PINDA AWATIMUA WAKURUGENZI SITA...

Waziri Mkuu Mizengo Pinda (pichani) amewavua madaraka Wakurugenzi sita wa Halmashauri nchini, kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo udhaifu katika kutekeleza majukumu yao.
Uamuzi huo ulitangazwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia aliyeonya kuwa, Waziri Mkuu hatasita kuendelea kuwachukulia hatua watumishi watakaoshindwa kuwajibika.
Ghasia aliwataja waliovuliwa madaraka na Waziri Mkuu kuwa ni pamoja na Mpangalukela Tatala (Geita) na Theonest Nyamhanga (Kishapu), ambao sababu za kuvuliwa kwao madaraka zimetajwa kuwa ni kushindwa kusimamia rasilimali watu na fedha.
Aidha, Eden Munisi (Morogoro) ameondolewa kutokana na kuisababishia halmashauri yake kupata hati chafu, kushindwa kusimamia rasilimali watu na uzembe.
Wengine, Mhando Senyangwa (Kyela) ana kesi mahakamani wakati Nicholaus Kileka wa Ngorongoro alikuwa na kesi iliyoendeshwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), wakati mmoja, Willy Njau wa Mwanga, ameomba kuachwa katika nafasi yake kutokana na sababu za kiafya.
"Michakato ya kinidhamu inaendelea na baadhi yao tayari wana kesi mahakamani na wengine tumeshawafikisha Takukuru, na kwa sasa Tamisemi tumejipanga vizuri, tutawachukulia hatua za kinidhamu watumishi wote ambao hawawajibiki ipasavyo," alisema Ghasia.
Wakati hao wakivuliwa madaraka, Serikali imetangaza majina ya Wakurugenzi wapya 14 na Halmashauri zao katika mabano kuwa ni Naomi Nko (Magu), Mohammed Maje (Namtumbo), Abdallah Mfaume (Kyela), Adam Mgoyi (Mbarali), Estomih Chang’a (Mpanda), Leti Shuma (Mwanga), Fulgency Mponji (Moshi) na Robert Nehata (Tunduru).
Wengine ni Isabela O. Chilumba (Kahama), Isabela D. Chilumba (Ulanga), Fikiri Malembeka (Sengerema), Nassib Mbaga (Biharamulo), Jovin Jungu (Chamwino). Saba wameteuliwa kukaimu, nao ni Abdallah Kidwanka (Geita), Rutius Bilakwata (Kishapu), Twalib Mbasha (Monduli), Henry Rugayu (Urambo), Iddi Nganya (Makete), Paul Malala (Njombe) na Felix Mabula (Hanang).
Aidha, Serikali imewahamisha Wakurugenzi 27 kutoka vituo vyao vya kazi. Waliohamishwa na majina ya sehemu wanazotoka zikiwa kwenye mabano ni Bibie Mnyamagola, Kongwa (Kilindi), Daudi Mayeji, Kilindi (Chamwino), Protace Magayane, Nkasi (Igunga), Saada Mwaruka, Mkuranga (Nkasi), Sipora Liana, Tabora (Mkuranga), Hadija Makuwani, Tabora (Tabora Manispaa), Doroth Anatoli, Kasulu (Tabora), Kelvin Makonda, Lindi (Kasulu).
Wengine ni Pudenciana Kisaka, Iringa (Ulanga), Tina Sekambo, Makambako (Iringa), Beatrice Dominic, Masasi (Bukoba), Gladyness Ndyamvuye, Bukoba (Masasi), Nathan Mshana, Ngorongoro (Musoma), Cornel Ngudungi, Ngara (Magu) na Mohammed Mkupete, Mtwara (Njombe).
Pia wamo Koroine Ole Kuney, Misungwi (Ngorongoro), Ephraim Ole Nguyaine, Rorya (Tunduru), Goody Pamba, Igunga (Hanang), Fidelis Lumato, Ludewa (Tarime), Athuman O, Tarime (Kongwa) na Ahmad Sawa, Musoma (Lindi).
Wakurugenzi wanaohamishwa kwenda kwenye halmashauri mpya ni Magreth Nakainga, Geita (Mtwara), Eliza Bwana, Bariadi (Kahama), Zuberi Mbyana, Ilemela (Biharamulo), Mohammed Nanyanje, Masasi (Sumbawanga), Erica Musika, Kahama (Sengerema) na Imelda Ishuza, Busokelo (Makete).

No comments: