KAMATI YA KUCHUNGUZA MAUAJI YA MWANDISHI YAKIRI POLISI KUTUMIA NGUVU KUBWA...

Siku polisi walipotumia nguvu kubwa kumdhibiti mwandishi Daudi Mwangosi na hatimaye kusababisha kifo chake.
Kamati iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza kifo cha aliyekuwa mwakilishi wa kituo cha Televisheni cha Channel Ten, mkoani Iringa Daudi Mwangosi imekabidhi ripoti yake na kukiri kuwepo kwa nguvu kubwa ya Jeshi la Polisi lakini haikutumika moja kwa moja katika mauaji hayo.
Aidha imebaini kutokuwepo kwa uhalali wa mkutano katika eneo hilo na kuwepo kwa agizo la kusitisha kutokana na kuendelea kwa shughuli za sensa.
Kadhalika kubaini kutokuwepo kwa mahusiano mazuri baina ya baadhi ya vyama vya siasa na jeshi la Polisi nchini na hivyo kupendekeza kuundwa kwa jukwaa la mawasiliano ili kuepuka misuguano isiyo ya lazima.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jaji mstaafu, Steven Ihema alisoma ripoti hiyo jana Dar es Salaam, mbele ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchini na kuongeza kuwa madai ya kuwepo kwa waandishi wa habari watatu wanaokusudiwa kushughulikiwa na Jeshi la Polisi hayakupata ushahidi.
Akizungumza, Jaji Ihema alisema baada ya kuteuliwa Septemba 6,2012 kufanya kazi hiyo, walipewa hadidu sita za rejea ikiwa ni pamoja na kuangalia kama kuna nguvu zilizotumika na jeshi la polisi hadi kusababisha kifo cha Mwangosi.
"Nguvu iliyotumika ilionekana ni kubwa kwa upande wa ngazi ya viongozi wa vijiji, pia viongozi wa dini waliona hivyo,kwani waliona harakati zilizokuwa zikiendelea pale...nguvu ni kubwa, askari walivalia mavazi yaliyoashiria kungekuwa na vurugu, ingawaje katika Kamati za ulinzi za wilaya na mkoa ziliona nguvu hiyo ni sahihi," alisema Jaji Ihema.
Hata hivyo alisema Kamati ilijidhirisha kuwa nguvu hiyo haikutumika moja kwa moja na mauaji ya Mwangosi kwani opereshemi ilimalizika baada ya wafuasi kutawanyika kutokana na mabomu yaliyolipuliwa ambayo hayakuwa na madhara.
"Kwa maana hiyo tukio la kuuawa kwa Mwangosi halikutokana na nguvu hiyo ya Polisi.. uchunguzi ulibaini kuwa operesheni ilifanyika na baada ya amri ya kuondoka eneo hilo kutolewa, wafuasi walitii na wakati askari wakiondoa eneo hilo ndio purukushani ya polisi na na Mwangosi ikaanza," alisema Jaji Ihema na kuongeza kuwa ushahidi zaidi katika hilo waliupata kutoka kwa mmoja wa waandishi wa habari.
Kuhusu uhalali wa mkutano huo ambao uliitishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alisema hapakuwepo kwa uhalali wa mkutano siku hiyo ambapo vilevile kulikuwepo kwa agizo la kusitisha mikutano wakati wa sensa baada ya muda kuongezwa.
"Kilichobainika ni kuwa taarifa ya kuongezwa kwa muda iliwafikiwa walengwa ikiwa imechelewa ambapo wakati tukizunguma na Katibu wa Chadema mkoa wa Iringa alisema, OCD wa Mafinga alitoa kibali lakini baadae amri ilitoka kwamba kwa vile sensa inaendelea mkutano usingekuwepo ambapo baada ya kupewa taarifa hiyo, jibu alilolitoa ni hapana," alisema Jaji Ihema.
Kuhusu mahusiano ya madai ya kuwepo kwa uhasama wa Jeshi la Polisi mkoani Iringa na kwamba waandishi watatu wamepangwa kushughulikiwa na polisi na chanzo chake alisema hilo halikupatiwa ushahidi na kwamba hata walipozungumza na waandishi wenyewe hakuna aliyejitokeza kuthibitisha.
Alisema hata suala la kutokuwepo kwa mahuasiano mazuri baina ya jeshi la Polisi na waandishi wa habari sio mazuri kwani polisi wenyewe wanasema wako vizuri huku wandishi wenyewe wakisema wananyanyaswa hivyo kupendekeza pande hizo ziunganzishwe ili zifanye kazi pamoja.
Kadhalika alisema Kamati imebaini kuwepo kwa mahusiano yasiyoidhisha kati ya Polisi na baadhi ya vyama vya siasa na kupendekeza kuundwa kwa jukwaa la mawasilaino litakalosaidia kuondoa msuguano baiana ya pande hizo.
Akitoa mapendekezo Jaji Ihema alisema Jeshi la Polisi litaendelea kuwa nguzo ya kusimamia ulinzi na usalama na kwamba siasa za ubabe zifutwe kwani zinaleta msuguano.
Kwa upande wake, Dk. Nchimbi alisema kamati imefanya kazi kubwa na kwamba atakutana na wadau mbalimbali kwa ajili ya kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na kamati hiyo.
Alisema kuhusu taarifa za nani alihusika na mauaji hayo taarifa hiyi ipo lakini haiwezi kutolewa kwa umma kwa sasa kwa sababu kuna kesi inayoendelea Mahakamani.
Vurugu zilizosababisha kuuawa kwa Mwangosi zilitokea Septemba 2, mwaka huu katika Kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi wakati Polisi walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakifungua tawi la chama hicho katika kijiji hicho.
Wajumbe wa Kamati hiyo Jaji Mstaafu, Steven Ihema ambaye alikuwa Mwenyekiti na Mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga, Mwakilishi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili Mtambalike, Mtaalamu wa milipuko kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Wema Wapo na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Isaya Mngulu ambapo walifanya kazi kwa siku 19.

No comments: