HALI YA DK ULIMBOKA YABADILIKA GHAFLA, SASA HAJITAMBUI AFRIKA KUSINI...


Kurejea tena mgomo wa madaktari na kuwaacha wagonjwa bila huduma katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Taasisi ya Mifupa (MOI) inadaiwa kumetokana na kubadilika ghafla hali ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Dk Steven Ulimboka.
Hospitalini hapo palikuwa na umati mkubwa wa wagonjwa hasa katika taasisi ya MOI lakini kinyume na matarajio yao wengi wao waliishia kurudishwa nyumbani huku sababu ikitolewa kuwa hakuna madaktari.
Mmoja wa madaktari hospitalini hapo alisema kuwa chanzo cha mabadiliko ya madaktari hao ni taarifa zilizowafikia mapema asubuhi jana kuwa Dk Ulimboka aliyeko Afrika Kusini akitibiwa hali yake ni mbaya na hajitambui.
"Kweli tulisharejea kazini na kuanza kutoa huduma lakini tumepata taarifa kuwa Dk Ulimboka anapumulia mashine na hajitambui, hili limetuchanganya sana," alisema daktari huyo.
Aidha chanzo kingine hospitalini hapo kilithibitisha kuwapo kwa taarifa za hali ya Dk Ulimboka kuzidi kuwa mbaya na kuwa baada ya taarifa hizo kusambaa, madaktari waliokuwa kazini walichanganyikiwa na kutawanyika.
Wagonjwa walionekana wakiwa wamejikusanya nje ya MOI huku wengine waliowahi wakithibitisha kutibiwa na wengine waliochelewa wakidai kufunguliwa kadi na kuishia kupangiwa tarehe ya kuonana na daktari kwa kuwa kwa muda huo hakuna madaktari.
Katika eneo la MOI lililokuwa limefurika watu kutokana na menejimenti ya taasisi hiyo juzi kutangaza kuwa mgomo haupo katika taasisi hiyo, lilianza kuonekana kupwaya kwa kuwa kadri muda ulivyokuwa unaenda, watu walizidi kupungua ambapo hadi kufikia saa sita mchana hakukuwa na wagonjwa kabisa.
Msemaji wa taasisi hiyo, Jumaa Almasi alipoulizwa kuhusu hali hiyo hakuzungumza chochote zaidi ya kudai kuwa wagonjwa wanatibiwa na huduma zinaendelea kama kawaida.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) Dk Rodrick Kabangila, alikiri kusikia tetesi za hali ya Dk Ulimboka kubadilika na kuwa mbaya huku wengine wakidai amefariki dunia jambo ambalo aligoma kuthibitisha.
"Naomba nisizungumze chochote kuhusu hali mbaya ya Dk Ulimboka au kwamba amefariki… sina uhakika na hayo na mimi pia nimeyasikia, ila taarifa niliyonayo tangu jana jioni (juzi) hali yake ilikuwa inaendelea hiyo hivyo," alisema Dk Kabangila bilakufafanua.
Aidha daktari huyo, alisema kwa sasa wanajiandaa na maandamano makubwa ya amani ambayo hakutaja lini na wapi yataanzia ma kuishia akidai kuwa hizo ni taarifa za ndani bado hazijafanyiwa kazi na kwamba zikikamilika zitatangazwa.
Pamoja na hayo jana jioni uvumi ulienea kuwa Dk Ulimboka amefariki huku uvumi mwingine ukidaiwa kuwa hali yake ni mbaya sana na anapumulia mashine jambo ambalo liliwaweka katika wakati mgumu madaktari.
Juzi Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MOI Balozi Charles Mutalemwa akiongozana na menejimenti ya taasisi hiyo, walitangaza rasmi mgomo kuisha katika taasisi hiyo kutokana na juhudi za menejimenti hiyo kuwasihi madaktari kurejea kazini.

No comments: