MIFUPA YA MTU ALIYEKUFA ZAIDI YA MIAKA 15 YAKUTWA KITANDANI...

Mifupa ya mitupu ya binadamu akiwa bado kavalia nguo zake za kulalia kitandani inaaminika imekuwa hapo bila kugundulika kwa zaidi ya miaka 15 kwenye nyumba moja iliyotelekezwa.
Polisi wa Ufaransa wanajaribu kuutambua mwili huo, uliokutwa kaskazini mwa jiji la Lille, ambao unadhaniwa kuwa ni wa mtu mzima aliyekuwa mmiliki wa nyumba hiyo.
Mwanaume huyo alikuwa akiishi mwenyewe na inaonekana hakuwa na ndugu. Mamlaka husika zimekuta lundo la barua ambazo hazijafunguliwa za tangu mwaka 1996 ndani ya nyumba hiyo.
Alikuwa na asili ya Hispania na kwamba alizaliwa mwaka 1921, kwa mujibu wa ripoti za Ufaransa.
"Mazingira ya nyumbani hapo yanaashiria kwamba kilikuwa kifo cha kawaida cha mtu aliyefia kwenye kitanda chake," ofisa wa usalama wa raia Didier Perroudon alisema.
Aliongeza kwamba hakuna ripoti zozote zilizotolewa hapo kabla kuhusu kupotea kwa mtu huyo, na kueleza: "Alikuwa kitandani kwake, akiwa kavalia nguo zake za kulalia."
Didier alisema: "Hakukuwa na chochote, Nyumba ilikuwa imefungwa kwa nje. Hakuna kinachoashiria kitendo chochote cha jinai."
Mwili wa mtu huyo ambaye hakufahamika uliondolewa mahali hapo kwa ajili ya kuufanyia uchunguzi zaidi.
Alikutwa amekufa Ijumaa iliyopita wakati wakaguzi wa afya wanaofanya kazi hiyo kwa niaba ya jiji hilo kutembelea nyumba hiyo.
Didier aliongeza: "Kwa sasa, hatufahamu zaidi.
"Uchunguzi umeanza. Itachukua muda kugundua mahali anakotokea, alikuwa akifanya nini na waliko jamaa zake."

No comments: