WALIOGOMEA SENSA SASA KUKIONA CHAMOTO...

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki (pichani) amesema wanaogomea Sensa ya Watu na Makazi, watatambulika kwa namba za nyumba zao na baada ya siku saba baada ya sensa, watachukuliwa hatua za kisheria kwa kutenda kosa la jinai.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Sadiki alisema wapo baadhi ya watu mitaani wamegoma kuhesabiwa na kufafanua kuwa watatambuliwa kwa nyumba zao kwa kushirikiana na viongozi wa mitaa wanaofuatana na makarani wa sensa.
"Makarani wetu wana ramani zinazowaonesha nyumba wanazotakiwa kuhesabu zikiwa na namba, pia wanafuatana na viongozi wa mitaa, hawa ndio watatusaidia kutambua waliogoma kuhesabiwa ili tuwachukulie hatua," alisisitiza.
Alisema kwa sasa hawatawachukulia hatua waliovunja sheria, kwa kuwa wanaweza kudai kuwa bado watu wanaendelea kuhesabiwa, lakini wataanza kuwachukulia hatua baada ya siku za sensa kumalizika.
Akielezea hali ya sensa ilivyo, Sadiki alisema baadhi ya matukio yaliyojitokeza ni pamoja na watu wanane kushikiliwa kwa kushawishi mgomo wa sensa, ikiwa ni pamoja na kutuma ujumbe mfupi wa maneno kwa simu.
Alisema kati yao, yumo aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) akafukuzwa, aliyekamatwa Mbagala, Yusuph Ernest ambaye na wenzake watatu wanaendelea kushikiliwa na Polisi kwa mahojiano.
Alisema wengine waliogoma kuhesabiwa walikutwa Magomeni Kagera, wakihamasisha watu kugoma, lakini baadaye walidhibitiwa na kuacha uhamasishaji.
Aliwataka watu kutoa ushirikiano kwa kuwaripoti wanaokataa kuhesabiwa au kukwamisha sensa, ili sheria ichukue mkondo wake.
Mkoani Kigoma, kulikuwa na changamoto kadhaa baada ya baadhi ya waumini wa dini ya kiislamu kukimbilia misikitini ili wasifikiwe na makarani.
Mkuu wa Wilaya Kigoma, Ramadhani Maneno alisema jana kuwa katika pitapita yao kufanya tathmini, walikutana na changamoto hiyo na wameanza kuifanyia kazi.

Alitaja maeneo waliyogundua tatizo hilo ni Mwandiga na Katonga, ambapo licha ya kutaka kuzungumza na viongozi wao, alikosa ushirikiano.
Kutokana na ukaidi huo, Maneno alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama inatarajia kujadili kuhusu hatua za kuchukua.
Mkuu wa Wilaya alisema katika baadhi ya misikiti, waumini walijichimbia huko wakifanya ibada na kulala ili kuhakikisha makarani hao hawawafikii.
Mbali na hao waliolala msikitini, Maneno alisema katika kijiji cha Bubango kata ya Bitale wilayani Kigoma, familia 40 kati ya 64 za eneo hilo zilikataa kuhesabiwa.

Alisema makarani walipokwenda kwenye familia hizo, wenyeji walieleza kuwa wakuu wa kaya hawapo na hawajui kutoa maelezo ya chochote hadi viongozi hao wa kaya wawepo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa Kigoma, Fraiser Kashai alisema watu 11 walitiwa mbaroni katika maeneo kadhaa ya mkoa huo wakihusishwa na kuchochea wananchi kususia sensa akiwamo Mwenyekiti wa Kitongoji wilayani Kibondo.
Kamanda Kashai alitaja watu hao kuwa ni Juma Hussein, Shuri Hamad, Hadija Siajari na Yapemacho Hussein ambao walikamatwa Mwandiga.

Wengine ni Nkatula Issa, mkazi wa Uvinza ambaye alikamatwa akisambaza vipeperushi vya kuhamasisha watu kususia sensa.
Pia Mussa Sadick, Japhari Abdallah, Husein Hassan na Halfani Rashidi ambao walilala msikitini na kuhamasisha watu kukataa kuhesabiwa.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Kalunde B, Kibondo ambaye alikataa kutoa msaada kwa makarani na kuhamasisha jamii kutoshiriki sensa, alikamatwa pamoja na Idrisa Ibrahimu ambaye ni mvuvi wa Katonga aliyekuwa akichochea watu kugomea sensa.

No comments: