PEDESHEE PAPAA MSOFE ALALAMIKIA KESI YAKE KUCHELEWESHWA...

Marijani Msofe 'Papaa Msofe' alipokuwa akiingia mahakamani kusikiliza kesi yake.
Upande wa utetezi katika kesi ya mauaji inayomkabili mfanyabiashara maarufu Dar es Salaam, Marijani Msofe (50) maarufu Papaa Msofe, umeulalamikia upande wa mashitaka kuchelewesha upelelezi wa kesi hiyo.
Wakili wa Msofe, Richard Rweyongeza alidai hayo jana mbele ya Hakimu Agness Mchome wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Alidai tangu mteja wake alipokamatwa, polisi wamelala na hawafanyi kazi yoyote na kwamba ndiyo maana upelelezi wa kesi hiyo unachelewa.
Alidai kuwa mshitakiwa alikamatwa mwaka mmoja baada ya kufanyika kwa tukio hilo, lakini mpaka sasa upelelezi haujakamilika.
Hakimu Mchome alisema ili kuepusha maneno na malalamiko kila jambo linalofanyika liwe wazi kwa mahakama kwa sababu kutoa taarifa kunaonesha uwajibikaji.
Akikubali hoja za Wakili Rweyongeza, Hakimu aliamuru upande wa mashitaka kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo. Kesi hiyo itatajwa tena Novemba 13 mwaka huu.
Inadaiwa kuwa Novemba 6 mwaka jana katika eneo la Magomeni, Msofe alimuua  Onesphory Kitoli jambo ambalo ni kinyume na kifungu cha 196 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.
Kwa mara ya kwanza Msofe alifikishwa mahakamani hapo Agosti 10 mwaka huu, hata hivyo hakuruhusiwa kujibu mashitaka kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa Mahakama Kuu.
Shauri hilo limefunguliwa mahakamani hapo katika hatua ya upelelezi na baadaye itahamishiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

No comments: