Haya ni maisha ya kipekee ya Faustino Barrientos, mchunga ng'ombe ambaye ameishi zaidi ya miaka 46 katika upweke kando ya Ziwa O'Higgins, moja ya kona zinazofikika kwa shida sana duniani.
Tangu mwaka 1965, Barrientos amekuwa akifanya kazi kama mchunga ng'ombe, mwendeshaji farasi kwenye ranchi na mchunga kondoo anayeishi eneo la kusini mpakani mwa Chile na Argentina.
Desemba mwaka jana, alitembelewa na waandishi wa habari kutoka chombo binafsi cha habari cha mjini Brooklyn, New York. Iliwachukua waandishi siku nne kufika nyumbani kwake, nyumba iliyojengwa kutokana na boti ya wokovu ya uvuvi.
"Sihitaji pesa," aliwaambia waandishi baada ya kuwakaribisha nyumbani kwake. "Nina chakula cha kutosha. Maisha yanakuwa mazuri unapokuwa peke yako.
"Wanataka kuniondoa hapa lakini hawawezi. Ninaishi hapa hadi mwisho kabisa."
Barrientos amekulia kwenye ufuko wa Ziwa O'Higgins lakini baada ya ndugu zake 11 kuhama na Pinochet kuanza kuanza kupandisha mabavu ya utawala wake, akahamia Argentina.
Wakati akisafiri maeneo mbalimbali nchini humo na kufanya kazi za ujenzi, alipata mbinu za kujikimu mwenyewe wakati aliporejea kwenye majabali, eneo la milima la Patagonia huko Chile.
Ziwa O'Higgins ni moja kati ya maeneo yasiyofikika kwa urahisi katika Patagonia na ndio mkoa wenye idadi ndogo ya watu katika Chile. Pia ni moja kati ya sehemu zenye idadi ndogo kabisa ya watu duniani nje ya Antarctica.
Ardhi ya Barrientos ina majengo mawili, kibanda kidogo ambako analala, kula, kusikiliza redio na kusomea magazeti ambayo huletewa mara mbili kwa mwaka.
Jengo jingine huhifadhia makasha ya chakula, mapipa ya supu, magunia ya sukari na unga ambavyo huletwa kwa boti ambayo inakatiza kona zake zilizo kimya kabisa kila baada ya siku kumi.
Pia anaishi kwa kutegemea ng'ombe na kondoo katika ardhi yake, na amekuwa akifuatilia muda kupitia kalenda yake ambayo huchora mstari kila siku inayopita.
Kila baada ya miaka miwili amekuwa akiswaga mifugo yake kwa siku mbili kwenye bustani iliyoko Ziwa O'Higgins, ambako huishi jamii ndogo ya watu wapatao 100 umbali wa maili 25 kutoka kwake.
Anaongoza mifugo yake kwenye korongo na kuvuka mito kuelekea mjini. Huko huuza mifugo, na kujiongezea pesa za kutosha kwa ajili ya maisha yake yasiyotaka makuu.
Anafurahia huduma bora za kisasa, kuendelea na siasa na matokeo ya michezo kupitia redio yake akiwa nyumbani kwake. Amewahi kutazama televisheni mara moja tu katika maisha yake.
"Ni vema kujua kinachoendelea huko nje," alisema. Redio ndio njia yangu pekee inayonifanya nijifunze siasa za nchi mbalimbali. Hivi ndivyo ninavyojifunza mwenyewe kuhusu siasa."
Miaka miwili iliyopita, pale serikali ilipogundua kuwa anamiliki bunduki kadhaa kwenye makazi yake, walikwenda na kufanya naye makubaliano. Walitaka awape bunduki na wao wampatie mitambo ya umeme wa nguvu ya jua.
Aliwapa kama walivyotaka katika ofa yao, lakini anasema mara chache anatumia mitambo hiyo ya nguvu ya jua. Na akaongeza, hata hivyo ameshapata bunduki mpya. "Nimepata nyingine zaidi lakini sasa sitowakabidhi," alisema.
Lakini maisha yake yamezidi kuwa mzigo kutokana na maisha ya kisasa. Takribani miaka 10 iliyopita, meli za serikali zilianza kurandaranda ziwani humo kila wiki.
Sasa, pia kuna meli ya utalii ambayo inawatembeza wageni kuona barafu ya O'Higgins kila baada ya siku kumi.
Pia ana watu wanaopanga kwenye ardhi yake, mtu na mkewe ambao wameleta mifugo yao na kujichanganya na wa Barrientos. Wapangaji hao wamemuelezea Barrientos kama mtu wa kushangaza mwenye ushirikiano mkubwa.
Barrientos anaonekana kwenye filamu hapo juu iliyopigwa Desemba mwaka jana. Timu ndogo ilikwenda kuzungumza naye kuhusu mabadiliko ya sura ya Patagonia na maisha ya ufugaji ng'ombe.
No comments:
Post a Comment