MADAKTARI WAANZA KUREJEA KAZINI MUHIMBILI...

Huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam, zimerejea katika hali ya kawaida baada ya madaktari kurejea kazini jana Julai mosi. 
Taarifa ya uongozi wa hospitali hiyo iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, ilieleza kuwa tathimini iliyofanyika kuanzia asubuhi saa mbili hadi saa 11 jioni, ilionesha kuwa katika Idara ya Tiba, madaktari bingwa 19 kati ya 21 walifika kazini na watatu wako likizo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotumwa na Ofisa Uhusiano Mwandamizi, Aminiel Aligaesha watumishi wa idara za masijala wote 12 walifika kazini na kliniki zote za tiba zimefanyika kama kawaida. 
Aidha, katika Idara ya Watoto, yenye madaktari bingwa 16, 14 walifika kazini na wengine wawili wako likizo ambapo pia na watumishi wa idara za masijala watatu kati ya sita, walifika kazini ambapo watatu wako likizo. 
Upande wa kliniki za kila siku zenye yenye Registrars saba, Aligaesha alisema sita kati yao walikuja kazini na mmoja yuko likizo. Aidha, madaktari bingwa wote walikuja kazini. 
Idara ya Magonjwa ya Afya ya Akili yenye madaktari bingwa 10, tisa walifika kazini na mmoja yuko masomoni. 
Upande wa Idara ya Dharura, taarifa hiyo ilieleza kuwa watumishi wa idara za masijala 10 walikuja kazini. 
Taarifa hiyo ilieleza kuwa kuhusu huduma za upasuaji, wagonjwa wote waliolazwa wodini walionwa na baadhi ya kliniki za huduma ya upasuaji zilifanyika. Hata hivyo, upasuaji haukufanyika kwani hakukuwa na orodha ya wagonjwa waliopangwa kufanyiwa upasuaji.  
Wakati Muhimbili wakitoa taarifa hiyo, taarifa nyingine iliyolifikia gazeti hili ilidai kuwa madaktari bingwa katika hospitali hiyo walitangaza kuanza mgomo rasmi jana hadi hapo Serikali itakapotangaza kuwarejesha madaktari wote walioko mafunzoni ambao wamefukuzwa.

Msimamo huo wa jumuiya na madaktari bingwa ulitangazwa na wawakilishi wao mara baada ya kufanyika vikao mbalimbali hospitalini hapo.
Mwakilishi huyo, Dk Catherine Mng’ong’ alidai kama ni suala la kufukuzwa kazi, wao madaktari bingwa wako tayari lakini hawawezi kufanya kazi bila kuwepo kwa madaktari walioko mafunzoni.

No comments: