WANANDOA WALIOIZUNGUKA DUNIA WAFA KWA KUGONGWA NA TRENI...

Wanandoa wawili ambao walitumia miaka mitano kusafiri pamoja duniani wamefariki ikiwa ni siku mbili tu baada ya kurejea nyumbani kwa kugongwa na treni mita chache kutoka yalipo makazi yao.
Daniela Weiss an mpenzi wake, Daniel Oelter, wote wanye miaka 38, walisafiri kuzunguka sehemu za hatari zaidi katika mabara kadhaa kwenye ziara ya marathoni iliyowapeleka hadi Asia, Mashariki ya Kati na Amerika ya Kusini.
Lakini waliuawa pale walipogongwa na treni wakati wakivuka reli karibu na nyumbani kwao huko Granichen, Uswisi, majira ya Saa 3:20 usiku wa Jumatano.
Wanandoa hao walionekana wakiwa wamekumbatiana muda mfupi kabla hawajagongwa na treni lililokuwa likisafiri kwa mwendokasi wa kilomita 70 kwa saa.
Daniel alikufa palepale, wakati Daniela alikimbizwa hospitali mjini Aarau lakini alifariki asubuhi ya siku inayofuata.
Mama wa Daniela, Margit Weiss mwenye miaka 70 alisema: "Nilijua walikuwa safarini sehemu mbalimbali zenye hatari. Mara zote nilijua kuna kitu fulani kinaweza kutokea. Nilihofu kila siku. Ilikuwa pale waliporejea ndipo nikaacha kuhofu, sikuwaza kitu hiki kingeweza kutokea mbele ya mlango wangu.
"Majira ya Saa 7:30 alfajiri nilisikia mlango ukigongwa. Nilidhani Daniela kasahau funguo zake. Lakini nilipofungua walikuwa polisi.
"Pale polisi waliponieleza kilichotokea koo langu lilikauka mate. Nilihisi siwezi kupumua. Daniela ni mtoto wetu mkubwa.
"Daniela alikuwa binti bora ambaye kila mtu angependa kumpata na Daniel alikuwa mpenzi wa kipekee kwake. Wote walikuwa wa kipekee.
"Ilikuwa jambo la kufurahisha mno kumwona tena binti yangu akirejea nyumbani lakini amekufa katika sehemu ambayo ni ya salama zaidi duniani," aliongeza.
Daniela aliamua kurejea nyumbani Uswisi kutokana na matatizo yake ya meno na alitakiwa kupatiwa matibabu.
Wanandoa hao wazunguka dunia walikutana na kuzama kwenye mapenzi mwaka 2005. Walikuwa wakifanya kazi Uswisi na kushiriki tabia ya kupenda kusafiri, na hatimaye wakaamua kuacha kazi, wakauza kila walichonacho na kuandaa safari zao.
Margit alisema: "Alikuwa mtu mzuri. Wote wawili walikuwa watu wazuri mno kwa pamoja. Daniela alikuwa anajali sana. Mara zote alikuwa akipiga simu nyumbani na kutusimulia maajabu aliyojifunza. Walinifanya niwe na furaha sana.
"Machi, mwaka huu Daniela alianza kuwa na matatizo ya meno. Yalizidi kiasi cha kuanza kushindwa kula. Alisubiri kwa kitambo, lakini hakupata nafuu. Hivyo wote wakakubaliana kurejea Uswisi kwa ajili ya matibabu.
"Nilijihisi vizuri kumwona tena binti yangu. Hatimaye binti yangu akarejea. Na yeye alikuwa na furaha pia, furaha ya kuweza kuwa kwenye mikono salama, kuweza kula na kulala na kupata matibabu yake.
"Katika siku yake ya mwisho alitoka kwa matembezi na Daniel na kurejea kama baada ya masaa mawili. Alipenda sana kuzurura mitaani. Kisha nikaenda na binti yangu kununua TV na kisha tukatoka tena kwa matembezi tena.
"Wakati tukiwa njiani mchumba wake akampigia simu na kumweleza amemtafutia kazi. Tulikula chakula cha jioni pamoja. Kisha nikaenda kulala. Daniela alinitakia usiku mwema na nikamuaga kabla ya kutoka na Daniel kwa matembezi ya kupunga upepo."
Lakini sikuweza tena kuwaona wanandoa hao.
Shuhuda aliyeona ajali hiyo alidai wawili hao walikuwa wakijadili kitu muda mfupi kabla ya vifo vyao na kwamba walionekana wakikumbatiana kando ya reli.
Mama wa Daniela Margit alisema: "Hawakusimama kando ya reli kwa makusudi. Walikuwa wakitafakari maisha yao ya baadaye Uswisi.
"Wawili hao wanawezekana kabisa kuwa walikuwa wakijadili kazi mpya ya Daniela.
Kwa Margit pia maisha yake yamekomea kwenye magurudumu ya treni.
Aliongeza: "Kupoteza mwanao ni kitu kibaya mno kuweza kutokea kwa yeyote yule. Huwezi kupata mfano kitakapokupata, pale tulipofikiri tumepata kumwona tena mwanetu na pale tulipofikiri pia tumepata mtoto wa kiume, tumewapoteza wote moja kwa moja."

No comments: