MTOTO AVUNA PAUNI 120,000 KWA WIKI, MAMA AISHI KIFUKARA KWA PAUNI 6...

Analipwa Pauni za Uingereza 120,000 kwa wiki, hupendelea kunywa shampeni moja kwa moja kwenye chupa na mara moja hutoa mamia ya pauni kwenye sahani ya sadaka kanisani.
Lakini ukarimu wa Mario Balotelli hauonekani kufika hadi kwa mama yake, ambaye anafanya kibarua cha mfagizi wa ofisi umbali wa maili kadhaa tu kutoka jumba la kifahari la mwanae lenye thamani ya Pauni za Uingereza milioni 3.
Wakati mwanasoka huyo wa Manchester City aking'ara mitaani na gari lake la kifahari aina ya Bentley Continental GT lenye thamani ya Pauni 120,000, Rose Barwuah anahangaika na usafiri wa basi la jumuiya Namba 11.
Mara tano kwa wiki, anapanda basi kwenda kazini kama mfagizi wa ofisi kwenye kampuni ya kukodisha magari iliyoko eneo la Cheadle, jirani na Manchester, akijipatia ujira wa karibu Pauni 6.08 kwa saa.
Mahali anapoishi ni makazi ya nyumba za halmashauri mjini Wythenshawe, eneo linalotumika kutengeneza filamu ya Shameless, kipindi cha vichekesho kinachorushwa na televisheni ya Channel 4.
Mama huyo mwenye miaka 46 alimkabidhi Balotelli kuasiliwa na familia nyingine akiwa na miaka miwili, na yeye na mumewe walikuwa wakiishi katika umaskini kwenye ghorofa moja chakavu mjini Brescia, Italia.
Desemba mwaka jana alihamia kwenye eneo la Manchester ili kuwa karibu na mwanae mtukutu, ambaye sasa ana miaka 21.
Chanzo cha habari kimesema: "Wakati alipokuja kutoka Italia akiwa na binti yake, Rose, alisema alitaka kuwa karibu na mwanae na kwamba hataki chochote kutoka kwenye utajiri mkubwa alionao mwanae ama raha anazopata kwa sasa.
"Na anaonekana kweli alimaanisha alichosema, akiishi kwa kipato chake kidogo anachopata na kufanya kazi kwa bidii. Ni kazi ngumu anayofanya lakini hapo kabla alikuwa akifanya kazi sokoni hivyo hakika ni mhangaikaji.
Aliongeza: "Mama yake sio mashuhuri sana, hataki Mario ajisikie mwenye mzigo kutokana na yeye kuhamia Uingereza. Anachotaka tu kuunda upya uhusiano wake na mwanae kama ambavyo maam yeyote angetaka kufanya."
Balotelli alimtembelea mama yake katika matukio kadhaa kwenye kijumba chake kidogo, akiegesha gari lake aina ya Bentley jeupe nje.
Yeye na mumewe Thomas, ambao wana asili kutoka Ghana, walishauriwa kumtoa Mario alipokuwa na miaka miwili sababu alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya utumbo mkubwa yaliyokuwa yakitishia maisha yake yaliyochangiwa zaidi na kuishi kwenye makazi duni.
Mama yake alidai baadaye familia ya Balotelli, ambayo ilimuasili Mario, wamembadilisha dhidi ya jamaa zake wa kuzaliwa nao na alilazimika kufanya kazi kubwa kujenga uhusiano naye.
Hivi karibuni alisema: "Mario amekuja kuniona mara chache. Hatuonani wakati wote kutokana na ukweli kwamba ana maisha yake na mimi nina yangu."

No comments: