MAASKOFU WAISHUKIA SERIKALI KUHUSU VURUGU ZA MBAGALA...

Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia wakiwakamata watuhumiwa wa vurugu zilizosababisha kuharibiwa vibaya mali za makanisa kadhaa katika eneo la Mbagala juzi.
Maaskofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania wameitaka Serikali kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya waumini wa Kiislamu waliofanya fujo kuharibu baadhi ya makanisa likiwamo la Anglikana la Roho Mtakatifu lililoko jijini Dar es Salaam.
Kauli ya maaskofu hao 22 ilitolewa jana jijini Mwanza na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Valentino Mokiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari ambapo walitoa tamko la kulaani vitendo hivyo vilivyofanywa na baadhi ya waumini hao.
“Tunalaani, tumeshtuka kwa vile sio mara ya kwanza kutokea hapa nchini. Katika siku za hivi karibuni, kumetokea matukio kama hayo Zanzibar na Bagamoyo, ambako makanisa yaliharibiwa na kuchomwa moto na baadhi ya waumini wa dini hiyo kwa sababu wanazozijua wao,” alisema.
 Askofu Mokiwa alisema hawajawahi kusikia watu waliohusika na uharibifu wa majengo ya ibada na mali za Kanisa wamechukuliwa hatua stahili na Serikali, ikiwamo kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa Sheria.
“Tunajiuliza kwa nini hilo halikutokea Zanzibar wala Bagamoyo, tunaanza kufikiri kuwa huenda Serikali inawaogopa au kuwalinda waumini hao wanaoutumia mwavuli wa dini yao kuharibu majengo ya makanisa na mali zilizoko kwenye makanisa hayo.   
Alimshukuru Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum kwa jinsi alivyoelewa mgogoro huo na kuuelezea kupitia vyombo vya habari juu ya chanzo  kuwa ni ubishi, ushindani wa barabarani wa watoto wawili wa shule.
Pia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimelaani vurugu, udhalilishwaji wa dini na uharibifu wa nyumba za ibada vilivyofanyika Mbagala na kuvitaka vyombo vya Dola viwachukulie hatua za kisheria wahusika.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Uenezi na Itikadi wa chama hicho, Nape Nnauye, alisema vurugu zilizotokea kuhusisha dini ni kinyume na mila na desturi za Watanzania.
“Kitendo cha kukojolea kitabu kitakatifu cha Waislamu hakikubaliki lakini pia kitendo cha kuvamia na kuchoma moto nyumba za ibada za Wakristo na vurugu pia hakikubaliki,” alisema Nape.
Katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) lililochomwa, jana waumini wake walitakiwa kutolipiza kisasi kwa mtu yeyote, wala kumchukia kwa kuchoma moto na kuharibu Kanisa na kuwataka kuombea amani ya nchi.
Akihubiri katika Ibada KKKT Usharika wa Mbagala, Kaimu Katibu Mkuu, Theolojia, Misioni na Uinjilisiti Mchungaji Boniface Kombo alisema pamoja na huzuni waliyoipata kutokana na uharibifu huo, ni vema kuwaombea rehema wahusika na si kuomba laana maana maandiko hayaruhusu kufanya hivyo.
“Kuna watu wanasema upole wenu (Wakristo) ndio unaowagharimu, lakini sisi tunasema upole wetu una faida kwa Mungu, hata mjinga akinyamaza anaonekana ana hekima. Hii si vita yetu ni ya Mungu, Mungu, anajua kushughulika nao,” alisema Mchungaji Kombo.
Kutokana na uharibifu uliofanyika juzi, mamia ya waumini wa kanisa hilo walilazimika kufanya ibada nje ya kanisa hilo.
Awali, akitoa salaam za Jimbo Kuu la Kusini Diyosisi ya Mashariki na Pwani, Mkuu wa jimbo hilo, Amani Lymo alisema Kanisa lina imani na uongozi wa Rais Jakaya Kikwete kuwa atalishughulikia suala hili kwa umakini.
Mchungaji Lymo aliwakumbusha waumini kuwa wao si watu wa kulipiza kisasi wala kumpigania Mungu, kwani Mungu wanayemuamini anajitetea mwenyewe na hata kisasi ni juu yake.
Alisema hakuna dini yoyote inayoruhusu kufanya uovu dhidi ya mwingine na kuwa kulipiza kisasi kutazidisha chuki za dini na kuondoa amani kama hali ilivyo katika nchi za Nigeria na Ghana.
Kwa upande wake, Rais Jakaya Kikwete amewataka viongozi wa dini nchini kutochukua uamuzi wakiwa na hasira kutokana na tukio la vurugu na uharibifu wa nyumba za ibada lililotokea Mbagala jijini Dar es Salaam kwa kuwa kuna hatari ya kufanya makosa.
Aliyasema hayo wakati akihutubia Taifa kwenye sherehe za kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru na miaka 13 ya Kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere zilizofanyika mkoani Shinyanga.
Alisema kilichotokea Mbagala kuanzia kijana kuharibiwa Kitabu Kitakatifu cha Waislamu na hatua za wanaharakati wa Kiislamu kuanzisha vurugu na kuharibu mali za makanisa, hakikubaliki na lazima wahusika wachukuliwe hatua.
“Yule kijana hakutumwa na Kanisa wala mtu yeyote kilichotokea ni matokeo ya ubishi wa watoto na tayari alikuwa yupo Polisi sasa kitendo cha wanahakati wa Kiislamu kwenda Polisi na kutaka wakabidhiwe mtoto huyo wamuadhibu hakikuwa sahihi,” alisema Kikwete.
Alisema vurugu na uvunjaji wa vifaa vya makanisa ni vitendo ambavyo havina maelezo ya kujitosheleza kwa kuwa ni makosa. “Ndio maana nawaomba tujiepusha na matendo kama haya ya kuchukua hatua mikononi, tuachie vyombo vya Dola vifanye kazi yake,” alisisitiza.
Alisema kutokana na matukio yale jamii nzima ilipata wasiwasi na wengi walidhani kungetokea vita ya Waislamu na Wakristo nchini jambo ambalo lilizua wasiwasi usiostahili katika jamii.
“Narudia kusema, jana (juzi) katika ziara yangu niliwasihi viongozi wa dini na wananchi wajiepusha na jazba na kulipiza kisasi, niliwashauri wasifanye uamuzi wakiwa na hasira kwani wanaweza kutoa maamuzi yenye makosa,” alisema Rais Kikwete.

No comments: