KAMATI YA BUNGE YA MADINI YAVUNJWA...

Spika wa Bunge, Anne Makinda ameivunja Kamati ya Nishati na Madini kutokana na tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo.
Uamuzi huo aliutangaza jana bungeni muda mfupi baada ya Bunge kupitisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini na kusema kuwa pia kamati nyingine za Bunge ambazo zinatuhuma mbalimbali atazifanyia kazi na atachukua hatua ya kuzivunja.
Hatua hiyo ya Spika Makinda ilitokana na hoja iliyotolewa na Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa (CCM), aliyetaka Kamati ya Nishati na Madini ivunjwe kutokana na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo kutuhumiwa masuala ya rushwa.
Pia Kawawa alitoa hoja kuwa licha ya Kamati hiyo ya Nishati na Madini, ambayo Mwenyekiti wake ni Mbunge wa Bukene, Suleiman Zedi (CCM), pia kamati nyingine ambazo zimepata kutuhumiwa masuala mbalimbali ya rushwa nazo pia zivunjwe.
Mbunge huyo alisema suala la kuwepo wabunge wanaotuhumiwa kuchukua rushwa limedhalilisha Bunge, hivyo kuomba pia lifanyiwe kazi na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo, Hassan Ngwilizi, ili watakaobainika wachukuliwe hatua.
Akizungumza wakati akijibu hoja hiyo, Spika Makinda alisema hoja hiyo ipo wazi na ni tabia mbaya ambayo inalidhalilisha Bunge na kuwaonya wabunge kuwa wasipokuwa makini wanakwenda kubaya, kwani hawawezi kuisimamia Serikali wakati wanaomba vitu mbalimbali.
Alisema unaweza kukuta Mbunge anachangia hoja huku jasho likimtoka kumbe anafanya kazi ya kutumwa na mtu kwa maslahi binafsi na kuwa ameagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kutengeneza kanuni za maadili na mtu yeyote atakayetuhumiwa katika mazingira ya rushwa lazima hatua kubwa zichukuliwe.
"Serikali yetu na nchi yetu inapita katika kipindi cha mpito na kama nyie wabunge hamtakuwa imara kuweza kuisimamia Serikali kwa ukweli hatutaweza kwenda matumaini ya wananchi yako wapi kama si Bunge?
"Kitendo hiki kwa kweli hakikubaliki ndani ya Bunge, hatuwezi kuisimamia Serikali huku tunapokea pokea, unaisimamiaje Serikali kwa mtindo huu?
"Kwa hiyo ninaamini wabunge mkikaa vizuri na kufanya kazi yetu vizuri mabadiliko makubwa katika Serikali yatatokea, lakini wenzetu wanakwenda huko mara wajipendekeze mara waombe hiki hatuwezi kwenda hivyo," alisema na kuongeza kuwa kwa kutumia kanuni hiyo 53(3) amelipeleka suala hilo katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, ili walifanyie uchunguzi na kuleta taarifa bungeni.
"Mliokuwa mkitaka watajwe sasa hiyo kamati itafanya kazi hiyo, ya pili kwa kutumia kanuni 113 (3) baada ya kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Kawawa, naridhia ombi hilo nitaivunja na nyingine ambazo zimeonekana zikilalamikiwa katika hili," alisema.
Wajumbe wanaounda Kamati ya Nishati na Madini iliyotangazwa kuvunjwa jana licha ya Mwenyekiti Zedi ni Diana Chilolo ambaye ni Makamu Mwenyekiti, Yussuf Haji Khamis, Mariam Kisangi, Catherine Magige, Abia Nyabakari, Charles Mwijage, Yusuph Nassir, Christopher ole Sendeka na Dk Festus Limbu.
Wengine ni Shafin Amedal Sumar, Athumani Mfutakamba, Lucy Mayenga, Josephine Chagulla, Mwanamrisho Abama, David Silinde, Suleiman Nchambis Suleiman, Kisyeri Chambiri, Ali Mbarouk Salim, Sarah Ali Msafiri, Munde Abdallah Tambwe, Vicky Kamata na John Mnyika.
Katika michango mbalimbali ya wabunge juzi na jana kwa wizara hiyo, zilitolewa tuhuma mbalimbali kwa baadhi ya wabunge na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kuhongwa na kampuni za mafuta kwa ajili ya kutaka wamshinikize Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospter Muhongo na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakim Maswi wang’oke katika nyadhifa zao.
Katika mjadala huo baadhi ya wabunge walipokuwa wakichangia, waliwatuhumu baadhi ya wabunge wenzao kwamba wanawaunga mkono mafisadi na kumtisha Waziri Muhongo na Katibu Mkuu Maswi kwa madai ya kukiuka sheria ya manunuzi ya umma na kuwa wabunge hao walikuwa wakifanya hivyo kwa shinikizo la baadhi ya kampuni za mafuta.
Ilidaiwa na baadhi ya wachangiaji kuwa baadhi ya wabunge wamekuwa wakiendesha kampeni kutaka watendaji hao wang'oke kwa madai walikiuka sheria ya manunuzi ya umma na kuipa zabuni Kampuni ya Puma Energy na kuwa baadhi ya wabunge walienda mbali zaidi kwa kumtumia ujumbe wa vitisho Maswi kwa simu yake ya kiganjani.

No comments: