BEI YA PETROLI YAPANDA TENA KWA ASILIMIA 15...


Bei ya mafuta ya petroli imepanda kuanzia kwa Sh 291 kwa lita sawa na asilimia 14.50 ya ongezeko huku dizeli ikiongezeka kwa Sh 199 kwa lita, sawa na asilimia 10.26 ya ongezeko.  
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza ongezeko hilo la bei ambapo bei ya Mafuta ya Taa pia imepanda kwa Sh 67 kwa lita, sawa na asilimia 3.47 yan ongezeko la bei.
Kutokana na ongezeko hilo, bei ya kikomo ya Petroli jijini Dar es Salaam, itakuwa Sh 2,300, Dizeli Sh 2,142 na mafuta ya taa Sh 1,993.
Bei ya juu kabisa ya nishati hiyo itakuwa katika Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma ambapo Petroli itauzwa kwa Sh 2,543, Dizeli Sh 2,385 na Mafuta ya Taa, Sh 2,236.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko. Ewura itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta,” ilieleza taarifa ya Ewura.  
Ewura pia ilizitaka kampuni za mafuta kuwa huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziwe chini ya bei kikomo.
Sababu ya kupanda kwa bei hiyo kwa mujibu wa Ewura, ni kupanda kwa gharama halisi za uagizaji wa mafuta kutoka kwenye soko la dunia.


No comments: