MBUNGE MUSSA AZZAN ZUNGU WA CCM ATIWA MBARONI KWA RUSHWA...

Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu.
Mbunge wa Ilala kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Azzan Zungu ni miongoni mwa watu waliotiwa mbaroni mkoani hapa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) baada ya kubambwa wakigawa fedha kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM.
Zungu, ambaye alikuwa mgombea wa nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupitia jumuiya hiyo katika uchaguzi uliofanyika jana, alikamatwa katika Hoteli ya Golden Crown akiwa na wapambe wake watatu usiku wa kuamkia juzi, akidai kutoa rushwa kwa wajumbe ili wampigie kura.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Eunice Mmari alisema Zungu ameachiwa kwa dhamana huku uchunguzi ukiendelea na atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi huo kukamilika.
Mmari aliwataja waliokamatwa wakiwa na Zungu kuwa ni Yahya Danga, Busolo Pazi na Frank Magati.
Akielezea tukio hilo, Mmari alisema waliweka mtego kwenye hoteli hiyo na Zungu alikwenda kwenye bustani ambako kulikuwa na wajumbe na wakati huo alikuwa ndani ya gari ndogo aina ya Mark II na alikuwa akizungumza kwa kuwashawishi wajumbe ili wamchague huku gari nyingine aina ya Prado likiwa karibu na hapo.
Kamanda huyo alidai Prado lilikuwa na fedha za kugawia wajumbe na baada ya wachunguzi wa Takukuru kuvamia gari la Zungu, Prado ilitoweka haraka na hivyo hawakukamata fedha hizo kama ushahidi.
“Zungu alikuwa na wapambe watatu na mmoja wa wapambe hao alikuwa akitaja kiwango cha kuwalipa wajumbe, tunaendelea na uchunguzi, ukikamilika wote watafikishwa mahakamani,” alisema Mmari.
Pia Mmari alisema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Mbeya, Fatuma Kasenga na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Wazazi Taifa, alikamatwa usiku wa kuamkia jana akiwa analipia baadhi ya wajumbe  wa mkutano huo chakula na vinywaji.
“Inaaminika kuwa huo ulikuwa ni ushawishi wa wajumbe hao, mmoja wa wagombea katika uchaguzi huo alikamatwa katika nyumba ya kulala wageni ya Kitoli iliyopo eneo la Barabara ya Iringa,” alisema.
Zungu alikuwa Mwenyekiti wa Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam katika miaka mitano iliyopita, na pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Hakupatikana jana kuzungumzia suala hili, kwani simu zake zote za mkononi hakuwa anazipokea.
Kamanda Mmari alisema Takukuru imekuwa ikifuatilia vitendo vya rushwa katika uchaguzi huo.
Alisema mtuhumiwa mwingine ambaye wanaendelea kumfanyia uchunguzi ni aliyekuwa akigombea nafasi ya Mjumbe wa Baraza Kuu la Wazazi Taifa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Dk Damas Mukasa ambaye alikamatwa Oktoba 8, mwaka huu nje ya Ukumbi wa Kilimani mjini hapa kwa kosa la kutoa rushwa kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu ili wampigie kura.
Mmari alisema wajumbe wawili wa mkutano huo walikamatwa kwa kosa la kupokea rushwa kutoka kwa Dk Mukasa ambaye alitumia mbinu ya kutoa fedha hizo kupitia kwa wauza nguo waliokuwa wakifanya biashara nje ya ukumbi huo wa mkutano.
Aidha, Mmari aliwatahadharisha wajumbe wa Mkutano Mkuu kuwa makini kwani Takukuru wamejipanga kuhakikisha wanakamata wale wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.
Alisema baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo ni wajumbe kushirikiana na wagombea na wapambe wao katika vitendo vya rushwa na hivyo kukosa ushirikiano; tabia ya wananchi kuona vitendo vya rushwa vikiendelea bila kuchukua hatua zozote huku baadhi ya vitendo vya rushwa vikifanyika ndani ya nyumba za wajumbe usiku wa manane, kulingana na wingi wa wajumbe inakuwa shida maofisa kuwapo kila eneo.
Hivi karibuni, wakati akifunga Mkutano Mkuu wa UWT, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete alielezea kukerwa na rushwa katika uchaguzi wa CCM na kushangazwa na hatua ya wanawake nao kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Katika kufungua Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM), Rais Kikwete alirejea pia suala hilo la rushwa na kuwataka vijana hao kuiondolea aibu CCM kwa kuchagua viongozi wasiotoa rushwa.
Lakini licha ya kauli zake kumekuwapo na kelele kutoka kwa umma, na wanachama na wapenzi wa CCM wakitaka matokeo ya uchaguzi wa UWT Taifa na UVCCM Taifa yafutwe.
Katika hatua nyingine, matokeo ya awali ya kura katika uchaguzi wa Wazazi Taifa yanaonesha kuwa kada maarufu wa chama hicho, Abdallah Bulembo ndiye aliyekuwa akiongoza dhidi ya wapinzani wake, Katibu wa CCM wa Mkoa mstaafu John Barongo na Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata.

No comments: