WATAKA KATIBA ISEME MWISHO WA UBUNGE...

Wabunge wakiwa katika moja ya vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano mjini Dodoma, hivi karibuni.
Suala la ukomo wa muda wa madaraka kwa wagombea wote wa uongozi katika nafasi zao limeibuka katika utoaji maoni ya Katiba mpya ambapo imependekezwa nafasi za uwakilishi kisiasa ziwe na ukomo.
Akitoa maoni yake mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba juzi mkazi wa Ngangamfumuni, Moshi mjini, Philip Senga alipendekeza Katiba mpya iweke muda wa miaka 10, kwa wanasiasa wakiwamo madiwani na wabunge kukaa madarakani kama ilivyo kwa Rais.
Alifafanua, kwamba miaka mitano ya awali, iwe ya kujadiliwa na mitano iwe ya utendaji. "Tunataka wabunge na madiwani wawe na ukomo wa vipindi vya kuwa kwenye nafasi hizo, si wengine tangu vijana hadi wamezeeka bado ni wabunge, sasa vijana watapata wapi kazi ilhali wengine wamezihodhi?" Alihoji Senga.
Aidha, alipendekeza Azimio la Arusha lirudishwe kwenye Katiba ili kurejesha heshima  ya viongozi na watawala  na kwamba watendaji wasiotekeleza majukumu yao nao wawajibishwe kwa mujibu wa Katiba.
Anna Kisaka alipendekeza Katiba mpya iweke mfumo bayana wa wabunge kulipwa mishahara
kulingana na sifa na viwango vya elimu waliyonayo, ili kuleta usawa kwa watumishi wote nchini.
Alisema kama Katiba itaweka mfumo huo, ni wazi hakutakuwa na upendeleo wa mishahara, kwani mfumo wa sasa wa wabunge ni kupata mshahara unaofanana, ingawa wametofautiana sifa za elimu na taaluma zao.
Alifafanua, kuwa hivi sasa inaonekana mbunge hata mwenye elimu ya msingi, anamzidi mshahara daktari au mwanasheria.
"Mimi nataka Katiba mpya iweke ngazi ya mishahara ya wabunge kulingana na sifa za elimu walizonazo, si mbunge wa darasa la saba amzidi mshahara daktari ambaye amesoma chuo zaidi ya miaka saba, si sahihi hata kidogo," alisema Kisaka.
Aliongeza, kama utakuwapo mfumo huo wa ngazi za mishahara, ni wazi hata wananchi wataona usawa kwani hivi sasa kila mtu anataka kuwa mbunge, kwa kuwa anafahamu hata kama hana elimu, akifanikiwa kuwa mbunge atakuwa na mshahara mzuri.
Aidha, alisema suala la wabunge kuwa wakuu wa mikoa lipigwe marufuku kwenye Katiba ijayo, kwani ni kuwanyima fursa vijana na watu wengine wenye sifa za kupata ajira badala yake wachache kuhodhi madaraka mengi.
Mkazi wa Kata ya Kiusa, Abdalah Kahumba alipendekeza Katiba ijayo iweke bayana kipengele cha wagombea wa nafasi za kisiasa kupeperusha bendera ya Taifa badala ya zile za vyama.
"Nataka Katiba mpya itamke hivyo, hawa wagombea kupeperusha bendera za vyama vyao ni kukosa uzalendo na nchi yao na hiyo inaonesha dhahiri kwamba ni suala la maslahi binafsi na si la Taifa," alisema Kahumba.
Alisema  kufanya hivyo kutatanguliza uzalendo na kwamba zipo baadhi ya nchi kwenye kampeni zao wanatumia bendera za mataifa na kwamba hicho ni kielelezo kwamba maslahi ya nchi ni bora kuliko ya vyama.

No comments: