KAMBA ZA PAZIA ZAMNYONGA BINTI MTOTO WA BILIONEA...

KUSHOTO: Bilionea wa Norway, Morten Hoegh. KULIA: Mapazia kama haya ndiyo yamechukua uhai wa mtoto Alexandra.
Binti mwenye miaka miwili wa mmoja wa matajiri Uingereza amekufa baada ya kukutwa akiwa katundikwa kwenye kamba za pazia ndani ya kitanda chake kidogo.
Alexandra Lucy Hoegh aligunduliwa na mama yake aliyejawa hofu Dana, ambaye alikimbia nje ya nyumba yao ya familia yenye thamani ya Pauni za Uingereza milioni 12 iliyoko Notting Hill akipiga kelele: "Jamani nisaidieni, mtoto hapumui".
Mtoto huyo ni binti wa tajiri wa meli na mafuta mwenye asili ya Norway, Morten Hoegh, ambaye anaendesha kampuni yake yenye utajiri wa mabilioni ya Pauni kati ya miji ya London na Oslo.
Madaktari walifika eneo la tukio huko magharibi mwa London lakini mtoto huyo akafariki wakiwa njiani kumpeleka hospitali Jumatatu.
Kifo chake kimeangazia hatari iliyoko katika mapazia ya kamba, huku mtoto huyo akiwa ni mmoja kati ya takribani watoto kumi waliokufa kwa namna hiyo tangu mwaka 2010.
Polisi amesema Alexandra anawezekana kuwa alisokotwa kwenye kamba na kupata matatizo ya moyo, akiongezea kuwa wanachukulia kifo chake kuwa cha kawaida.
Mama yake mwenye miaka 37, Dana, ambaye anatokea Marekani, alipelekwa hospitali kwa matibabu kutokana na mshituko.
Morten mwenye miaka 39, ni mwenyekiti wa kampuni tajiri ya usafirishaji mafuta na gesi yenye makao yake makuu Norway ya Hoegh LNG.
Anatambulika kuwa ni mmoja kati ya watu matajiri zaidi nchini Uingereza mwenye utajiri unaokadiriwa kufikia Pauni za Uingereza milioni 175 na kuorodheshwa kwenye Listi ya Matajiri katika gazeti la Sunday Times.
Wawili hao pia wana mtoto wa kiume mwenye miaka sita, Morten na binti wa miaka mitano Henrietta.
Jirani mmoja ameeleza: "Hakujua (Dana) la kufanya. Hakika ni janga.
"Mama huyo alitoka nje akipiga kelele mtaani.
"Alisema mtoto alikuwa anakufa na kwamba alikuwa akihitaji msaada kuokoa maisha ya mtoto huyo. Gari la wagonjwa liliwasili na madaktari walikimbilia ndani."
Mkazi mwingine alisema: "Ni tukio la kuhuzunisha. Ingeweza kuwa rahisi kujilaumu mwenyewe, lakini kwa huzuni ajali hutokea.
"Nilisikia vurumai kubwa.
"Nilipotoka mlangoni kulikuwa na gari la wagonjwa nje."
Rafiki wa familia hiyo alisema: "Dana na Morten ni wanandoa wa kushangaza.
"Alexandra alikuwa binti mzuri mno kuwahi kukutana naye.
"Hakika siwezi kuamini hiki kilichotokea."
Takwimu za kushitusha zinaonesha kumekuwa na vifo takribani 22 vinavyosababishwa na mapazia ya kamba tangu mwaka 1999, nusu ya matukio hayo yakiwa yametokea tangu kuanza kwa mwaka 2010.
Takwimu hizo zinashawishi wanaharakati wa usalama kushinikiza kupigwa marufuku mapazia ya aina hiyo.
Wataalamu wa Usalama wamesema kwamba karibu watoto wawili kwa mwaka wanakufa kutokana na mapazia hayo ya kamba nchini Uingereza.
Sheila Merrill, meneja usalama majumbani kutoka Taasisi ya Kuzuia Ajali alisema: "Ushauri wetu ni kutundika kamba za mapazia hayo juu mbali sehemu wasiyofikia watoto wadogo au kukata kitanzi hivyo kuning'inia katika ncha mbili."

No comments: