KIMBUNGA SANDY CHAFUKUA MAKABURI NA KUACHA MAJENEZA NJE...

Baada ya kuwa imesawazisha karibu eneo lote linalozingira Jiji la New York na Pwani ya Mashariki huku ikifanya uharibifu mkubwa katika eneo hilo Jumatatu usiku, kimbunga cha Sandy kimeondosha udongo na kusababisha majeneza kuchomoza kutoka kwenye makaburi yalimofukiwa.
Kwenye makaburi mjini Crisfield, Maryland, majeneza mawili, moja la shaba na jingine fedha, yalichomoza kutoka ardhini kufuatia mafuriko ya maji yaliyopita kasi kubwa yaliyosababishwa na kimbunga cha Sandy kuchimba udongo.
Yalikuwa na nguvu kubwa kiasi cha kubomoa kuta za saruji zilizokuwa zimefunika makaburi hayo.
Kimbunga kikubwa kilichosababisha uharibifu mkubwa kuwahi kutokea katika miongo kadhaa kimeikumba miji ya Marekani yenye wakazi wengi zaidi na kuathiri watu na viumbe huku ikikata mawasiliano ya kisasa na kuwaacha mamilioni ya watu bila nishati ya umeme na maelfu waliokimbia nyumba zao zilizoharibiwa na mafuriko wakijiuliza lini, na kama maisha yao yatarejea katika hali ya kawaida.
Kimbunga cha Sandy kimeua takribani watu 50, wengi wakipoteza maisha kutokana na kuangukiwa na miti, na bado hakijaisha. Kimeshambulia nchi kavu maeneo yote ya Pennsylvania kuelekea magharibi mwa New York kumwaga sehemu kubwa ya maji yake na kwamba ilitarajiwa kusababisha uharibifu mkubwa juzi usiku.
Meya wa Mji wa New York Michael Bloomberg alisema anatathmini uharibifu katika jiji lake.
Zaidi ya wakazi milioni 8.2 wamekosa huduma ya umeme katika majimbo 17 kuelekea magharibi hadi Michigan.
Karibu milioni mbili kati ya hao walikuwa New York, ambako sehemu kubwa walikosa umeme na mitaa yote iliishia kuzingirwa na maji - kama ilivyotokea kwenye njia saba za treni za chini kwa chini ya kati ya Manhattan na Brooklyn kwa upande mmoja.
Soko la Hisa la New York lilifungwa kwa siku ya pili kutokana na hali ya hewa, hii ikiwa ni mara ya kwanza kutokea tangu dhoruba kali ya theluji mwaka 1888.

No comments: