kwenye Mahakama Kuu ya Vuga, washitakiwa hao pia walishindwa kutimiza masharti ya dhamana katika kesi inayowakabili katika Mahakama ya Mwanakwerekwe.
Awali kabla ya washitakiwa hao kurejeshwa rumande, mawakili wao wakiongozwa na Abdalla Juma na Salum Toufiqi waliiomba mahakama kutoa agizo la kuwapa haki zinazostahili wateja wao, ikiwamo askari wa Magereza kuruhusu mahabusu hao waonane na familia zao na wapewe chakula kizuri.
Mawakili hao pia walitaka wateja wao wawekwe katika chumba kimoja na kupinga utaratibu wa kuwaweka kila mtu na chumba chake.
“Tunasikitika sana, si haki na inaonekana wazi kwamba askari wa vyuo vya mafunzo (Magereza) wanapindisha sheria ikiwamo kuwanyima haki ya kuonana na mawakili wao,” alidai Wakili Juma.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Novemba 21 itakapotajwa na washitakiwa leo wanatazamiwa kufikishwa katika Mahakama ya Vuga kujibu mashitaka matatu mengine, ikiwamo la uharibifu wa mali, kushawishi na kuchochea, kurubuni watu kufanya fujo na kula njama ya kujificha kwa Shekhe Farid.
Shekhe Azan atasomewa mashitaka pekee yake ambayo ni ya uvunjifu wa mali pamoja na kumshambulia kwa maneno makali Kamishna wa Polisi.
Wakati Shekhe  Ponda akiendelea kusota rumande kwa kunyimwa dhamana na hati ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),  wafuasi wake 49  wanaokabiliwa na mashitaka ya uchochezi na wizi wa mali zenye thamani ya Sh  milioni 59 wamepata dhamana.
Washitakiwa hao walipata dhamana baada ya kukamilisha masharti yaliyowataka kuwa na mdhamini mmoja anayefanya kazi katika taasisi inayofahamika, atakayesaini hati ya Sh milioni moja.
Hakimu Victoria Nongwa wa Mahakama ya Hakimu Kisutu alitoa dhamana hizo juzi kwa washitakiwa 19 na jana washitakiwa 30.
Washitakiwa walifikishwa mahakamani hapo wakiwa chini ya ulinzi wakisindikizwa na magari saba ya Polisi likiwamo gari la maji ya kuwasha, na kila aliyeingia mahakamani hapo alikuwa akikaguliwa kwa kifaa maalumu kinachobaini kama amebeba silaha.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matano ya kula njama na kuingia kwa nguvu na kujimilikisha kiwanja kinachomilikiwa na kampuni ya AgriTanzania  Ltd, kilichopo katika eneo la Chang’ombe Markasi na kisha kuiba mali zenye thamani ya Sh milioni 59.7. 
Aidha, katika mashitaka ya uchochezi yanayomkabili Shekhe Ponda peke yake, inadaiwa katika eneo hilo kwa maelezo kuwa yeye ni Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu (T) alishawishi  wafuasi wake ambao ni washitakiwa hao kutenda makosa hayo.
Katika hatua nyingine Salum Shaban, Salum Mkuraga, Ernest Sylvester, Josephat Aloyce, Edwin Sadoki, Stanley Nhonya, Athuman Sajuki, Thabit Kombo, Abdully Rashid, Sadick Mustapha, Niga Ndinganya wamefikishwa mahakamani hapo wakishitakiwa kufanya mkusanyiko bila kibali.
Wakili wa Serikali Shedrack Kimaro alidai mbele ya Hakimu Liad Chamshana kuwa Novemba 2 mwaka huu katika Msikiti wa Idrisa uliopo mtaa wa Tandamti, washitakiwa hawakutii amri ya askari iliyowataka wasifanye mkusanyiko wa aina yoyote.
Aliendelea kudai kuwa, siku hiyo washitakiwa walifanya mkusanyiko usio halali wenye lengo la kuvunja amani. Washitakiwa walikana mashitaka na kurudishwa rumande baada ya kukosa wadhamini na kesi hiyo itatajwa Novemba 20 mwaka huu.

No comments: