WAFUASI WA UAMSHO WASHAMBULIA MITAANI ZANZIBAR...

Moto ukiwa unawaka katikati ya barabara mbele ya maghorofa ya Michenzani, Zanzibar baada ya wafuasi wa kikundi cha Uamsho kuvamia maduka na kupora mali huku Maskani ya Kisonge ikichomwa moto jana.
Imeripotiwa kwamba fujo kubwa zimeibuka katika Manispaa ya Mji wa Unguja ambazo zinasadikiwa zimefanywa na wafuasi wa Uamsho na kusababisha kuchomwa moto kwa Maskani ya Kisonge pamoja na baa iliyopo eneo la Amani.
Fujo hizo ziliibuka majira ya saa 7 mchana ambapo katika maeneo ya Darajani, watu walivamia maduka na kusababisha uporaji mkubwa huku Maskani ya Kisonge ikichomwa moto.
“Tunasikitika Maskani ya Kisonge imechomwa moto na watu ambao tuna hakika ni wafuasi wa Uamsho ambao kwa muda mrefu lengo lao ni kuhakikisha wanaharibu maskani hii,” alisema mmoja ya wanachama wa maskani hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Ali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Azizi Juma alithibitisha kutokea kwa fujo hizo ambazo zinahusishwa kukamatwa kwa kiongozi wa kikundi cha Uamsho na Mihadhara, Farid Hadi.
“Tunafanya uchunguzi zaidi kujua chanzo cha fujo hizo ingawa mimi sijui kutekwa kwa kiongozi wa kikundi cha Uamsho, Farid Hadi,” alisema kwa ufupi Kamanda Azizi na kuongeza kwamba alikuwa katika mkutano uliowahusisha Makamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi na mikoa ya jirani.
Hadi tunakwenda mitamboni, kikao hicho kilikuwa kinaendelea.
Fujo na vurugu za wafuasi wa Uamsho walivamia baa maarufu iliyopo Amani inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu, Mbawala ambayo ilichomwa moto.
Magari mawili ya Kikosi cha Zimamoto yalifika katika eneo la Amani na kufanya kazi ya kuzima moto huo ambao uliharibu vibaya nyumba hiyo iliyokuwa ikitumika pia kwa kulaza wageni.
Aidha, duka moja la linalouza pombe lililopo eneo la Darajani lilivamiwa na kuvunjwa na watu wasiojulikana ambao wengine walipora pombe na kukimbia.
Katibu wa Jumuiya ya Uamsho, Shekhe Abdalla Said akizungumza na waandishi wa habari alikiri kutoweka kwa Shekhe Farid juzi majira ya saa 3 za usiku na watu wasiojulikana.
“Ni kweli Shekhe Farid ametoweka katika mazingira ya kutatanisha na hadi sasa hajulikani wapi alipo na tayari tumetoa taarifa zetu polisi,” alisema Shekhe Said.
Katibu wa Kamati Maalumu ya CCM Idara ya Itikadi na Uenezi, Ussi Haji Ussi alieleza kusikitishwa na tabia iliyojitokeza ya kushambulia maskani za chama hicho.
Ussi alisema CCM hadi sasa inajiuliza kina nasaba gani na watu wanaofanya fujo ambapo kazi yao kubwa kuzishambulia maskani zao.
“Tunasikitika sana hatujuhi Chama Cha Mapinduzi kwa nini maskani zake zinashambuliwa na wafuasi wa Uamsho. Sijui kimefanya nini kwa kweli?” alihoji Ussi na kuvitaka vyombo vya Dola kufanya kazi ya uchunguzi wa matukio hayo.
Mwezi uliopita, wafuasi wa Uamsho walivamia Maskani ya Kashorora na kuchoma moto na kusababisha hasara kubwa ikiwamo samani za viti na meza.
Mitaa mbalimbali katika mji wa Unguja, imewekwa vizuizi na Jeshi la Polisi kutokana na kuibuka kwa fujo hizo ambapo vijana wamekuwa wakirusha mawe na kuwasha mipira ya gari barabarani.

No comments: