KESI YA PAUNI 2,000 YAMSABABISHIA BIBI KULIPA PAUNI 30,000...


Bibi anakabiliwa na hatari ya kupoteza nyumba na biashara yake baada ya gharama za kesi kupaa ghafla na kufikia Pauni za Uingereza 30,000 kwa kazi ya kupigania kukwepa kulipa fidia ya Pauni za Uingereza 2,000 tu.
Jean Taylor mwenye miaka 52, alishitakiwa na fundi wa gesi baada ya kuteleza na kuanguka kwenye sakafu iliyokuwa na unyevu kwenye mgahawa wa bibi huyo wakati akisoma mita yake.
Mdai Richard Newsham mwenye miaka 67, ambaye alivunjika mbavu zake mbili alipoanguka ameuamuru mgahawa huo kufanya utaratibu wa kumlipa fidia kwa kumsababishia majeraha wakati akitekeleza majukumu yake.
Baadaye mdai huyo alilipwa Pauni za Uingereza 2,000 baada ya kukubaliana kumaliza suala hilo nje ya mahakama mwaka 2008 lakini kampuni ya uwakili ambayo hujinadi kwa kaulimbiu yake ya "Wawekezaji kwa Wananchi", kisha kumtwika Bibi Jean gharama za kesi za awali kiasi cha Pauni za Uingereza 20,000.
Bibi Jean ambaye ameendesha mgahawa huo wa Jean's Diner uliopo Ribbleton Lane, mjini Preston kwa miaka 10 alipinga kiwango cha ada ya uwakili lakini akashindwa kesi yake ya kupinga ada hiyo kwenye mahakama ya Preston County.
Mwezi uh alishindwa kesi, ambayo ilisikilizwa kwenye mahakama ya Preston County na kusema aliamriwa kulipa Pauni za Uingereza 30,000, bili ambayo inatakiwa kulipwa kutokana na biashara yake ya kusambaza chakula kwa wateja. Tayari ameshalipa zaidi ya Pauni za Uingereza 3,500 kwa ajili ya mawakili wake binafsi.
Bibi Jean alisema: "Nitaweza kupoteza biashara yangu au nyumba yangu. Nimekasirika sana. Wakati hukumu ikitolewa, niliishiwa nguvu kabisa. Nililazimika kuondoka kwenda kutuliza akili yangu.
"Hatuwezi kuelewa jinsi ilivyokwenda mbali hivyo kwa jambo dogo tu. Tumepambana kwa miaka mingi.
"Nilitoa ofa ya kujaribu kulipa Pauni za Uingereza 50 kila wiki, lakini nikaambiwa natakiwa kulipa kiasi kisichopungua Pauni za Uingereza 1,500 kwa mwezi.
"Biashara yangu ndio kwanza imeanza kuimarika baada ya kunusurika kufilisiwa eneo la Ribbleton Lane, ambapo inatuumiza sana. Nimefanua kazi bila malipo kwa miezi sita wakati nikiendelea na shughuli hii. Ni kwamba siwezi kulipa."
Bibi Jean, mama wa watoto watatu na wajukuu wanne, amesema mama yake na mjukuu wake wa kike wote wameajiriwa kwenye biashara yake hiyo ndogo.
Wanasheria wake wamesema kA sababu amekaidi kulipa gharama za mawakili wa mdai wake, Marsden Rawsthorn, wakati walipofikia gharama ya Pauni za Uingereza 20,000, sasa atalazimika kubamizwa na bili ya Pauni za Uingereza 30,087.39, ambayo imejumusisha riba na 'ada ya mafanikio'.
Jane Gale, mshirika wa mawakili wa O'Donnell ambao walisimama kwa niaba ya Bibi Jean, wamesema: "Nafasi ya Bibi Jean ni ya kutisha, na ni matokeo ya moja kwa moja ya hatua zilizochukuliwa na Serikali na sekta ya bima.
"Wadai wamechukua hatua kwa msaada wa kisheria, ambapo gharama zinadhibitiwa.
Mawakili wa Richard, Marsden Rawsthorn ambao wana ofisi zao mjini Preston na Chorley wamesema hawawezi kutolea maoni kesi binafsi bila ruhusa ya wateja wao.

No comments: