TUME YA KATIBA YAONGEZA MUDA...

Tume ya Mabadiliko ya Katiba imelazimika kuongeza muda wa kupokea maoni ya wananchi katika baadhi ya mikutano ya kukusanya maoni na wakati mwingine kuongeza idadi ya mikutano ili kutoa fursa zaidi kwa wananchi kutoa maoni yao.
Katibu wa Tume hiyo, Assaa Rashid alisema hayo jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kufafanua malalamiko yaliyoelekezwa kwa Tume hiyo ikiwamo madai kuwa imeweka ukomo wa idadi ya wananchi wanaotoa maoni katika mikutano yake inayoendelea katika mikoa minane nchini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ilidaiwa na baadhi ya wananchi walionukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari kuwa Tume hiyo imekuwa ikitoa nafasi 10 tu kwa wananchi wanaopaswa kuuliza maswali yasiyozidi kumi katika mkutano mmoja.
Mbali na madai hayo, mengine ni kuachwa kwa baadhi ya kata katika baadhi ya wilaya ikiwamo ya Biharamulo mkoani Kagera yenye kata 15, ambapo kata sita tu ndizo zilizofikiwa.
Katika ufafanuzi wake, Assaa alisema Tume ingependa kupata maoni ya kila mwananchi na hivyo haiwezi kuweka ukomo kwa wananchi kutoa maoni katika mikutano inayoiitisha.
"Katika baadhi ya wilaya, kama Kusini Unguja na Bahi mkoani Dodoma, Tume imelazimika kuongeza muda wa kupokea maoni ya wananchi na wakati mwingine kuongeza idadi ya mikutano hadi kufikia mitatu badala ya miwili kwa siku. Hatua hizi zinalenga kutoa fursa zaidi kwa wananchi kutoa maoni yao," alisema Assaa.
Kuhusu baadhi ya kata kuachwa, Assaa alisema Tume haikupanga ratiba ya mikutano ya kukusanya maoni kwa kuzingatia kata, bali imepangwa kwa kuzingatia eneo linaloweza kujumuisha wananchi kutoka zaidi ya kata moja.
Akitolea mfano huo wa Wilaya ya Biharamulo, Assaa alisema Tume ilipanga na imefanya mikutano sita kuanzia Julai 2, mwaka huu hadi Julai 4, na wananchi 267 walitoa maoni yao kwa mdomo na wananchi wengine 265 walitoa maoni yao kwa maandishi.
Katika wilaya hiyo, Assaa alisema vituo ambavyo mikutano hiyo ilifanyika ni Kelenge, Movata, Nyamigogo, Runazi, Nyakanazi na Biharamulo Mjini.
Hata hivyo, Assaa alisema ingawa Tume ingependa kumfikia kila mmoja mahali alipo, jambo hilo halitawezekana kutokana na jiografia ya nchi na muda ambao Tume imepewa.
Aliwasihi wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi katika maeneo ambayo Tume itafanya mikutano kama ratiba iliyotolewa inavyoelekeza na kutoa maoni yao kwa uhuru na uwazi.

No comments: