MWALIMU MKUU KIZIMBANI KWA KUIBA MALIMBIKIZO YA WENZAKE...

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Juhudi, Ilala mkoani Dar es Salaam, Simon Pilla amefikishwa mahakamani akidaiwa kutumia madaraka yake vibaya na kuiba Sh milioni 11.8 za malimbikizo ya walimu wa Manispaa ya Ilala.
Mwalimu Pilla anadaiwa kuiba fedha hizo akishirikiana na mtumishi wa Wizara ya Fedha Kitengo cha Kompyuta, Clara Nyongeja na wafanyakazi wa Manispaa ya Ilala.
Wafanyakazi hao walitajwa jana kuwa ni Kaimu Ofisa Elimu wa Manispaa ya Ilala, Elizabeth Thomas, Joseph Kaika na Mercy Nyalusi ambaye hakufika mahakamani kwa madai kwamba amelazwa hospitalini kwa ugonjwa wa moyo. Nyalusi na Kaika wametajwa kuwa wahasibu wa Manispaa ya Ilala.
Mbele ya Hakimu Agnes Mchome wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Allen Kasamara alidai kuwa washitakiwa bila kukagua, waliingiza maombi ya malimbikizo ya walimu 23 isivyo halali.
Katika mashitaka ya pili hadi ya saba ambayo yanamkabili Mwalimu Pilla peke yake, anadaiwa kuwa katika siku tofauti Machi mwaka juzi akiwa Mwalimu Mkuu Juhudi na Ukonga, alitumia madaraka yake vibaya na kulazimisha walimu wa shule hizo kumpa fedha za malimbikizo ambazo zilikuwa malipo yao halali.
Mwalimu Pilla anadaiwa pia kuwalazimisha walimu Bahati Saidi kutoa Sh milioni 3.8, Esther Mdachi Sh milioni 4.03, Mwaija Chowo Sh milioni 3 na George Masinde Sh milioni 3.9.
Washitakiwa hao ambao wako nje kwa dhamana walikana mashitaka yao na upande wa Mashitaka kuiambia Mahakama kuwa upelelezi umekamilika. Kesi hiyo itatajwa Oktoba 24 mwaka huu.
Walimu nchini wamekuwa wakiilalamikia Serikali kwa madai ya kutowalipa stahili zao yakiwamo malimbikizo yao hata kusababisha migomo ambayo imekuwa ikiratibiwa na kusimamiwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT).
Malimbikizo hayo yamekuwa yakihusisha nyongeza za mishahara, posho za kujikimu za uhamisho na stahili zingine.

No comments: