ALIYEKUWA MKUU WA WILAYA YA MBARALI AFARIKI DUNIA...

Hawa Ngulume
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Hawa Ngulume amefariki dunia jana asubuhi katika hospitali ya Jeshi ya Lugalo kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya mapafu kwa muda mrefu.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, alithibitisha kutokea kwa msiba huo ambapo alifafanua kuwa msiba uko nyumbani kwa marehemu Goba jijini Dar es Salaam.
"Ni kweli tumepokea kwa masikitiko taarifa ya msiba wa mheshimiwa Ngulume ila bado hatujajua sababu ya kifo hicho tunasubiri taarifa ya madaktari wa Lugalo ambako alilazwa kwa muda wa wiki nzima," alisema Rugimbana.
Hata hivyo kwa mujibu wa Msemaji wa familia hiyo, Alhaji Mwenza, alisema Ngulume alifariki jana majira ya saa 4.25 asubuhi ambako alikuwa akitibiwa ugonjwa wa saratani ya mapafu.
Alisema kwa mujibu wa taarifa za awali alizokuwa nazo marehemu ilikuwa azikwe leo saa saba mara baada ya sala ya Ijumaa nyumbani kwake Goba, lakini baadaye ratiba ilibadilika na leo anatarajiwa kusafirishwa kijijini kwao Kintiko mkoani Singida.
"Kwa mujibu wa watoto wake, kesho (leo) atasafirishwa kupelekwa Singida katika tarafa ya Kintiko ambako anatarajiwa kuzikwa keshokutwa (kesho) kama mambo yote yataenda sawa," alisema Mwenza.
Ngulume wakati wa uhai wake aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo ukuu wa wilaya katika wilaya za Kinondoni, Bagamoyo na Mbarali ambako ndiko alikostaafu wadhifa huo.
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Ngulume.
Rais Kikwete alisema jana kuwa marehemu Ngulume, enzi za uhai wake, alikuwa kiongozi shupavu aliyesimamia uamuzi wake katika majukumu muhimu ya kitaifa kwa lengo la kuletea wananchi maendeleo sehemu zote alizotumikia.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana ilisema alipopewa wadhifa wa Mkuu wa Wilaya za Singida Mjini mkoani Singida, Kinondoni, Dar es Salaam na mara ya mwisho katika wilaya ya Mbarali, Mbeya.
"Nilimfahamu marehemu, enzi za uhai wake, akiwa kiongozi mwanamke shupavu aliyesimamia kikamilifu uamuzi wake na hivyo kuthibitisha ukweli, kwamba wanawake wakipewa fursa wanaweza," alisema Rais Kikwete.
"Kutokana na msiba huo mkubwa, natuma salamu za rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kwa familia ya marehemu, Hawa Ngulume kwa kuondokewa na mhimili muhimu na kiongozi wa familia.
"Natambua machungu mliyonayo hivi sasa kwa kumpoteza mama wa familia, lakini nawahakikishieni kuwa niko pamoja nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa," aliongeza Rais Kikwete katika salamu zake.
Rais aliwataka wanafamilia wawe na moyo wa uvumilivu na ujasiri wakati huu wanapoomboleza msiba wa mpendwa wao kwani yote ni mapenzi yake Mola. Alisema anamwomba Mwenyezi Mungu, aipokee na kuilaza mahali pema peponi roho ya marehemu.
Marehemu ameacha watoto wawili pamoja na wajukuu watano.

No comments: