WANAOTUMIA ARVs WATISHIA KUISHITAKI SERIKALI...

Waziri wa Afya, Dk. Hussein Mwinyi
Baadhi ya wananchi wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) mkoani Rukwa wametishia kuwasiliana na wanasheria wao ili waweze kuwashtaki mahakamani wote waliobainika kuhusika kusambazwa kwa Dawa za Kupunguza Makali ya Ukimwi (ARVs) ambazo ni bandia ili washtakiwe na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Wamewafananisha wote hao kuwa ni sawa na wauaji na wanastahili kushitakiwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Kiongozi wa chama cha watu wanaoishi na VVU (Shidepha+) Mkoa wa Rukwa, Salum Korongo aliyasema hayo jana wakati akizungumza mjini hapa, huku akiwahimiza wanaotumia ARVs kupima CD4 zao ili kubaini kama nao wameathiriwa kwa kutumia dawa hizo bandia ili hatua za kisheria dhidi ya wote wanaotuhumiwa ziweze kuchukuliwa.
"Mimi nilipata mshtuko mkubwa sana kwani ninatumia ARVs na CD4 zangu zimepanda na kufikia 1,890 hivyo kama nitakuwa nimetumia dawa hizo bandia lazima zitadhoofisha CD4 zangu.
"Tumejipanga kwenda kupima hizo CD4 zetu na tukibaini kuwa zimeathirika basi tutawasiliana na Mwanasheria wetu ili wote wanaotuhumiwa na kashfa hii washughulikiwe, sisi tunawafananisha na wauaji tutawashtaki ili hatua kali dhidi yao ziweze kuchukuliwa, " alisema.
Baadhi ya wanaoishi na VVU wanaotumia dawa hizo za kupunguza makali ambao hawakuwa tayari majina yao yaandikwe walidai kuwa baada ya kutumia dawa hizo kwa miezi miwili sasa wamepatwa na hofu kubwa baada ya kujikuta baadhi ya magonjwa nyemelezi yaliyokuwa yamedhibitiwa kwa kutumia dawa hizo sasa yameanza kuwashambulia tena.
"Hofu kubwa ninayo maana sasa hata magonjwa nyemelezi yameanza kunishambulia tena wakati nilikuwa nimeyadhibiti kwa kunywa dawa hizo sasa sijui, labda inawezekana dawa nilizokuwa nakunywa hivi karibuni ndizo hizi wanazodai kuwa ni bandia…najipanga kwenda kupima CD4 zangu nione kama zimedhoofika," alisema mmoja wao.
Hata hivyo, kwa mujibu wa kiongozi wa Shidepha + mkoani humo, Korongo alikiri kuwa hana hakika kama dawa zilizokuwa zikisambazwa katika vituo vya afya katika Manispaa ya Sumbawanga na kwingineko mkoani humo zilikuwa za bandia au la.
Kauli hizo zimekuja siku chache baada taarifa za kusambazwa kwa ARVs bandia ambazo zilibainika Agosti kwenye Hospitali ya Wilaya ya Tarime, huku Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi likidai kuwa dawa hizo zimesambazwa katika mikoa ya Mara, Tanga na Dar es Salaam tofauti na kauli ya Serikali kuwa ni Tanga, Iringa na Mwanza.
Katika hatua nyingine, baadhi ya watu wanaodaiwa kuishi na VVU mkoani hapa wameipongeza Serikali kwa jitihada zake makusudikwa kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Joseph Mgaya kwa tuhuma za ununuzi wa dawa bandia za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kuwa hofu ilikuwa imewatanda juu ya mustakabali ya maisha yao ambapo walichukua fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa jitihada zake hizo za kuingilia katika na kumchukulia hatua za hiyo ya kinidhamu Mkurugenzi huyo wa MSD ili kupisha uchunguzi kwamba hatua hiyo inastahili pongezi za kipekee.
Pia wameipongeza Serikali kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), kusitisha uzalishaji wa dawa zote katika kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPI hadi uchunguzi unaofanywa kupitia vyombo vya usalama kuhusu uzalishaji wa dawa bandia utakapokamilika kwa hatua zaidi za kisheria.
Kwa mujibu wa kiongozi wa Shidepha mkoani hapa, Korongo alisema mtandao wao huo nao unatoa pongezi za dhati kwa Serikali kwa hatua hizo ilizozichukua kwamba ni dalili na faraja kuwa inawajali.

No comments: