MKURUGENZI MTENDAJI ALIYESIMAMISHWA TANESCO ATIMULIWA KAZI...

William Mhando.
Hatimaye Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), imetangaza kumwachisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, William Mhando kuanzia Oktoba 29, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Bodi hiyo, Mhando ameachishwa kazi kwa sababu ya kukiuka taratibu za shirika na matumizi mabaya ya madaraka.
Taarifa iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco, Robert Mboma, ilieleza kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya uchunguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kubaini tuhuma zilizoelekezwa kwa Mhando kuwa ni za kweli.
“Kufuatia tuhuma mbalimbali za ukiukwaji wa taratibu za Shirika ikiwemo matumizi mabaya ya mamlaka, mnamo tarehe 16, Julai 2012, Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania, Shirika liliamua kumsimamisha kazi pamoja na maofisa wengine waandamizi, Mkurugenzi Mtendaji, Mhandisi William Geoffrey Mhando kwa nia ya kupisha uchunguzi huru na wa haki ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo.
“Baada ya hapo, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Mashirika ya Umma ilifanya uchunguzi ili kubaini ukweli juu ya tuhuma zilizokuwa zinamkabili Mhandisi William Geoffrey Mhando ambapo katika uchunguzi huo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Mashirika ya Umma, aligundua kuwepo kwa ushahidi wa dhahiri wa ukiukwaji wa taratibu za Shirika na matumizi mabaya ya madaraka dhidi ya Mkurugenzi Mtendaji, Mhandisi William Geoffrey Mhando,” ilieleza taarifa ya Mwenyekiti wa Bodi.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa baada ya kupokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bodi ya Tanesco iliteua jopo la watu watatu ili kusikiliza utetezi wa Mhando dhidi ya tuhuma mbalimbali zilizoibuliwa na CAG.
“Baada ya kusikiliza, jopo hilo lilimkuta Mhandisi William Geoffrey Mhando na hatia dhidi ya makosa yanayohusiana na ukiukwaji wa taratibu za Shirika ikiwemo mgongano wa maslahi,” ilieleza taarifa hiyo.
Ilieleza kwamba pamoja na yote hayo, Bodi ilikutana Oktoba 29, mwaka huu, na kujiridhisha kuwa Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Tanesco alifanya makosa yanayohusiana na kuingia kwenye mikataba yenye mgongano wa kimaslahi kinyume na taratibu za shirika.
“Hivyo basi, kufuatia hayo, Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO iliamua kumwachisha kazi Mhandisi William Geoffrey Mhando kuanzia tarehe 29.10.2012,” ilieleza taarifa hiyo ya Mwenyekiti Mboma.
Mapema wiki hii, Jumatatu na Jumanne, Tanesco ilikuwa imeita vyombo vya habari ofisini kwake kwa ajili ya kuzungumza na vyombo vya habari, lakini ikaahirisha mara zote huku habari zikianza kuvuja kwamba kulikuwa na maamuzi mazito kuhusu hatima ya Mkurugenzi Mtendaji Mhando.
Wakati wa Bunge la Bajeti, Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alimtuhumu Mhando kutumia madaraka yake vibaya kwa kutoa kazi kwa Kampuni ya Santa Clara ambayo inadaiwa kuwa ya mkewe mkurugenzi huyo, jambo ambalo lina mgongano wa maslahi.
Aidha, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliituhumu Tanesco chini ya uongozi wa Mhando, kwa kununua nguzo za umeme mkoani Iringa na kisha kuzipeleka Mombasa nchini Kenya, kabla ya kuziingiza tena nchini, na kuuzwa kwa Tanesco kwa bei ya Afrika Kusini.
Pia chini ya uongozi wa Mhando, Tanesco inatuhumiwa kuagiza vipuri kutoka nje ya nchi, lakini mzigo ulipofikishwa nchini, iligundulika kwamba lilikuwa ni kasha la misumari.
Mbali ya Mhando, wengine waliokuwa wamesimamishwa kupisha uchunguzi wa CAG ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi katika Ununuzi, Harun Mattambo. Hatima yao haikuelezwa katika taarifa ya jana.

No comments: