JESHI LA ULINZI LA WANANCHI WA TANZANIA
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
22 Oktoba, 2012
Zipo taarifa ambazo katika wiki hii zimetumwa kwa njia ya simu za mikononi (SMS) zikitahadharisha wananchi wasiokote kitu chochote ambacho wanamashaka nacho, kuwa kuna mabomu yamerushwa toka Malawi. Kwamba mabomu hayo yapo zaidi ya 30 na yenye uzito usiopungua tani 100. Aidha, imeelezwa kwamba taarifa hizi zimetolewa na JWTZ/L S 5 CAMRM.
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania linachukua fursa hii kuwaeleza wananchi wote wa Tanzania kuwa taarifa hizo ni za uzushi na wala hazikutumwa na JWTZ. Uzito wa mabomu ulioelezwa ni mkubwa sana kiasi ambacho ni vigumu kubebwa kwa ndege au kurushwa na mzinga wowote ule. Aidha, zebaki (Mercury) ndio madini nzito kuliko yoyote duniani. Umbo la chupa ya chai ya madini haya hayawezi kufikia hata kilo 15 (lita ya zebaki moja ni sawa na kilo 13.6). Hivyo, hata kama chupa zote 30 zikipimwa hazitazidi kilo 450, hiyo Tani 100 ni kitendawili.
Tunawaomba wananchi wote wazione taarifa hizi kuwa ni za uzushi na wala hazikutolewa na JWTZ. Hatari ya mabomu haiwezi kutolewa na Jeshi kwa njia ya simu, zitatolewa kupitia Vyombo vya Habari vya Radio, Runinga na magazeti. Aidha, Serikali itatoa taarifa hiyo kwa wananchi kwa kutumia mfumo ulio rasmi zaidi na si kupitia SMS za simu za mikononi.
Imetolewa na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga
SLP 9203, Simu: 0764-742161
Email:ulinzimagazine@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment