WANAFUNZI 10 WA KIDATO CHA NNE WASIMAMISHWA...


Bodi ya Sekondari ya Mafulala mjini hapa, imesimamisha masomo wanafunzi 10 wa kidato cha nne kwa utovu wa nidhamu, huku wakiruhusiwa kufanya mitihani kwa masharti, ikiwa ni pamoja na kulindwa  na wazazi wao kipindi chote cha mitihani.
Kila mwanafunzi kwa masharti hayo, atalazimika kufanya mtihani akiwa na mzazi au mlezi eneo la shule katika kipindi chote cha mitihani hiyo inayotarajiwa kuanza Oktoba 8, vinginevyo hataruhusiwa kufanya mitihani.
Hayo yalithibitishwa jana na Mkuu wa Shule hiyo, Robert Mwaihojo na kuongeza kwamba waliosimamishwa ni pamoja na viranja wakuu wawili.  
Akifafanua, alisema masharti ya kulindwa na wazazi katika kipindi chote cha mitihani yanatokana na hofu ya wanafunzi hao kufanya fujo.
Alisema  wazazi waliitwa  shuleni na kupewa  masharti  hayo kimaandishi na kimsingi  waliyakubali na kumthibitishia Ofisa Mtendaji wa Kata ya Izia.
Kwa mujibu  wa Mkuu  wa Shule  wanafunzi  hao  walisimamishwa Septemba 17  kwa  tuhuma za kuchochea  wenzao  kufanya  fujo.
Mkuu  wa Shule aliyezungumza juzi, alidai  kuwa hakuwa tayari kutoa maelezo zaidi akisema yeye si msemaji wa  shule  na kumwomba mwandishi awasiliane na Ofisa Elimu Sekondari wa Manispaa  ya Sumbawanga.
Lakini baadhi ya wanafunzi  shuleni  hapo walidai kuwa mvutano ulianza mapema mwezi huu baada ya uongozi  wa  shule kufuta sherehe  za  mahafali ya  kidato  cha  nne  ukihofia fujo, ikidaiwa kuwa baadhi yao ni walevi wa pombe na bangi.
Baadhi ya wanafunzi  waliosimamishwa  masomo, walikiri kusimamishwa masomo, lakini wakahofia kuwa huenda wasifanye mitihani wakiamini itakuwa vigumu kwa wazazi kushinda shuleni katika kipindi chote cha mitihani.
“Mimi nimekata tamaa, kwanza tumeshaathirika kisaikolojia, isitoshe wazazi wangu  wote ni  watumishi  hawatapata  nafasi hiyo  ya kunisubiri kutwa nzima kwa  wiki  nzima  wakati  wa mitihani. Adhabu  hii ni kali na imelenga kutukomoa tu,“ alisema mmoja wao huku akilengwa machozi.
Alitumia fursa hiyo kufichua kuwa, si wote walioshiriki, bali mmoja wao ambaye pia ni kiongozi kuwa  ndiye aliandika barua ya uchochezi  peke  yake  bila kuwashirikisha. Alikiri ni kweli kiongozi huyo ni mlevi.
Kwa mujibu wa ratiba  ya mitihani, wanafunzi  wa masomo ya Sanaa  watafanya  mitihani  kwa siku tano  huku  wa masomo ya Sayansi  wakifanya kwa siku nane.
Hata hivyo, jitihada za  kumpata  Ofisa Elimu (Sekondari) wa  Manispaa ya Sumbawanga, Gwakisa  Lusanjo ziligonga  mwamba  kwani  simu  yake ya mkononi  ilikuwa ikiitwa bila kupokewa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda  alidai kutotaarifiwa tukio  hilo,  lakini  kama Ofisa Elimu atahitaji ulinzi  shuleni  hapo  kwa siku  hizo, watakuwa tayari kufanya hivyo.
“Hawajatuarifu, labda  wanadhani  wanaweza kulikabili  wao  wenyewe,  unajua  huwa hatuingilii   masuala ambayo wahusika wanadhani wanaweza kuyamudu wenyewe,  kazi  yetu  ndiyo  hiyo  ya   kulinda mali  na  maisha ya watu, hivyo kama Ofisa Elimu atatuhitaji basi tuko tayari wakati  wowote  kutoa ulinzi  shuleni  hapo,” alisema Kamanda.

No comments: