BAJETI YA WIZARA YA NISHATI NA MADI KWA MWAKA WA FEDHA 2012 - 2013...


HOTUBA YA WAZIRI WA NISHATI NA MADINI MHESHIMIWA PROF. SOSPETER MWIJARUBI MUHONGO (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA  MATUMIZI  KWA MWAKA 2012/13

UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba kutokana na Taarifa iliyowasilishwa leo ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, iliyochambua Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Utekelezaji ya Mwaka 2011/12 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara na Taasisi zilizo chini yake kwa Mwaka 2012/13. 
Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba kutumia nafasi hii kumshukuru Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani yake kubwa kwangu kwa kuniteua kuwa Mbunge na Waziri wa Nishati na Madini. Uteuzi huu ni dhamana kubwa na changamoto kwangu, hususan katika kuhakikisha kuwa sekta za nishati na madini zinachangia ipasavyo katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Naahidi kwa neema ya Mwenyezi Mungu kuyatekeleza majukumu aliyonipa kwa uadilifu kwa kushirikiana na Bunge lako Tukufu pamoja na wananchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee namshukuru Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilali na Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb.) kwa miongozo na ushirikiano wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu. Nitumie nafasi hii pia kukupongeza wewe Mhe. Anne Semamba Makinda (Mb.) na Naibu Spika Mhe. Job Yustino Ndugai (Mb.), kwa namna ya pekee mnavyosimamia shughuli za Bunge hili. Aidha, nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote walioteuliwa kuongoza Wizara mbalimbali. Pia, nawapongeza Mhe. George Boniface Simbachawene (Mb.) na Mhe. Stephen Julius Masele (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Naibu Mawaziri wa Wizara ya Nishati na Madini. Katika kipindi kifupi nilichofanya nao kazi wamenipa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yangu na wameonesha uwezo mkubwa katika uongozi. Nawashukuru sana. 
Mheshimiwa Spika, nampongeza Mhe. Musa Zungu Azzan (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge hili. Aidha, nawapongeza Wenyeviti wote wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa jinsi wanavyosimamia majukumu yao. Kwa namna ya pekee natoa shukrani zangu za dhati kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Selemani Jumanne Zedi (Mb.), Makamu Mwenyekiti Mhe. Diana Mkumbo Chilolo (Mb.) na wajumbe wote wa Kamati kwa ushauri na ushirikiano unaolenga kuimarisha utendaji wa Wizara. Nakiri kuwa Kamati hii imefanya kazi kubwa ya kuchambua kwa kina mapendekezo ya Bajeti ya Wizara kwa Mwaka 2012/13 na kutoa ushauri wa msingi kuhusu Bajeti hiyo. Ushauri huo umetuwezesha kufika hapa tulipo leo na kutoa mwelekeo mpya wa namna bora ya kuendesha na kusimamia ustawi wa sekta za nishati na madini. 
Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, naomba kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Shughuli za Wizara ya Nishati na Madini kwa Mwaka 2011/12. 

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA WIZARA KWA MWAKA 2011/12 
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2011/12 ulikuwa wenye changamoto nyingi kwa Wizara ya Nishati na Madini ikiwemo kuondoa mgawo wa umeme nchini. Pamoja na changamoto hizo, Wizara imetekeleza majukumu yake kwa kiwango cha kuridhisha.
Ukusanyaji wa Mapato
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2011/12, Wizara ilipangiwa lengo la kukusanya jumla ya Shilingi 131,266,153,300. Hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2012 jumla ya Shilingi 138,094,409,550, sawa na asilimia 105 ya lengo zilikusanywa. Lengo hili limefikiwa kutokana na kuimarika kwa usimamizi na ufuatiliaji wa ukusanyaji wa maduhuli kutoka sekta za nishati na madini kwa mujibu wa sheria zilizopo. 
Matumizi
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2011/12, Wizara iliidhinishiwa jumla ya Shilingi 402,402,071,000 ili kutekeleza majukumu yake. Kati ya fedha hizo, Shilingi 76,953,934,000, sawa na asilimia 19.12 zilikuwa ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 325,448,137,000, sawa na asilimia 80.88 ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Hata hivyo, Bajeti hiyo iliongezeka kwa Shilingi 136,112,000,000 baada ya kufanyika uhamisho na kufikia Shilingi 538,514,071,000.
Mheshimiwa Spika, uhamisho wa fedha uliofanyika katika kipindi husika ulikuwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya dharura ya kufua umeme ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mafuta mazito ya kuendesha mitambo ya kufua umeme; malipo kwa mkandarasi anayejenga mitambo ya kufua umeme wa MW 60 huko Nyakato, Mwanza; na ulipaji wa madeni ya TANESCO. 
 Mheshimiwa Spika, jumla ya fedha zilizopokelewa na Wizara kutoka Hazina hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Juni, 2012 zilikuwa Shilingi 453,223,402,600 sawa na asilimia 84.16 ya bajeti ya Wizara kwa Mwaka 2011/12. Kati ya fedha hizo, Shilingi 297,708,810,730 zilikuwa ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo, sawa na asilimia 65.69, ambapo Shilingi 267,326,750,000 sawa na asilimia 89.79 ya fedha za maendeleo zilizopokelewa zilikuwa fedha za ndani na Shilingi                         30,382,060,730 sawa na asilimia 10.21 ya fedha za maendeleo zilizopokelewa ni fedha za nje. Aidha, Shilingi 155,514,591,870 zilikuwa ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, sawa na asilimia 34.31 ya fedha zilizopokelewa katika Mwaka 2011/12.
Utekelezaji wa Shughuli Zilizopangwa katika Sekta ya  Nishati 
Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa kutekelezwa kwa Mwaka 2011/12 katika Sekta ya Nishati ni pamoja na kuongeza ufuaji wa umeme; upanuzi na uboreshaji wa njia za kusafirisha umeme; kuwezesha upelekaji wa umeme vijijini; kutekeleza miradi ya Tanzania Energy Development and Access Expansion Project (TEDAP); kuimarisha na kupanua miundombinu ya gesi asili na mafuta; kuendeleza shughuli za utafutaji wa gesi asili na mafuta; kuendeleza nishati jadidifu (renewable energies); na kudurusu na kuandaa sera za nishati.
 Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza kazi zilizopangwa kwa Mwaka 2011/12, Wizara ilifanikiwa kuondoa mgawo wa umeme kwa kutekeleza Mpango wa Dharura wa Umeme nchini; kukamilisha ujenzi wa mtambo wa kufua umeme kwa kutumia gesi asili wa MW 105 Dar es Salaam (Ubungo II); kununua mitambo ya MW 18 ya Mtwara kutoka Kampuni ya Wentworth; kukamilisha ufungaji na uzinduzi wa jenereta za kufua umeme katika Wilaya za Kasulu, Kibondo, Ngorongoro, Songea na Sumbawanga; kuzindua ufuaji umeme kwa kutumia maporomoko madogo ya maji kW 300 – Mawengi (Wilaya ya Ludewa), mwezi Novemba, 2011 ambapo zaidi ya kaya 300 ziliunganishiwa umeme; kukamilisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kV 33 ya kuunganisha Mtwara na Msimbati; kukamilisha ujenzi wa njia za umeme za msongo wa kV 33 kwa maeneo ya Mgwashi (Tanga)  na Mbwewe (Pwani) na kukamilisha Tathmini ya Matumizi ya Nishati Vijijini Mwaka 2011 inayoonesha kuwa hadi  kufikia Disemba, 2011 kiwango cha asilimia 6.6 ya Watanzania waishio vijijini wameunganishiwa umeme, hii ni sehemu ya asilimia 18.4 ya Watanzania wote waliounganishiwa umeme kwa sasa.   
 Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine ni kusainiwa kwa mkataba wa mkopo kati ya Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China tarehe 20 Juni, 2012 kwa ajili ya ujenzi wa mtambo wa kusafisha gesi asili katika maeneo ya Songo Songo na Mnazi Bay, na ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asili kutoka Mnazi Bay kupitia Somanga Fungu hadi Dar es Salaam; kusainiwa kwa mikataba mitano (5) ya uzalishaji na ugawanaji wa mapato ya mafuta na gesi asili katika maeneo ya Rukwa, Kyela, Kilosa, Pangani na Kitalu Na. 8 kilichopo Mashariki mwa Mafia; kugunduliwa kwa gesi asili katika maeneo ya Mtwara kisima cha Ntorya - I na visima vilivyopo kina kirefu cha bahari vya Zafarani – I, Jodari – I, Mzia – I; na Lavani - I (Lindi); na kuanza kwa utekelezaji wa  Mpango wa Uagizaji wa Mafuta wa Pamoja (Bulk Procurement) mwezi Januari, 2012.
Utekelezaji wa Shughuli Zilizopangwa katika Sekta ya  Madini
  Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2011/12, maeneo yaliyopewa kipaumbele katika Sekta ya Madini ni kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli; kusimamia Sheria ya Madini ya Mwaka 2010; kuhamasisha uwekezaji katika Sekta ya Madini; kuendeleza uchimbaji wa kati na mdogo ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo ya uchimbaji mdogo; kuimarisha Mfuko wa Wachimbaji Wadogo; kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo; kuendelea kuimarisha ukaguzi wa shughuli za migodi ili kuongeza usalama, afya na mazingira bora; kuimarisha Mfumo wa Usimamizi na Utoaji Leseni za Madini katika ofisi ya Makao Makuu ya Wizara  na ofisi za Madini za Kanda na Afisa Madini Mkazi ili kuongeza kasi ya utoaji  leseni; kuimarisha na kuwezesha mashirika/taasisi zilizo chini ya Wizara ambazo ni STAMICO, GST, TMAA na Chuo cha Madini, Dodoma (MRI) kutekeleza majukumu yake ipasavyo; na kudurusu sheria mbalimbali za madini.
  Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Madini ni pamoja na migodi mikubwa nchini yenye mikataba (MDAs) kuanza kulipa mrabaha wa asilimia 4 ya mauzo ya madini kulingana na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010; kulipwa kwa Shilingi bilioni 188.1 za kodi ya mapato Serikalini kutoka Kampuni ya Geita Gold Mine Limited na Shilingi bilioni 37.2 kutoka Kampuni ya Resolute Tanzania Limited kulikowezeshwa na ukaguzi uliofanywa na Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA); kuanzishwa kwa vocha za mauzo ya madini ya ujenzi zilizowezesha kukusanywa kwa mrabaha wa Shilingi milioni 350.59 ikilinganishwa na Shilingi milioni 30 zilizokuwa zinakusanywa kwa mwaka katika kanda zote za madini;  na kutolewa kwa leseni za madini 1,097 za utafutaji mkubwa wa madini, 19 za uchimbaji wa kati; na 9,997 za uchimbaji mdogo wa madini.
 Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine ni kusainiwa kwa makubaliano ya ubia kati ya STAMICO na Tanzania American International Development Corporation (2000) Limited (TANZAM 2000) na kuunda kampuni ya ubia, ambapo STAMICO inamiliki hisa asilimia 45 na TANZAM 2000 asilimia 55; na kusainiwa kwa makubaliano ya ubia kati ya STAMICO na Obtala Resources Limited na kuanzisha Kampuni ya ubia (Stabtala Investments) kwa hisa asilimia 50 kwa 50. Kampuni ya Stabtala Investments itaingia ubia na Watanzania wenye leseni kwa ajili ya kufungua migodi ya dhahabu yenye ukubwa wa kati. Mafanikio mengine ni kutengwa kwa eneo la Itandula la uchimbaji mdogo wa madini lenye jumla ya hekta 37 lililoko Wilayani Tarime na hekta 15,605 eneo la Mbesa Wilayani Tunduru; kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo 380 katika Mikoa ya Lindi, Kigoma, Singida, Morogoro, Manyara na Tabora; kubadilisha ramani 33 kutoka kwenye mfumo wa analogue kwenda kwenye mfumo wa digital na kuingizwa kwenye kompyuta documents meta-data zipatazo 1,206; kufanyika kwa uchoraji wa ramani za kijiolojia na kijiokemia katika QDS 194, 212, 230 na 148; na kukamilika kwa ujenzi wa Ofisi ya Madini ya Kanda ya Kati – Singida. 

Changamoto Zinazokabili Sekta za Nishati na Madini
 Mheshimiwa Spika, licha ya mafanikio yaliyopatikana, Sekta ya Nishati imeendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kukidhi kasi ya ukuaji wa mahitaji ya umeme; uchakavu wa miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme; kufikia lengo la asilimia 30 ya Watanzania ambao wameunganishiwa umeme ifikapo 2015; kupunguza upotevu wa umeme; kuwa na miundombinu ya gesi asili inayokidhi mahitaji; upungufu wa umeme kutokana na ukame uliosababisha kupungua kwa maji katika mabwawa makubwa ya kuzalisha umeme;  kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia; na upatikanaji wa vifaa hapa nchini kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya umeme. 
 Mheshimiwa Spika, changamoto katika Sekta ya Madini ni pamoja na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa; kuongeza fungamanisho la Sekta ya Madini na sekta nyingine za uchumi; ukuaji wa kasi wa shughuli za uchimbaji usio rasmi; biashara haramu ya madini; upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa bidhaa za madini; mtaji mdogo wa uwekezaji kwenye uchimbaji mdogo; kushughulikia masuala ya fidia na uhamisho kupisha shughuli za migodi; migogoro ya kimaslahi na mahusiano baina ya wadau wa Sekta ya Madini; na uharibifu wa mazingira katika maeneo ya migodi na mfumuko wa madini. 
SEKTA YA NISHATI
Hali ya Uzalishaji Umeme
  Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2011/12, Wizara iliendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuboresha upatikanaji wa nishati ya umeme nchini. Hadi mwezi Juni, 2012 uwezo wa mitambo ya kufua umeme (installed capacity) ulikuwa MW 1,375.74 (gesi asili - asilimia 40, maji - asilimia 41 na mafuta - asilimia 19). Uwezo huo ni ongezeko la MW 367 sawa na asilimia 36 ikilinganishwa na uwezo wa MW 1,013.74 uliokuwepo mwezi Juni, 2011. Mwaka 2011 kiasi cha umeme kilichoingizwa kwenye Gridi ya Taifa kilikuwa MWh 5,153,400 ikilinganishwa na MWh 5,189,320 Mwaka 2010. Aidha, mahitaji ya juu ya umeme kwa Mwaka 2011/12  yalifikia wastani wa MW 820.35, ikilinganishwa na MW 730 kwa Mwaka 2010/11.
Kuongeza Uzalishaji wa Umeme

Mpango wa Kuondoa Mgawo wa Umeme Nchini
 Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa mwezi Julai, 2011 wakati bajeti ya Wizara yangu ilipowasilishwa katika Bunge hili, nchi yetu ilikuwa katika mgawo wa umeme. Mgawo huo ulitokana na upungufu wa umeme wa takriban MW 300 uliosababishwa na upungufu wa maji katika mabwawa kwenye vituo vya kufua umeme. Kufuatia hali hiyo, Serikali ililazimika kuandaa Mpango wa Dharura wa Kuondoa Mgawo wa Umeme nchini ulioridhiwa na Bunge hili. Katika Mpango huo, jumla ya MW 572 zilipangwa kuzalishwa na kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa.  
 Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Juni, 2012 uwezo wa ufuaji umeme kutokana na Mpango wa Dharura wa Kuondoa Mgawo wa Umeme ulifikia jumla ya MW 422. Mitambo hiyo inajumuisha Symbion MW 137, Aggreko MW 100; IPTL MW 80; na Mtambo wa Gesi Asili wa Ubungo - II MW 105. Kutokana na kukosekana kwa mitambo ya MW 150 ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) iliyokadiriwa kugharimu Dola za Marekani milioni 162, sawa na Shilingi bilioni 259.20, lengo la awali la Mpango wa Dharura lilipungua kutoka MW 572 hadi MW 422.
 Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Juni, 2012 lengo la kuondoa mgawo wa umeme lilifikiwa kwa asilimia 100. Kwa sasa hakuna mgawo wa umeme kwa kuwa upungufu uliokuwepo ulikuwa ni kati ya MW 260 na MW 300 ikilinganishwa na uwezo wa MW 422 uliyoongezeka. 

Mitambo ya Kufua Umeme ya MW 105 Dar es Salaam na MW 60 Mwanza

 Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2011/12, Serikali ilikamilisha ujenzi wa mtambo wa kufua umeme wa MW 105 Ubungo II, Dar es Salaam na kuzinduliwa rasmi tarehe 01 Julai, 2012. Mradi huo uligharimu jumla ya Dola za Marekani milioni 125, sawa na Shilingi bilioni 200 kwa udhamini kutoka Serikali ya Norway. Sambamba na mtambo huo, kazi za ufungaji wa mtambo wa kufua umeme wa MW 60 Nyakato - Mwanza ziliendelea chini ya Kampuni za M/S SEMCO Maritime AS na Rolls Royce Marine AS zote za Norway. Gharama za mradi huo ni Dola za Marekani milioni 75, sawa na Shilingi bilioni 120. Mradi huo ulipangwa kukamilika mwezi Juni, 2012. Hata hivyo, kutokana na kuchelewa kupatikana kwa fedha, mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba, 2012.
Kujenga Bomba la Kusafirisha Gesi Asili kutoka Mtwara Hadi Dar es Salaam

  Mheshimiwa Spika,  mwezi Septemba, 2011 TPDC kwa niaba ya Serikali ilisaini Mkataba wa Usanifu, Ununuzi na Ujenzi yaani Engineering, Procurement and Construction (EPC) na “China Petroleum Technology and Development Corporation (CPTDC)” kwa ajili ya ujenzi wa bomba na mitambo ya kusafisha gesi asili. Aidha, mwezi Juni, 2012 Serikali ilisaini makubaliano ya mkopo nafuu na Benki ya Exim ya China kwa ajili ya ujenzi wa mitambo ya kusafisha gesi asili na bomba la kusafirisha gesi asili kutoka Mnazi Bay - Mtwara na Songo Songo Kisiwani (Lindi) hadi Dar es Salaam. Gharama za mradi huu ni Dola za Marekani milioni 1,225.3, sawa na Shilingi trilioni 1.96. Kati ya fedha hizo asilimia 95 ni mkopo nafuu kutoka Benki ya Exim ya China na Serikali itachangia asilimia 5, sawa na Dola za Marekani milioni 61.26 zitakazolipwa kwa awamu tatu.
 Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zilizofanyika chini ya mradi huo ni tathmini ya fidia ya mali katika mkuza wa bomba iliyokamilika mwezi Mei, 2012; tathmini ya athari za kijamii na kimazingira (ESIA) iliyokamilika mwezi Aprili, 2012 na kuridhiwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC); na kukamilisha taratibu za kumpata mshauri wa kusimamia utekelezaji wa mradi. 
Mitambo ya Kinyerezi I-MW 150 na Kinyerezi II-MW 240

  Mheshimiwa Spika, mwezi Juni, 2012 Serikali ilipata udhamini wa fedha kutoka Norwegian Export Credit Agency kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Kinyerezi I-MW 150. Mradi huu utagharamiwa na Serikali kwa njia ya mkopo, ambapo Dola za Marekani milioni 166.3, sawa na Shilingi bilioni 261.3 zitahitajika. Aidha, Serikali kupitia TANESCO ilifanya majadiliano na Kampuni ya Sumitomo kwa ajili ya kujenga mtambo wa kufua umeme wa Kinyerezi - II MW 240. Gharama ya mradi huu ni Dola za Marekani milioni 432, sawa na Shilingi bilioni 691.20. Asilimia 85 ya fedha za utekelezaji wa mradi huu zitapatikana kupitia kwa mdhamini, Export Credit Agency for Japan (ECA). Fedha za mkopo zitatolewa na Japan Bank for International Corporation (JBIC), Nippon Export and Investment Insurance, Sumitomo Mitsui Banking Corporation (SMBC) za Japani na asilimia 15 itatolewa na Development Bank of South Africa (DBSA). Mkataba wa EPC ulisainiwa mwezi Juni, 2012. 
 Mradi wa Somanga Fungu MW 320 

 Mheshimiwa Spika, mradi huu wa MW 320 unatekelezwa na Kampuni ya Kilwa Energy Limited ya hapa nchini ikishirikiana na Kampuni ya ETG Power kutoka Dubai. TANESCO inajadiliana na Kampuni ya Kilwa Energy Limited kuhusu mkataba wa kuuziana umeme (Power Purchase Agreement - PPA). Mradi huu unaendelezwa na mwekezaji binafsi na gharama yake ni Dola za Marekani milioni 365, sawa na Shilingi bilioni 584.
 Mradi wa Kufua Umeme wa Mchuchuma MW 600 

  Mheshimiwa Spika, mradi huo unaendelezwa kwa ubia kati ya NDC (asilimia 20) na Kampuni ya Sichuan Hongda ya China (asilimia 80). Mkataba wa ubia (Joint Venture Agreement) kati ya NDC na Kampuni ya Sichuan Hongda ulisainiwa mwezi Septemba, 2011. Kampuni hiyo inaendelea kufanya utafiti wa kuhakiki kiasi na ubora wa makaa ya mawe yaliyopo katika eneo hilo. Kwa sasa, eneo hilo linakadiriwa kuwa na mashapo ya makaa ya mawe kiasi cha tani milioni 454.

 Mradi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka MW 400

  Mheshimiwa Spika, mradi wa Ngaka wa kuzalisha umeme kutokana na makaa ya mawe unatekelezwa na Kampuni ya Tancoal Energy Limited ambayo ni kampuni ya ubia kati ya Serikali kupitia NDC na Kampuni ya Intra Energy Limited. Uchimbaji wa makaa ya mawe umeanza katika mradi huo kwa ajili ya matumizi viwandani na kuuzwa nje ya nchi, hususan Malawi na Msumbiji. Mradi unatarajiwa kuzalisha umeme kiasi cha MW 200 kwa kuanzia ifikapo Mwaka 2015/16 na kuongezeka hadi kufikia MW 400 Mwaka 2017/18. Uwekezaji kwa ajili ya kufua MW 200 utagharimu Dola za Marekani milioni 400, sawa na Shilingi bilioni 640
Mradi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira MW 200

  Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2011/12 Serikali ilifikia mwafaka na Kampuni ya Tan Power Resources Limited ili irejeshe rasmi hisa asilimia 70 ilizokuwa inamiliki katika Kampuni ya Kiwira Coal and Power Limited (KCPL). Aidha, wafanyakazi 398 wa mgodi huo waliachishwa kazi na kulipwa mafao yao ya jumla ya Shilingi bilioni 1.56. Hata hivyo, wamebakizwa wafanyakazi 48 kwa ajili ya kutunza mgodi. Mgodi umekabidhiwa STAMICO ili itafute mbia wa kuendeleza mradi kwa njia ya ushindani. Eneo hilo linakadiriwa kuwa na  tani milioni 35.5 za mashapo ya makaa ya mawe na mradi  utagharimu takriban Dola za Marekani milioni 400, sawa na Shilingi bilioni 640. Hadi Juni 2012, STAMICO imepokea maombi kutoka Kampuni 16 zilizoonesha nia ya kuingia ubia kwa ajili ya kuendeleza mradi huu. 

 Mradi wa Kufua Umeme wa Ruhudji MW 358
 Mheshimiwa Spika, awali mradi huu ulikuwa unaendelezwa na Kampuni ya Aldwych International ya Uingereza. Hata hivyo, Kampuni hiyo iliamua kuungana na Kampuni ya Sithe Global Power Ventures kutoka Marekani mwezi Disemba, 2011 ili kuendeleza mradi huo. Aidha, Makubaliano ya Awali (MoU) kati ya Serikali na Muungano wa Kampuni hizo yalisainiwa mwezi Januari, 2012. Mradi utagharimu takriban Dola za Marekani milioni 900, sawa na Shilingi trilioni 1.44 na utaendelezwa kwa utaratibu wa Public Private Partnership (PPP) kati ya Kampuni hizo na TANESCO. 
Mradi wa Kufua Umeme wa Rusumo MW 75
 Mheshimiwa Spika, taarifa ya upembuzi yakinifu na tathmini ya athari za mazingira zilikamilika mwezi Aprili, 2012. Taarifa hiyo, inaonesha kuwa umeme wa MW 90 ungeweza kuzalishwa ikilinganishwa na MW 63 ya tathmini ya awali. Hata hivyo, kutokana na fidia na athari kubwa za mazingira, nchi washiriki yaani Tanzania, Burundi na Rwanda zimeamua mradi huo uendelezwe bila kuwa na bwawa kubwa (run-of-the river scheme) na kiasi cha MW 75 kifuliwe badala ya MW 90. Kutokana na uamuzi huo, Mshauri wa mradi (Kampuni ya SNC Lavalin kutoka Canada) ameelekezwa kudurusu tathmini ya mazingira. Mshauri huyo atakamilisha kazi ya kudurusu mradi huo ifikapo mwezi Agosti, 2012. Jumla ya gharama za mradi huu ni Dola za Marekani milioni 100, sawa na Shilingi bilioni 160, ambapo mchango wa Serikali ni Dola za Marekani milioni 28, sawa na Shilingi bilioni 44.80.
Mradi wa Kufua Umeme wa Murongo/Kikagati MW 16
 Mheshimiwa Spika, mradi huo unaendelezwa na Kampuni ya Trond Energy kutoka Norway. Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Uganda zimekubaliana kuingia mkataba wa ushirikiano (Bilateral Agreement) ili kuendeleza mradi huo. Majadiliano ya mkataba wa ushirikiano yanaendelea. Mradi huo umepangwa kukamilika ndani ya miezi 30 baada ya kufikiwa makubaliano ya mkopo. Mradi utakapokamilika, utawezesha kila nchi kupata MW 8. Mradi utagharimu takriban Dola za Marekani milioni 30.46, sawa na Shilingi bilioni 48.74

  Mradi wa Kufua Umeme wa Stiegler’s Gorge MW 2,100 

 Mheshimiwa Spika, mwezi Aprili, 2012 Serikali ya Tanzania ilikutana na Serikali ya Brazil kujadili utekelezaji wa mradi wa Stiegler’s Gorge, ambapo mwekezaji binafsi kutoka huko anatarajiwa kuanza kudurusu mradi pamoja na tathmini ya athari za mazingira. Pamoja na ufuaji umeme, mradi huu utahusisha shughuli za uvuvi, utalii, kilimo cha umwagiliaji na kulipatia Jiji la Dar es Salaam maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Gharama za mradi zinakadiriwa kuwa Dola za Marekani bilioni 1.9, sawa na Shilingi trilioni 3.04. Mradi huu unasimamiwa na RUBADA.
Kujenga na Kuimarisha Njia za Kusafirisha Umeme

Mradi wa Kuboresha Mifumo ya Umeme katika Jiji la Dar es Salaam 

 Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2011/12 Serikali iliendelea na juhudi za kuimarisha miundombinu nchini ikiwemo kukarabati njia ya umeme kutoka Ilala mpaka Kurasini kwa kubadilisha waya kutoka milimita za mraba 150 hadi 432, kufunga transfoma za ukubwa wa MVA 15 katika vituo mbalimbali vya kupozea umeme, ambapo kituo cha City Centre kazi imekamilika. Aidha, kazi hiyo inaendelea katika vituo vya Gongolamboto, Kigamboni, Kipawa, Kurasini Mbagala, Mbezi Beach na Ubungo. Kazi nyingine iliyofanyika na kukamilika ni kubadilisha nyaya chakavu katika maeneo hayo. Mradi utatekelezwa kwa gharama ya Dola za Marekani  milioni 75, sawa na Shilingi bilioni 120

Mradi wa TEDAP

 Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2011/12 Serikali iliendelea na ujenzi wa misingi ya nguzo kwa ajili ya njia ya umeme ya msongo wa kV 132 Jijini Dar es Salaam pamoja na vituo vya kupozea umeme, kV 132/33 vyenye uwezo wa MVA 50 eneo la Gongolamboto (Factory Zone II) na Kipawa (Factory Zone III). Aidha, ujenzi wa kituo cha kupozea umeme eneo la uwanja wa ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (KIA) kV 132/33 chenye uwezo wa MVA 40 unaendelea. Miradi hii inatekelezwa kwa udhamini wa Benki ya Dunia. Gharama za mradi ni Dola za Marekani milioni 116, sawa na Shilingi bilioni 185.60.
Mradi wa Iringa - Shinyanga kV 400 (backbone) 
 Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mradi huu, mshauri amekamilisha upembuzi yakinifu wa kuvipatia umeme vijiji vitakavyopitiwa na njia mpya ya umeme. Aidha, Mshauri wa mradi, Kampuni ya Fitchner ya Ujerumani anaendelea na kazi ya kusanifu njia ya usafirishaji umeme na vituo vya kupozea umeme. Mradi utakapokamilika utagharimu Dola za Marekani milioni 650, sawa na Shilingi bilioni 1,040.
Mradi wa Dar es Salaam – Chalinze – Tanga – Arusha kV 400

  Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2011/12 Serikali kupitia TANESCO ilidurusu usanifu wa mradi (redesigning) ili uanzie Dar es Salaam kupitia Chalinze hadi Arusha badala ya kuanzia Morogoro. Uamuzi huu ulitokana na Serikali kuridhia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la gesi asili kutoka Mtwara na Songo Songo kupitia Somanga Fungu hadi Dar es Salaam. Baada ya bomba hilo kukamilika, Dar es Salaam itakuwa kitovu kikuu cha ufuaji umeme nchini na hivyo kuhitaji upanuzi wa mfumo wa usafirishaji umeme. Mwezi Juni, 2012 TANESCO na mkandarasi Kampuni ya TBEA ya China walisaini mkataba wa marekebisho (EPC addendum), hivyo kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme kutoka Dar es Salaam. Mradi huu utatekelezwa kwa mkopo  wa takribani Dola za Marekani milioni 770, sawa na Shilingi bilioni 1,232 kutoka Benki ya Exim ya China.
Mradi wa Ujenzi wa Njia ya Umeme ya kV 220 ya Bulyanhulu – Geita – Nyakanazi 

  Mheshimiwa Spika, mwezi Januari, 2011 Serikali ilisaini mkataba wa mkopo na taasisi ya fedha ya BADEA ya Misri na OFID ya Saudi Arabia. Lengo ni kutekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya umeme kV 220 kutoka Bulyanhulu hadi Nyakanazi kupitia Geita. Kazi ya kuandaa zabuni za kandarasi za ujenzi ilikamilika mwezi Juni, 2012. Mradi utagharimu Dola za Marekani milioni 53, sawa na Shilingi bilioni 84.8.
Mradi wa Makambako - Songea kV 220
 Mheshimiwa Spika, kutokana na kuwepo miradi mingi ya ufuaji umeme katika maeneo ambayo njia ya umeme kutoka Makambako mpaka Songea itapita kama vile Ngaka, Mchuchuma na Masigira, Serikali imeamua kudurusu mradi huo kutoka kV 132 mpaka kV 220. Serikali kupitia TANESCO ilisaini mkataba na Kampuni ya SWECO ya Sweden mwezi Agosti, 2011 kwa ajili ya kuandaa zabuni ya kumpata mkandarasi atakayesanifu na kutekeleza mradi. Tathmini ya fidia kwenye maeneo ambayo njia hiyo itapita inaendelea. Mradi huu unagharimiwa na Serikali ya Sweden kupitia Shirika la Maendeleo la Sweden (Sida) kwa kiasi cha Swedish Kroner milioni 500, sawa na Shilingi bilioni 112.

Upanuzi na Uboreshaji wa Mfumo wa Usambazaji wa Umeme 

Mradi wa Electricity - V
Mheshimiwa Spika, mradi huu unatekelezwa kwa mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na utahusisha usambazaji wa umeme katika vijiji, miji midogo na makao makuu ya wilaya katika Mikoa ya Geita (Bukombe), Mwanza (Magu na Kwimba) na Simiyu (Bariadi) na kukarabati vituo vikubwa vya kupozea umeme kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Arusha. Kazi ya kujenga njia za umeme na vituo vya kupozea umeme itaanza katika Mwaka 2012/13. Gharama za mradi ni Dola za Marekani ni milioni 31, sawa na Shilingi bilioni 49.6.
Miradi iliyo chini ya Ufadhili wa Millenium Challenge  Account (MCA-T) 
Mradi wa Kukarabati Miundombinu ya Usambazaji wa Umeme Kigoma na Kituo cha Kufua Umeme Malagarasi

 Mheshimiwa Spika, kazi ya ukarabati wa miundombinu ya kusambaza umeme inaendelea kutekelezwa na Kampuni ya Symbion Power LLC kupitia ufadhili wa MCA-T. Mradi huo unajumuisha ujenzi wa njia za umeme wa msongo wa kV 11 na upanuzi wa njia za umeme ili kuunganisha umeme kwa wateja mbalimbali. Kazi ya ujenzi wa mradi huu inatarajiwa kukamilika mwezi Disemba, 2012. TANESCO ilikamilisha upembuzi yakinifu wa mradi wa MW 42 katika Mto Malagarasi (Igamba III) mwezi Mei, 2012. Serikali inafanya majadiliano na Washirika wa Maendeleo na sekta binafsi kwa ajili ya kutekeleza mradi huu, hivyo kuongeza uwezo wa kufua umeme katika ukanda wa magharibi. 

Mradi wa Kujenga Njia za Kusambaza Umeme 

  Mheshimiwa Spika, mradi huu unahusu ujenzi wa njia za msongo wa kV 33 na kV 11 kwa ajili ya kusambaza umeme katika Mikoa ya Dodoma, Iringa, Mbeya, Morogoro, Mwanza na Tanga. Utekelezaji wa mradi unaendelea na umefikia kiwango cha asilimia 40, ambapo kilomita 349.09 kati ya kilomita 870.43 zimekamilika. Mradi mzima unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2013.
Mradi wa Kusanifu na Kujenga Vituo 24 vya Kupozea Umeme 
 Mheshimiwa Spika, mradi huu unahusu usanifu na ujenzi wa vituo 24 vya kupozea umeme kV 33/0.4 na kV 11/0.4 katika Mikoa ya Dodoma, Iringa, Mbeya, Morogoro, Mwanza na Tanga. Ujenzi wa vituo 22 kati ya 24 ulianza mwezi Aprili, 2012. Mradi umepangwa kukamilika mwezi Machi, 2013. 

Mradi wa Njia ya Pili ya Umeme kutoka Dar es Salaam kwenda Unguja

 Mheshimiwa Spika, mradi unahusu usanifu na uwekaji wa njia ya pili ya umeme kutoka Ubungo hadi Ras-Kilomoni na uwekaji wa nyaya za umeme chini ya bahari (submarine cable) kutoka Ras-Kilomoni hadi Mtoni – Unguja. Njia hii itakuwa na uwezo wa kusafirisha MW 100 kwa msongo wa kV 132. Kazi ya kuweka nyaya za umeme chini ya bahari imeanza mwezi huu wa Julai, 2012 na itakamilika mwezi Agosti, 2013. 
 Mheshimiwa Spika, miradi ya MCA-T katika sekta ndogo ya umeme iliyotajwa hapo juu inakadiriwa kugharimu Dola za Marekani milioni 201.25, sawa na Shilingi bilioni 322.
Upelekaji wa Umeme Makao Makuu ya Wilaya na Maeneo  ya Vijijini

  Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka 2011/12, Serikali kupitia TANESCO ilikamilisha ufungaji na uzinduzi wa jenereta za kufua umeme katika Wilaya za Kasulu, Kibondo, Ngorongoro na Songea. Gharama zilizotumika kukamilisha miradi hii ni Shilingi bilioni 33.61, ambazo ni fedha za ndani. Serikali pia imekamilisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kV 33 kutoka Sumbawanga mjini mpaka Namanyere - Nkasi. Kwa sasa mkandarasi, M/s Rousant International anakamilisha upanuzi na ufungaji wa vifaa katika kituo cha kupozea umeme cha Sumbawanga mjini kwa ajili ya njia ya umeme kwenda Nkasi. 

 Mheshimiwa Spika, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kuwezesha utekelezaji  wa Mradi Kabambe wa kusambaza umeme vijijini katika mikoa 16 ya Arusha, Dodoma, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro, Mara, Manyara, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Pwani, Rukwa, Shinyanga, Singida, Tabora na Tanga. Wateja wa awali wapatao 20,000 wataunganishiwa umeme mradi utakapokamilika mwezi Disemba, 2012. Gharama ya mradi huu ni Shilingi bilioni 100.75.
Miradi Midogo ya Nishati Vijijini

 Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia REA imeendelea kuhamasisha uendelezaji wa vyanzo vya nishati jadidifu katika maeneo ya vijijini yaliyo mbali na Gridi ya Taifa. Katika Mwaka 2011/12, mradi wa Mawengi wenye uwezo wa kuzalisha kW 300 kwa kutumia maporomoko madogo ya maji uliyopo Wilayani Ludewa ulizinduliwa na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Novemba, 2011. Mradi huu unamilikiwa na Ushirika wa LUMAMA na unahusisha vijiji vya Lupande, Madunda na Mawengi. Katika awamu ya kwanza ya mradi, zaidi ya kaya 300 ziliunganishiwa umeme. Katika mradi huu Serikali imechangia Dola za Marekani 571,500 sawa na Shilingi milioni 914.40 kwa ajili ya kuunganishia umeme wateja 1,143. 
  Mheshimiwa Spika, mwezi Juni, 2011 REA ilisajiliwa katika mpango wa Clean Development Mechanism-Programme of Activities (CDM-PoA). Mpango huo unahamasisha uendelezaji wa nishati jadidifu na matumizi bora ya nishati. Wakaguzi kutoka United Nations Framework Convention on Climate Change (UNFCCC) kwa kushirikiana na REA walikamilisha tathmini ya Mradi wa Mapembasi - Njombe (MW 10) mwezi Aprili, 2012. Utaratibu huu unamwezesha mwendelezaji kupata mapato ya awali kutokana na kiwango cha hewa ukaa alichopunguza katika mazingira na hivyo kupunguza gharama za uwekezaji katika miradi hiyo. 
 Mheshimiwa Spika, Wakala pia uliendelea kusimamia utekelezaji wa miradi 10 chini ya Lighting Rural Tanzania – 2010. Mradi huo unahamasisha matumizi ya nishati yenye mwanga bora vijijini ili kupunguza matumizi ya mafuta ya taa na mishumaa. Mikoa inayonufaika na mradi ni Iringa, Kagera, Manyara, Mara, Mbeya, Mwanza, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga na Singida. Gharama ya mradi huu ni takribani Dola za Marekani milioni 1.0, sawa na Shilingi bilioni 1.60 na unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2013. 
 Mheshimiwa Spika, Serikali ilikamilisha tathmini ya usambazaji umeme kwa gharama nafuu. Tathmini hiyo iliyokamilika mwezi Disemba, 2011 ilionesha kuwa gharama za uunganishaji umeme maeneo ya vijijini zinaweza kupungua kwa asilimia 30 kwa kurekebisha viwango vya vifaa kama vipozea umeme na nyaya za umeme; kuwa na mfumo wa ununuzi wa pamoja wa vifaa; matumizi ya ready boards; na kutumia mfumo wa single wire earth-return. Miradi ya mfano  itatekelezwa katika Wilaya ya Kilombero (kituo cha umeme Kihansi mpaka Gereza la Idete) na Wilaya ya Mbozi (Vwawa  mpaka Itaka). Wateja wa awali wapatao 15,000 wanatarajiwa kuunganishiwa umeme kwa utaratibu huu. Gharama ya mradi huu ni Shilingi bilioni 16.
Mikakati ya Serikali katika Kuboresha Huduma za Umeme Kupitia TANESCO
 Mheshimiwa Spika, Serikali katika kutekeleza jukumu lake la kusimamia taasisi zilizo chini yake imegundua kuwa TANESCO inakabiliwa na changamoto kubwa ya upotevu wa umeme wa kiufundi na usio wa kiufundi unaokadiriwa kufikia asilimia 21. Wizara imegundua kuwa sehemu kubwa ya upotevu wa umeme usiokuwa wa kiufundi (non technical losses) unasababishwa na wizi unaofanywa na wananchi kwa kushirikiana na baadhi ya wafanyakazi wa TANESCO wasio waaminifu na mafundi wa mitaani wajulikanao kama vishoka. Aidha, wateja wengi wenye nyumba za biashara, za kuishi na viwanda katika Jiji la Dar es Salaam na baadhi ya mikoa ya Tanzania wamekuwa wakitumia umeme kwa njia zisizo halali. Pia, baadhi ya wafanyakazi wa TANESCO wamekuwa wakishiriki katika vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali za Shirika. 
 Mheshimiwa Spika, hali hii imeleta taswira isiyokuwa nzuri kwa Shirika na kurudisha nyuma juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za umeme. Ili kuondoa tatizo hilo, katika Mwaka 2011/12 Serikali kupitia TANESCO imechukua hatua mbalimbali za kinidhamu zikiwemo kuwafukuza kazi watumishi 17 na kuwafikisha mahakamani wengine 7; na kung’oa miundombinu iliyojengwa na vishoka. 
 Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua hizo zilizochukuliwa, natoa rai kwa wananchi wanaopata huduma ya umeme kwa njia zisizo halali kujisalimisha katika ofisi za TANESCO haraka iwezekanavyo. Hatua kali zitachukuliwa kwa wale ambao hawatatii rai hii zikiwemo kusitishiwa huduma ya umeme, kulipia gharama ya umeme kwa kipindi chote alichokuwa anapata huduma hiyo kwa njia zisizo halali pamoja na kulipa faini.  

 Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asili
 Mheshimiwa Spika, shughuli za utafutaji mafuta na gesi asili katika Bahari ya Hindi na nchi kavu zimeendelea kufanyika kwa kasi kubwa. Kwa sasa kuna kampuni 18 za utafutaji mafuta na gesi asili katika nchi kavu, baharini na kwenye maziwa na kuna jumla ya mikataba ya kugawana mapato (Production Sharing Agreements - PSAs) 26. Kampuni kubwa za kimataifa zinazojihusisha na utafutaji wa mafuta na gesi asili katika kina kirefu cha maji baharini ni pamoja na BG Group na Ophir za Uingereza; ExxonMobil ya Marekani; Dominion ya Australia; Mubadala ya Umoja wa Falme za Kiarabu; Petrobras ya Brazil, Shell ya Uholanzi; na Statoil ya Norway. 
 Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2011/12 Serikali kupitia TPDC ilisaini mikataba mitano (5) ya uzalishaji na ugawanaji mapato ya mafuta na gesi asili (PSAs) na Kampuni za Heritage (Ziwa Rukwa na  Bonde la Kyela); Petrobras (Kitalu Na. 8 karibu na Mafia); na Swala Oil and Gas (T) Limited (Bonde la Kilosa na Pangani). Serikali inaendelea kuboresha usimamizi wa mikataba hiyo na kujenga uwezo wa kufanya ukaguzi. Lengo ni kuhakikisha kuwa kampuni zote zinazofanya utafiti na uzalishaji wa gesi asili na mafuta zinatekeleza kazi zake kwa mujibu wa makubaliano yaliyomo katika mikataba. 
 Mheshimiwa Spika, mwezi Machi, 2012 Kampuni za Statoil na ExxonMobil  ziligundua gesi asili kiasi cha futi za ujazo trilioni 6 katika kisima cha Zafarani -1 na mwezi Juni, 2012 kampuni hizo pia ziligundua gesi asili kiasi cha futi za ujazo trilioni 3 katika kisima cha Lavani -1. Aidha, mwezi Mei, 2012 Kampuni za BG Group na Ophir zilichoronga visima viwili na kufanikiwa kupata gesi asili kiasi cha futi za ujazo trilioni 3.4 katika kisima cha Jodari-1, na kiasi cha futi za ujazo trilioni 4.6 katika kisima cha Mzia-1. 
 Mheshimiwa Spika, pia katika mwezi huo wa Mei, 2012 Kampuni ya Ndovu Resources (T) Limited iligundua gesi asili kwenye Kitalu cha Ruvuma katika kisima cha Ntorya-1. Kampuni hiyo inaendelea na uchambuzi wa takwimu ili kuhakiki kiasi cha gesi asili kilichopo. Aidha, Kampuni ya PanAfrican Energy (T) ilichoronga kisima SS 11 katika kisiwa cha Songo Songo ili kuongeza kiasi cha gesi asili kinachovunwa. Kisima hicho kina uwezo wa kuzalisha futi za ujazo milioni 60 kwa siku.
 Mheshimiwa Spika, kwa sasa, uvunaji wa gesi asili unafanyika katika maeneo ya Songo Songo (Kilwa) na Mnazi Bay (Mtwara) kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya soko la ndani. Gesi asili iliyopo (reserve) Songo Songo ni futi za ujazo kati ya trilioni 1.0 hadi 2.5 na Mnazi Bay ni futi za ujazo kati ya trilioni 3.0 hadi 5.0. Uwezo wa mitambo ya Songo Songo kusafisha gesi asili ni futi za ujazo milioni 110 kwa siku na Mnazi Bay ni futi za ujazo milioni 2 kwa siku.  
 Mheshimiwa Spika, visima vya Mkuranga na Kiliwani Kaskazini vilivyogunduliwa kuwa na gesi asili Mwaka 2007, bado havijaendelezwa. Ili kukidhi mahitaji ya gesi asili nchini visima vya Kiliwani Kaskazini, Nyuni na Ndovu vitaunganishwa na mitambo ya kusafisha gesi asili kisiwani Songo Songo. 
 Mheshimiwa Spika, matokeo ya utafiti wa mafuta na gesi asili unaoendelea hapa nchini, yanaonesha kuwepo kwa kiasi cha gesi asili kinachokadiriwa kuwa zaidi ya wastani wa futi za ujazo trilioni 26.99, sawa na mapipa ya mafuta bilioni 4.86 ikilinganishwa na kiasi cha awali cha futi za ujazo trilioni 5.0  katika maeneo ya Songo Songo na Mnazi Bay. Aidha, tafiti zaidi zinaendelea na inatarajiwa kuwa gesi asili nyingi zaidi itagundulika. Kiasi halisi cha gesi asili kilichopo kitafahamika baada ya kuchoronga visima vya utafutaji (exploration wells) katika maeneo husika. Fedha zilizotumika hadi sasa katika utafutaji huo ni Dola za Marekani milioni 919.90, sawa na Shilingi trilioni 1.47.
 Mheshimiwa Spika, ili kudhihirisha manufaa ya gesi asili na mafuta kwa wananchi wa maeneo ambayo rasilimali hizo zinapatikana, mwezi Januari, 2012 Serikali ilianza utaratibu wa kuhakikisha kuwa kampuni za utafutaji mafuta na gesi asili zinalipa tozo ya asilimia 0.3 ya mgawo wa faida ya gesi asili kwenye halmashauri husika. Utaratibu huu umeanza kutekelezwa katika Halmashauri ya Kilwa na utaimarisha uhusiano kati ya wananchi na wawekezaji kwenye maeneo hayo, katika kulinda miundombinu. Serikali pia inahimiza kampuni hizo ziongeze wajibu wa ushiriki katika masuala ya kijamii - Corporate Social Responsibility. Aidha, Kampuni ya Mauren and Prom imeelekezwa kuilipa Halmashauri ya Mtwara asilimia 0.3 ya service levy

Majadiliano kati ya Serikali na Kampuni ya Pan African Energy Tanzania Limited (PAT)

 Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwezi Januari hadi Mei, 2012 majadiliano kati ya TPDC kwa niaba ya Serikali na PAT yalifanyika kuhusu utekelezaji wa mkataba wa uzalishaji na ugawanaji mapato (PSA) kati ya pande hizo mbili. Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni uingizwaji kimakosa wa Dola za Marekani milioni 28.1 kwenye mahesabu ya mkataba kati ya TPDC na PAT. Baada ya uchambuzi kufanyika, Serikali ilibaini kuwa baadhi ya gharama zilizoingizwa kwenye vitabu vya PAT hazikuwa zimebainishwa kwenye mkataba. Kati ya fedha hizo, Dola za Marekani milioni 20.1 zingekuwa mgawo wa Serikali. Kimsingi PAT imekubali kuwepo kwa kasoro hizo na kuzifanyia marekebisho. Kuhusu kurejesha Serikalini Dola za Marekani milioni 20.1, uongozi wa PAT umewasilisha taarifa hizo kwa Kampuni mama  ya ORCA iliyopo nchini Uingereza kwa ajili ya uamuzi wa mwisho. Serikali imeelekeza PAT kuwasilisha uamuzi wake mwezi Agosti, 2012.

Ujenzi wa Bomba la Kusambaza Gesi Asili Jiji la Dar es Salaam
 Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na ujenzi wa miundombinu ya kusambaza gesi asili kutoka Ubungo mpaka  Mikocheni. Bomba hili litakuwa na sehemu za kuchepusha gesi asili kuelekea taasisi na nyumba zilizopo karibu na barabara ya Sam Nujoma. Taasisi hizo ni pamoja na Chuo cha Maji cha Rwegarulira, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Ardhi. Mradi huo utakapokamilika, viwanda 6 katika eneo la Mikocheni na nyumba 57 vitaunganishwa kwa ajili ya kutumia gesi asili. Mradi huu unatekelezwa kwa fedha za Serikali na kwa kutumia mkandarasi wa ndani (Kampuni ya BQ Contractors) kwa gharama ya Shilingi bilioni 5 na utakamilika mwezi Agosti, 2012. 

Uagizaji wa Mafuta wa Pamoja (Bulk Procurement) 

 Mheshimiwa Spika, Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja ulianza rasmi mwezi Januari, 2012. Katika kipindi cha kuanzia Januari, 2012 hadi Juni, 2012 kiasi cha tani 1,808,958 za mafuta aina ya petroli ziliingizwa nchini. Aidha, mafuta yaliyoagizwa kwa ajili ya soko la ndani ni tani 1,191,780 na nchi jirani ni tani 617,178. Mafuta yanayoingia rasmi katika soko la ndani yameongezeka kutoka wastani wa tani 160,000 kwa mwezi Mwaka 2011 hadi kufikia tani 198,000 kwa mwezi kati ya Januari, 2012. Mfumo huo umepunguza idadi ya siku ambazo meli inalipiwa gharama za demmurage kutoka siku 15 hadi siku 3 na kuboresha upatikanaji wa takwimu za mafuta nchini. Hata hivyo, utekelezaji wa mfumo huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuingizwa kwa mafuta yenye kiasi kikubwa cha ethanol. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali iliziagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kudurusu viwango vya kiasi cha ethanol kwenye mafuta yanayoingizwa nchini na kufanya marekebisho katika Kanuni za Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja na makabrasha ya zabuni. 
 Mheshimiwa Spika, tangu kuanza utekelezaji wa Kanuni na Mwongozo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja mwezi Januari, 2012, kumekuwepo na malalamiko mbalimbali. Malalamiko hayo ni pamoja na usimamizi wa zabuni za uagizaji mafuta kwa pamoja; kutokuwepo kwa Menejimenti ya Petroleum Importation Co-ordinator Limited (PIC); na Bodi ya PIC kusimamia shughuli zote ikiwemo kushiriki na kufanya maamuzi ya ununuzi. Kwa kutambua hilo, hatua kadhaa zilichukuliwa ikiwa ni pamoja na mapitio ya Mwongozo yaliyofanyika mwezi Mei, 2012 kwa kushirikisha wadau ili kuuboresha; PIC iliunda Kamati ya Zabuni ili kusimamia shughuli za ununuzi badala ya Bodi; na PIC pia iliajiri Menejimenti na wataalamu mbalimbali ili kusimamia shughuli zote za mfumo huo. Hatua hizi zitaboresha Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta wa Pamoja na kuondoa mgongano wa kimaslahi.
Hifadhi ya Taifa ya Mafuta (National Strategic Petroleum   Reserve)
 Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mafuta ya Mwaka 2008 inaipa TPDC jukumu la kuanzisha na kusimamia Hifadhi ya Taifa ya Mafuta nchini. Ili kufanikisha uanzishwaji wa Hifadhi ya Taifa ya Akiba ya Mafuta, Serikali iliamua kubadili matumizi ya  ghala la kuhifadhia mafuta la TIPER kuwa ghala la forodha. Aidha, mwezi Mei, 2012 TPDC ilipokea mapendekezo ya kutoka Kampuni ya kitaifa ya Falme za Kiarabu ya Emirates National Oil Company (ENOC) ya kuingia mkataba wa kuanzisha Hifadhi ya Mafuta hapa nchini. Serikali imeunda kikosi kazi kwa ajili ya kupitia mapendekezo hayo. Kikosi kazi hicho kinaundwa na wajumbe kutoka Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Madini, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Consolidated Holdings Corporation (CHC), EWURA na TPDC. Kikosi kazi kitakamilisha kupitia mapendekezo ya Kampuni ya ENOC mwezi Agosti, 2012. Kiasi cha fedha kinachohitajika ni Shilingi bilioni 98.
Udhibiti wa Bei na Ubora wa Mafuta
 Mheshimiwa Spika, EWURA imeendelea kudhibiti bei na kusimamia ubora wa baadhi ya bidhaa za petroli, dizeli na mafuta ya taa yanayouzwa nchini. Ili kukabiliana na tatizo la uchakachuaji, EWURA iliendelea kufanya ukaguzi wa kushtukiza; kuweka vinasaba kwenye mafuta yanayouzwa nchini; kutumia maabara zinazohamishika na kudhibiti matumizi ya mafuta ya ndege katika uchakachuaji. Aidha, katika Mwaka 2011/12, kati ya sampuli 115 zilizochukuliwa kwenye vituo vya mafuta ili kuhakiki ubora, sampuli 96 sawa na asilimia 83.5 zilithibitika kuwa na ubora unaotakiwa. 

 Uendelezaji wa Nishati Jadidifu 

Uendelezaji wa Nishati ya Jua
 Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuendeleza vyanzo mbalimbali vya nishati jadidifu, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini imeendelea kutoa kipaumbele katika kusambaza umeme kwenye maeneo yanayotoa huduma za kijamii. Ili kutekeleza azma hiyo, tathmini ya gharama za ufungaji wa nishati ya umeme wa jua zimefanyika na kubainika kuwa kwa wastani gharama za ufungaji mifumo ya umeme wa jua ni Shilingi milioni 12.4 kwa zahanati; Shilingi milioni 33.5 kwa kituo cha afya; Shilingi milioni 3.9 kwa shule yenye madarasa nane; na Shilingi milioni 12.5 kwa bweni.
 Mheshimiwa Spika, mwezi Machi, 2012 Millenium Challenge Acount Tanzania - MCA-T ilisaini mkataba na Kampuni ya Camco International (T) Limited wa kutekeleza mradi wa umeme wa jua (solar energy) wenye uwezo wa  kW 235.6 katika vijiji 25 mkoani Kigoma. Utekelezaji wa mradi huo umeanza na utakamilika mwezi Agosti, 2013. Gharama ya mradi huu ni Dola za Marekani milioni 4.75, sawa na Shilingi bilioni 7.60.

Uendelezaji wa Nishati ya Upepo

  Mheshimiwa Spika, Wizara iliendelea kuhamasisha matumizi ya upepo kwa ajili ya kuzalisha umeme. Hadi sasa kampuni zilizojitokeza kuanzisha miradi ya kufua umeme kwa kutumia upepo ni Geo-wind Power (T) Limited (Kititimo - Singida) ambayo ni ya ubia kati ya NDC, TANESCO na Power Pool East Africa Limited wanaotarajiwa kuzalisha MW 50 kwa kuanzia, na hatimaye kufikia MW 300; Wind East Africa Limited (Kititimo - Singida), ambayo ni ya ubia kati ya Kampuni za Six Telecoms, Aldwych na IFC wanaotarajiwa kuzalisha MW 100 utakapokamilika; na Sino Tan Renewable Energy Limited (Makambako - Iringa), ambayo itazalisha MW 100. 
 Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2011/12 Kampuni ya Geo-wind Power (T) Limited ilikamilisha ulipaji fidia kwa wananchi watakaopisha uendelezaji wa mradi. Kampuni pia inaendelea na majadiliano na Benki ya Exim ya China ili kupata mkopo wa masharti nafuu kwa ajili ya kuendeleza mradi huo. Aidha, Kampuni ya Wind East Africa Limited inafanya mashauriano na wananchi kwenye maeneo ya mradi ili kupata ardhi.

Uendelezaji wa Joto Ardhi (Geothermal)

 Mheshimiwa Spika, baada ya utafiti wa kijiokemia na kijiofizikia katika eneo la Ziwa Ngozi (Wilaya ya Mbozi) kukamilika,Wizara itawezesha kuanza kwa uchorongaji wa visima viwili katika eneo hilo. Katika Mwaka 2012/13, Wizara imetenga Shilingi bilioni 1 ili kuanza kazi hiyo.

 Uendelezaji wa Biofuel Kimiminika

 Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2011/12, Wizara iliandaa Rasimu ya Sera Biofuel Kimiminika (Liquid Biofuel Policy) ili kuendeleza biofuel  nchini. Pia, Wizara iliandaa Hadidu za Rejea kwa ajili ya kumpata mshauri atakayeainisha maeneo maalumu (agro-ecological zoning) ya uendelezaji wa Biofuel Kimiminika. 
 Mheshimiwa Spika, ili kuendeleza vyanzo vingine vya nishati, Wizara ilibainisha maeneo 12 ya maporomoko madogo ya maji kwa ajili kuzalisha umeme katika Wilaya za Kilombero, Kilosa, Morogoro Vijijini na Mvomero mkoani Morogoro. Pia, Wizara iliwezesha ujenzi wa mitambo ya biogas 1,500 kwa ajili ya kupikia majumbani katika Kanda ya Kaskazini kupitia programu ya biogas inayofadhiliwa na Serikali ya Uholanzi. 

SEKTA YA MADINI 
  
Ukuaji na Mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa
 Mheshimiwa Spika, kiwango cha ukuaji wa shughuli za Sekta ya Madini nchini kwa Mwaka 2011 kilikuwa asilimia 2.2 ikilinganishwa na asilimia 2.7 Mwaka 2010. Aidha, mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa kwa Mwaka 2011 ulikuwa asilimia 3.3 kama ulivyokuwa Mwaka 2010. Kupungua kwa ukuaji  na kutoongezeka kwa mchango wa Sekta ya Madini kumetokana na sababu mbalimbali zikiwemo kusitishwa kwa uzalishaji wa almasi katika shimo kuu (main pit) la mgodi wa Mwadui kwa takriban mwaka mzima kutokana na ukarabati wa mitambo kwenye mgodi huo; na kupungua kwa uzalishaji wa dhahabu katika migodi ya Tulawaka na Golden Pride ambayo inakaribia kufungwa.
Uzalishaji na Mauzo ya Madini
 Mheshimiwa Spika, thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi iliongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 1,508.7 Mwaka 2010 hadi kufikia Dola za Marekani milioni 1,980.2 Mwaka 2011, sawa na ongezeko la asilimia 31.3. Ongezeko  hilo lilichangiwa na kupanda kwa bei ya dhahabu ambayo ilikuwa ya wastani wa Dola za Marekani 1,571.28 kwa wakia Mwaka 2011 kutoka wastani wa Dola za Marekani 1,224.53 kwa wakia Mwaka 2010, sawa na ongezeko la asilimia 28.3. Asilimia 95 ya mauzo ya madini yote nje ya nchi ilichangiwa na mauzo ya dhahabu, ambapo thamani ya mauzo yake iliongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 1,436.2 Mwaka 2010 hadi Dola za Marekani milioni 1,879.62 Mwaka 2011, sawa na ongezeko la asilimia 31. Asilimia kubwa ya dhahabu inayozalishwa na migodi mikubwa Tanzania inauzwa nchi za Afrika Kusini, China, Japan na Switzerland.
 Mheshimiwa Spika, kwa upande wa uzalishaji na mauzo ya madini katika migodi mikubwa nchini katika kipindi cha Julai, 2011 hadi Juni, 2012 jumla ya wakia milioni 1.3 za dhahabu, wakia 391,522 za fedha na ratili milioni 13.3 za shaba zilizalishwa na kusafirishwa nje ya nchi kutoka migodi mikubwa ya Bulyanhulu, Buzwagi, Geita, Golden Pride, North Mara na Tulawaka. Jumla ya thamani ya madini hayo ni Dola za Marekani bilioni 2.2. Vilevile, jumla ya karati 59,894 za almasi na karati 613,851 za Tanzanite zilizalishwa na migodi ya Mwadui na TanzaniteOne. Aidha, karati 73,737 za Tanzanite iliyokatwa na gramu milioni 4.9 za Tanzanite ghafi zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 10.03 ziliuzwa nje ya nchi na mgodi wa TanzaniteOne, wakati karati 44,254 za almasi zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 10.01 ziliuzwa nje ya nchi na mgodi wa Mwadui. Jumla ya mrabaha uliolipwa Serikalini na wamiliki wote wa migodi mikubwa nchini katika kipindi hicho ni Dola za Marekani milioni 62.03
 Mheshimiwa Spika, Kitengo cha TANSORT pia kilithamini almasi za kampuni 17 zinazozalisha na kufanya biashara ya almasi nchini. Jumla ya karati 52,600 za almasi zilizouzwa nje ya nchi zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 13.03 zilithaminishwa. Almasi inayozalishwa katika mgodi wa Mwadui inauzwa Antwerp nchini Ubelgiji na soko kuu la almasi inayozalishwa na migodi mingine ni Afrika Kusini, Dubai, India, Israel na Russia. 

Kuimarisha Usimamizi wa Sheria ya Madini, 2010
 Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2011/12 Serikali iliahidi kukamilisha majadiliano na wamiliki wa migodi mikubwa yenye mikataba (MDAs) ili walipe mrabaha kulingana na viwango vilivyopo katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Serikali imetekeleza ahadi hii ambapo kampuni zote zinazomiliki migodi mikubwa ya dhahabu nchini zimeanza kulipa kiwango kipya cha mrabaha cha asilimia 4 ya mapato kabla ya kutoa gharama (Gross Value) badala ya asilimia 3 ya Net Back Value kuanzia tarehe 01 Mei, 2012. Kampuni hizo ni African Barrick Gold inayomiliki migodi ya dhahabu ya Bulyanhulu, Buzwagi, North Mara na Tulawaka; Kampuni ya Resolute Tanzania inayomiliki mgodi wa dhahabu wa Golden Pride; na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited inayomiliki mgodi wa dhahabu wa Geita. Kutokana na migodi mikubwa kuanza kulipa kiwango kipya cha mrabaha, Serikali inatarajia kukusanya mapato ya ziada ya Shilingi bilioni 30 katika Mwaka 2012/13. 
 Mheshimiwa Spika, Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 inaelekeza kuundwa kwa Bodi ya Ushauri ya Madini kwa ajili ya kumshauri Waziri mwenye dhamana ya madini masuala mbalimbali kuhusu maendeleo ya sekta. Bodi hiyo inatakiwa kuhusisha wadau muhimu wa sekta wakiwemo, wawakilishi wa wachimbaji wadogo na wakubwa na pia wafanyabiashara wa madini. Napenda kulitaarifu Bunge lako kuwa, Bodi hiyo imeundwa na kuzinduliwa rasmi tarehe 05 Aprili, 2012. 
 Utoaji na Usimamizi wa Leseni za Madini
 Mheshimiwa Spika, shughuli za utoaji wa leseni za madini nchini zimeendelea kuimarishwa na kuboreshwa, ambapo leseni za uchimbaji mdogo na biashara ya madini zimeanza kutolewa na Maafisa Madini wa Kanda kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010. Hatua hiyo imesaidia kupunguza mlundikano wa maombi ya leseni za uchimbaji mdogo katika Ofisi ya Makao Makuu ya Wizara na unalenga kuongeza kasi ya utoaji leseni kwa ujumla. Aidha, Wizara imeendelea kuimarisha Mfumo wa Utoaji na Usimamizi wa Leseni za Madini (Mining Cadastral Information Management System – MCIMS) kwa kuongeza kasi ya mawasiliano ya mtandao wa kompyuta; kutoa mafunzo kwa watendaji; na kuboresha mfumo wa kuingiza takwimu. 
 Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka 2011/12, jumla ya maombi 13,562 ya utafutaji na uchimbaji madini yalipokelewa na kuingizwa kwenye Mfumo wa Utoaji na Usimamizi wa Leseni za Madini, ikilinganishwa na maombi 5,921 katika Mwaka 2010/11, sawa na ongezeko la asilimia 129. Kati ya maombi yaliyopokelewa maombi 11,245 yalikuwa ni ya leseni ndogo za uchimbaji madini; maombi 65 ni ya uchimbaji wa kati; na maombi 2,252 ni kwa ajili ya leseni za utafutaji mkubwa wa madini. Aidha, jumla ya leseni 11,113 zilitolewa, kati ya hizo leseni 9,997 zilikuwa ni za uchimbaji mdogo, leseni 19 za uchimbaji wa kati na leseni 1,097 kwa ajili ya utafutaji mkubwa wa madini. Maombi ya leseni 334 yalikataliwa.
 Mheshimiwa Spika, sambamba na utoaji wa leseni, Wizara imechukua hatua za kutoa taarifa ya makosa (default notice) kwa wamiliki wa leseni za utafutaji madini ambao hawatimizi masharti ya leseni. Utekelezaji wa hatua hiyo ulianza mwezi Machi, 2012 kwa kutoa taarifa kupitia kwenye matangazo magazetini, ambapo jumla ya leseni za utafutaji 888 zilihusika. Kwa mujibu wa matangazo hayo, wamiliki wa leseni walitakiwa kurekebisha makosa yao ndani ya siku 30 kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa. Katika kipindi hicho, wamiliki wa leseni 246 walirekebisha makosa yao na wamiliki wa leseni 642 walipewa taarifa ya makosa ya siku 60 kwa mujibu wa Sheria. Wamiliki wa leseni zilizopewa taarifa za makosa na walioshindwa kurekebisha makosa yaliyobainishwa watafutiwa leseni zao na watatakiwa kulipa madeni husika. Maeneo ambayo leseni zitafutwa, yatagawiwa kwa waombaji wapya ili kuyaendeleza ama kutengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo ili kuongeza wigo wa kutoa ajira kwa vijana. Aidha, leseni zote za madini ambazo zimekuwa hazifanyiwi kazi kwa muda mrefu, zitafutwa ifikapo mwishoni mwa mwezi Disemba, 2012
 Mheshimiwa Spika, katika siku za karibuni, kumejitokeza biashara haramu ya madini inayofanywa na watu wasiokuwa waaminifu kwa kutumia nyaraka zisizo halali ikiwemo leseni za biashara ya madini. Kufuatia hali hiyo, Serikali ilitoa matangazo kwa umma kuhusu biashara hiyo na kushauri wanunuzi wa madini kushirikisha Ofisi za Madini zilizo karibu nao wakati wanafanya biashara hizo. Aidha, kutokana na matukio hayo, kuanzia tarehe 01 Julai, 2012 Wizara yangu imeanza kutoa leseni za biashara ya madini zisizoweza kughushiwa kirahisi. Napenda kuutaarifu umma kupitia Bunge lako Tukufu kuwa, mmiliki wa leseni au kampuni, ambayo itajihusisha na biashara haramu ya madini kwa njia yoyote, leseni yake itafutwa mara moja na wahusika watachukuliwa hatua za kisheria. 

Kuendeleza Uchimbaji Mdogo wa Madini
Kutenga Maeneo 

 Mheshimiwa Spika, uchimbaji mdogo ni mojawapo ya vyanzo muhimu vya ajira nchini, hususan, maeneo ya vijijini. Katika Mwaka 2011/12 Serikali ilitenga na kutoa leseni katika maeneo ya Itandula Wilayani Tarime lenye ukubwa wa hekta 37 na Mbesa Wilayani Tunduru lenye hekta 15,605 kwa ajili ya uchimbaji mdogo. Eneo la Itandula limegawiwa kwa vikundi vya wachimbaji wadogo vilivyoundwa. Vilevile, Serikali iliendelea kubainisha maeneo mengine yanayofaa kwa ajili ya uchimbaji mdogo yakiwemo Mogabiri, Nyakunguru na Goronga-Gibaso yenye jumla ya hekta 287.70 yaliyopo Wilayani Tarime. 
Kutoa Mikopo na Mitaji 

 Mheshimiwa Spika, Ibara ya 56(d) ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2010, pamoja na mambo mengine inahimiza kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata mikopo na mitaji kwa kuanzisha mifuko maalumu. Kwa kuzingatia maelekezo hayo, katika Mwaka 2011/12 Serikali ilitenga Shilingi bilioni 1.19 kwa ajili ya Mfuko wa Kuendeleza Wachimbaji Wadogo wa Madini. Fedha hizo zimetumika kwa ajili ya ukopeshaji na ukodishaji wa vifaa kwa wachimbaji wadogo katika maeneo ya Rwamugaza Wilayani Geita kupitia STAMICO; Londoni Wilayani Manyoni kupitia Kampuni ya Tan Discovery Mineral Consultancy; na Pongwe Msungura Wilayani Bagamoyo kupitia Kampuni ya Kilimo General Supplies Ltd. Kituo cha kuwaendeleza wachimbaji wadogo kitakachoendeshwa na STAMICO eneo la Rwamugaza mkoani Geita kitanufaisha wachimbaji wadogo wapatao 1,300 wanaofanya kazi katika maeneo ya Rwamugaza, Nyarugusu na Nyakagwe.
 Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kituo cha kuendeleza wachimbaji wadogo kilichopo eneo la Londoni mkoani Singida kwa kushirikiana na GST, kimeratibu magnetic survey kwa viwanja 22 vya wachimbaji wadogo katika maeneo ya Londoni na Sambaru. Hii ni hatua ya awali na muhimu ya kuwasaidia wachimbaji wadogo ili kubaini mashapo yenye dhahabu katika maeneo ya leseni zao. Hali hii inasaidia kufanya uchimbaji wao kuwa wa uhakika katika uzalishaji na kuwezesha kumudu gharama za ukodishaji wa zana. Lengo ni kuwanufaisha zaidi ya wachimbaji wadogo 13,400 katika maeneo ya Londoni na Sambaru. 
 Mheshimiwa Spika, Kampuni za Gemstyle na CE Holdings nazo zilipata mkopo kupitia Mfuko wa Kuendeleza Wachimbaji Wadogo kwa ajili ya kuendeleza mradi wa usanifu na uongezaji thamani madini. Vituo hivyo vinaendeshwa na vikundi vya wanawake. Kupitia mkopo huo, Kampuni ya Gemstyle imeongeza idadi ya mashine za kuongeza thamani kutoka tatu hadi sita na kutoa mafunzo kwa wachimbaji 30 katika shughuli za uongezaji thamani madini.  

Mafunzo kwa Wachimbaji Wadogo

 Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2011/12, Wizara yangu ilitoa mafunzo kuhusu Sera ya Madini ya Mwaka 2009, Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Kanuni zake, taratibu za umiliki wa leseni mbalimbali za madini na elimu ya ujasiriamali kwa wachimbaji wadogo wapatao 380 katika mikoa ya Kigoma, Lindi, Manyara, Morogoro, Singida na Tabora. 
 Mheshimiwa Spika, tarehe 23 Juni, 2012 nilikutana na wawakilishi wa wachimbaji wadogo kutoka nchi nzima kwa lengo la kujadiliana namna ya kuendeleza uchimbaji mdogo nchini. Katika mkutano huo changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wadogo zikiwemo ukosefu wa vifaa vya kisasa na maeneo ya kutosha kwa uchimbaji mdogo zilijadiliwa na kuwekewa mkakati wa kuzitatua. Wachimbaji wadogo waliagizwa kuimarisha vyama vyao vya uchimbaji kuanzia ngazi ya wilaya, mikoa hadi Taifa. Aidha, Wizara iliridhia kukutana na wachimbaji wadogo mwezi Disemba kila mwaka kwa ajili ya kutathmini maendeleo na changamoto za wachimbaji wadogo. Mpango Kazi wa kuboresha uchimbaji mdogo nchini unaotayarishwa na Serikali kupitia STAMICO utajadiliwa na kikao cha wachimbaji wadogo cha mwezi Disemba, 2012. 

Uimarishaji wa Masoko ya Madini ya Vito
 Mheshimiwa Spika, Sera ya Madini ya Mwaka 2009 inasisitiza uboreshaji wa mfumo wa masoko ya madini. Ili kufikia azma hiyo, Wizara yangu kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyabiashara wa Madini – TAMIDA iliandaa Maonesho ya Kwanza ya Kimataifa ya Vito na Usonara, mjini Arusha yaliyofanyika kuanzia tarehe 26 - 29 Aprili, 2012. 
 Mheshimiwa Spika, maonesho hayo yalihudhuriwa na jumla ya washiriki 777, wakiwemo wanunuzi 300 waliowakilisha kampuni 200 kutoka nchi 25; waoneshaji (exhibitors) 125; na washiriki binafsi wapatao 75. Kampuni za kitanzania zilizoshiriki katika uoneshaji (exhibition) katika maonesho hayo zilikuwa 39 kati ya 45. Wafanyabiashara wa ndani walipata fursa ya kutangaza madini yanayopatikana nchini na pia kukutana na wafanyabiashara wa kimataifa. Katika kipindi cha siku tatu za maonesho hayo, madini yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 3.88, sawa na takriban Shilingi bilioni 6.21 yaliuzwa na mrabaha wa Shilingi milioni 271.57 ulilipwa Serikalini.

Kuimarisha Afya, Usalama na Utunzaji wa Mazingira Migodini
 Mheshimiwa Spika, ili kuweza kuhakikisha kuwa shughuli za uchimbaji madini zinaendeshwa kwa kuzingatia Kanuni za usalama, afya na utunzaji wa mazingira, kwa kipindi cha Mwaka 2011/12, Wizara ilifanya ukaguzi wa kina katika migodi mikubwa nane ya  Bulyanhulu, North Mara, Geita, Williamson Diamond, Golden Pride, Buzwagi, Tulawaka na TanzaniteOne. Aidha, ukaguzi wa kina wa shughuli za utunzaji wa mazingira katika maeneo ya migodi ulifanyika kwenye migodi 34 ya wachimbaji wadogo na migodi 19 ya wachimbaji wa kati. 
 Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha utunzaji wa mazingira, wamiliki wa migodi mikubwa yote wanatakiwa kuwasilisha mipango ya ufungaji migodi (Mine Closure Plans) kwa mujibu wa Kanuni za usalama, afya na utunzaji wa mazingira, ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, inayowataka vilevile kuweka dhamana ya fedha za kukarabati mazingira (rehabilitation bond). Hadi sasa wamiliki wa migodi nane wamewasilisha mipango yao ya ufungaji migodi ambayo inawezesha kufahamu gharama zinazotakiwa kwa ajili ya kuweka dhamana ya ukarabati wa mazingira. Migodi hiyo ni Bulyanhulu, Buzwagi, Geita, Golden Pride, Mwadui, North Mara, TanzaniteOne na Tulawaka. Kamati ya Kisekta ya Kitaifa imepitia mipango hiyo na kuidhinisha mpango wa ufungaji wa mgodi wa Golden Pride. Migodi iliyobaki imeelekezwa kurekebisha mipango yake ya ufungaji migodi na kuwasilisha tena kwa Kamati hiyo kwa majadiliano. 
Uendelezaji wa Madini ya Urani Nchini 
 Mheshimiwa Spika, madini ya urani yanapatikana maeneo mbalimbali nchini yakiwemo Mto Mkuju (Wilaya za Liwale, Namtumbo na Tunduru); Bonde la Bahi (Wilaya ya Bahi) na Manyoni (Mkoa wa Singida); Gallapo na Minjingu katika Bonde la Ufa. Hata hivyo, ni maeneo ya Wilaya za Namtumbo na Manyoni tu ambayo kwa sasa yamethibitishwa kuwa na kiasi cha kutosha kuweza kuchimbwa kibiashara. Mradi wa urani uliopo Wilayani Namtumbo utaendelezwa na Kampuni ya Mantra Tanzania Limited na kiasi cha mashapo tani milioni 101.4 za urani yamethibitishwa. Gharama za awali za uwekezaji katika mradi huo zinakadiriwa kuwa Dola za Marekani milioni 450, sawa na Shilingi bilioni 720.
 Mheshimiwa Spika, sehemu ya eneo la mradi wa Namtumbo ipo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Selous Game Reserve, ambayo ni miongoni mwa maeneo ya urithi wa Dunia (WHC). Kutokana na sababu hiyo, Serikali iliwasilisha UNESCO maombi ya kurekebisha mipaka ya eneo la Urithi wa Dunia ili kuongeza eneo la mradi.  Katika kikao cha Kamati ya UNESCO ya Urithi wa Dunia kilichofanyika Saint Petersburg (Urusi) tarehe 02 Julai, 2012, ombi la Tanzania liliridhiwa.
 Mheshimiwa Spika, Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na Kanuni za Madini ya Mionzi Ayonisha za Mwaka 2010 - the Mining (Radioactive Minerals) Regulations, 2010 chini ya Sheria ya Madini, 2010 zinatumika katika kusimamia shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini ya urani nchini. Sheria na Kanuni zote zilizotungwa na zitakazoendelea kutungwa zinazohusiana na usimamizi wa madini ya urani pamoja na mambo mengine zinalenga kuzingatia  miongozo/taratibu za Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) za usimamizi wa madini hayo zinazohakikisha kuwa uchimbaji hauleti  athari kwa binadamu na mazingira.
Usimamizi wa Shughuli za Baruti Nchini
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2011/12 Wizara iliendelea kusimamia shughuli za uingizaji, usafirishaji, uhifadhi na ukusanyaji wa takwimu za baruti na matumizi yake katika Sekta ya Madini. Usimamizi huu umewezesha Wizara kupata taarifa sahihi za kiasi cha baruti kilichoingizwa na kutumika hapa nchini. Katika kipindi hicho tani 26,865 za baruti ziliingizwa nchini na kutumika katika shughuli za migodi; vyeti vya kulipua baruti 163 na leseni 18 za maghala ya kuhifadhi baruti vilitolewa. Aidha, Wizara iliendesha mafunzo ya matumizi sahihi na salama ya baruti katika mikoa ya Lindi na Kigoma kwa wachimbaji wadogo. 

Utekelezaji wa Shughuli za Tanzania Extractive  Industries Transparency Initiative -  TEITI 
Mheshimiwa Spika, Asasi ya Kimataifa ya Extractive Industries Transparency Initiative (EITI) huzitaka nchi zilizo katika hatua za awali za kujiunga kufanya tathmini kuonesha iwapo utekelezaji wa vigezo vya uwazi vimefikiwa. Katika kutimiza hitaji hili, Kamati Tekelezi ya TEITI iliajiri mhakiki (validator) mwezi Januari, 2011. Taarifa ya mhakiki iliwasilishwa kwenye Bodi ya EITI tarehe 15 Mei, 2011 kwa ajili ya kutolewa uamuzi. Bodi ya EITI ilionesha kuridhishwa na taarifa hiyo. Hata hivyo, vigezo vitano kati ya 18 havikukamilika kuiwezesha Tanzania kuwa mwanachama kamili. 
Mheshimiwa Spika, vigezo hivyo vitano ni kuwepo na fomu maalumu inayoonesha malipo yote ya mapato yanayofanyika; uwepo wa sheria inayoelekeza kampuni za madini, mafuta na gesi kutoa taarifa za malipo ya mapato yaliyofanyika Serikalini; uthibitisho wa takwimu za mapato zilizotolewa na Taasisi za Serikali kuwa zimekaguliwa kwa viwango vya kimataifa; uthibitisho kwamba malipo yote ya kampuni za madini, mafuta na gesi asili yamewasilishwa kwa reconciler; na uthibitisho kwamba malipo yote yaliyopokelewa na Serikali yamewasilishwa kwa reconciler. Bodi kwa kutambua jitihada iliyofanyika iliiongezea nchi yetu muda wa awali wa uanachama kwa miezi mingine 18 hadi tarehe 15 Februari, 2013. Katika kipindi hicho Tanzania itatakiwa iwe imekamilisha vigezo vyote vya kuiwezesha kupata uanachama kamili. 
Mheshimiwa Spika, mwezi Machi, 2012 Kamati ilikamilisha taarifa ya uchambuzi na uandaaji wa mapendekezo ya sheria ya usimamizi wa shughuli za TEITI. Taarifa hiyo kabla ya kukamilishwa, ilijadiliwa na wadau mwezi Septemba, 2011 na Machi, 2012. Kamati Tekelezi inakamilisha maandalizi ya kutoa elimu kuhusu shughuli za TEITI ili kuwafikia wananchi wengi zaidi nchini, hasa katika wilaya zilizo na shughuli za uchimbaji wa madini na gesi asili ili kupata maoni yatakayozingatiwa wakati wa uandaaji wa sheria ya TEITI.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya pili ya TEITI ya ulinganisho wa malipo na mapato yanayotokana na shughuli za uchimbaji madini na gesi asili kwa hesabu za Mwaka 2009/10 ilikamilika na kutolewa kwa umma tarehe 31 Mei, 2012. Matokeo yanaonesha kuwa malipo yaliyopokelewa Serikalini ni Shilingi bilioni 419 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 424 zilizolipwa na kampuni za utafutaji na uchimbaji madini, mafuta na gesi asili. Tofauti hiyo ya Shilingi bilioni 5 ni ndogo ikilinganishwa na tofauti ya Shilingi bilioni 46.5 iliyoainishwa katika taarifa ya kwanza ya TEITI. Hali hii inaonesha maboresho makubwa katika usahihi wa takwimu za malipo kati ya Serikali na kampuni husika. 
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mpango wa EITI umekuwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ucheleweshaji wa upatikanaji wa takwimu za malipo kutoka kwa baadhi ya wadau wanaotakiwa kuwasilisha taarifa hizo. Hali hii huathiri utoaji wa taarifa za ulinganisho wa malipo na mapato kwa wakati. Natoa wito kwa wadau hao kuwasilisha takwimu husika zinapohitajika kwa wakati. 

Kutoa Elimu kwa Umma kuhusu Manufaa ya Sekta ya Madini 
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa Sekta ya Madini imekuwa ikileta manufaa mbalimbali kwa Taifa, wananchi wengi bado wameendelea kuwa na mtazamo hasi juu ya sekta hiyo. Mtazamo huo unatokana na wananchi kutofahamu kwa kina manufaa yanayotokana na shughuli za uchimbaji madini nchini, ambapo wengi hufikiri faida inayopatikana ni mrabaha pekee. Ukweli ni kwamba yapo manufaa mengi zaidi ya malipo ya mrabaha. 
Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha Mwaka 2005 hadi 2011 manufaa mbalimbali yamepatikana kutokana na uwekezaji wa migodi mikubwa ya madini, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mapato ya Serikali kutokana na kodi mbalimbali kutoka Shilingi bilioni 37.16 hadi kufikia Shilingi bilioni 208.68; kuongezeka kwa ajira ya Watanzania kutoka 3,360 hadi kufikia 7,753; kuongezeka kwa ununuzi wa bidhaa na huduma za ndani unaofanywa na migodi hiyo kutoka Dola za Marekani milioni 237.97 hadi kufikia Dola za Marekani milioni 379.57; na kuongezeka kwa mrabaha unaolipwa Serikalini kutoka Dola za Marekani milioni 15.8 hadi Dola za Marekani milioni 57.5
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa takwimu zilizopo, wastani wa gharama za uzalishaji kwa wakia moja ya dhahabu ni Dola za Marekani 520. Kwa sasa mgawanyo wa mapato ya migodi mikubwa ni pamoja na mrahaba na kodi mbalimbali asilimia 8 ya mapato; gharama za uzalishaji ni asilimia 57 ya mapato; marejesho ya mitaji/mikopo na riba ni asilimia 19.5 ya mapato; faida na gawio kwa wanahisa ni asilimia 15 ya mapato; na gharama za miradi ya huduma za jamii ni asilimia 0.5 ya mapato.
Mheshimiwa Spika, takwimu hizo zinatoa taswira nzima ya  mapato yatokanayo na shughuli za migodi mikubwa ya dhahabu nchini. Napenda kusisitiza kuwa mapato ya Serikali yanatarajiwa kuendelea kuongezeka kadri migodi inavyokamilisha kurejesha mitaji na kuanza kulipa kodi ya mapato. Serikali itaendelea kuimarisha ukaguzi na uhakiki wa hesabu za fedha za migodi ili kuhakikisha kuwa migodi hiyo inalipa kodi na mrabaha stahiki. 

Huduma za Jamii Zitolewazo na Migodi

Mheshimiwa Spika, duniani kote migodi mikubwa inajizatiti katika utoaji wa huduma za jamii kwa hiari kwenye jamii inayozunguka mgodi, na maeneo mengine kwenye nchi husika. Migodi mikubwa iliyopo nchini imekuwa ikitoa huduma hizo katika nyanja za afya, elimu, maji, utunzaji wa miundombinu, utunzaji wa mazingira na uwezeshaji kiuchumi. Katika kipindi cha kuanzia Mwaka 1998 hadi 2011, migodi mikubwa nchini imetumia takriban Dola za Marekani milioni 38.6 kwa ajili ya huduma za jamii, sawa na asilimia 0.5 ya mapato yote ya migodi. Uzoefu wa kimataifa unaonesha kuwa, migodi mikubwa katika mataifa mbalimbali imekuwa ikitumia kati ya asilimia 0.3 hadi 2 ya mapato yake kwenye huduma za jamii. 
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na migodi katika eneo hilo. Serikali imeendelea kuhimiza migodi kuongeza mchango wake zaidi katika eneo hilo. Aidha, Serikali inaandaa mwongozo wa Kitaifa kuhusu huduma za jamii zitolewazo na migodi ili kutoa msukumo zaidi kwa migodi kutimiza wajibu wao, na kuhakikisha kuwa, miradi ya huduma za jamii inayotekelezwa na migodi inakuwa shirikishi na inayozingatia vipaumbele vya jamii husika. Mwongozo huo utakamilika katika Mwaka 2012/13.
 Ujenzi na Uboreshaji wa Ofisi za Madini
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2011/12, Wizara iliendelea kukarabati na kujenga ofisi za madini ili kuboresha mazingira ya utendaji kazi. Katika kipindi hicho ujenzi wa Ofisi ya Madini ya Kanda ya Kati (Singida) ulikamilika na ukarabati wa Ofisi ya Madini Kanda ya Kati - Magharibi (Shinyanga) ulianza. 

WAKALA WA UKAGUZI MADINI TANZANIA - TMAA
 Mheshimiwa Spika, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) uliendelea kutekeleza majukumu yake na kuwezesha kupatikana kwa mafanikio mbalimbali, ambapo katika kipindi cha Julai, 2011 hadi Juni, 2012 Mgodi wa Golden Pride uliopo Nzega unaomilikiwa na Kampuni ya Resolute umelipa kiasi cha Shilingi bilioni 37.2 kama kodi ya mapato (corporate tax). Hivyo, jumla ya kodi ya mapato iliyolipwa na mgodi huo tangu uanzishwe hadi sasa ni Shilingi bilioni 71.1. Katika kipindi hicho, Mgodi wa Dhahabu wa Geita unaomilikiwa na Kampuni ya AngloGold Ashanti umelipa jumla ya Shilingi bilioni 188.1 kama kodi ya mapato. Hivyo, jumla ya kodi ya mapato iliyolipwa na mgodi huo tangu uanzishwe ni Shilingi bilioni 191.3. Kiasi hicho cha kodi ya mapato kisingefikiwa endapo kazi ya ukaguzi wa gharama za uwekezaji na uendeshaji isingefanywa na TMAA kwa kushirikiana na TRA.
 SHIRIKA LA MADINI LA TAIFA – STAMICO
Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea kuiwezesha STAMICO kutekeleza majukumu yake. Mwezi Oktoba, 2011 Shirika lilisaini makubaliano na Kampuni ya Tanzanian American International Development Corporation (2000) – TANZAM 2000 Limited kwa ajili ya kufufua upya Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef mkoani Geita. STAMICO inamiliki hisa asilimia 45 na ina wajumbe katika Bodi ya Wakurugenzi na katika Kamati ya Kusimamia utekelezaji wa mradi. Mbali ya kodi na mrabaha, Serikali kupitia STAMICO itanufaika kwa kupata gawiwo la faida kutokana na asilimia 45 za hisa katika mgodi huo. 
Mheshimiwa Spika, hatua ya kwanza iliyochukuliwa na kampuni ya ubia imekuwa kuendeleza upembuzi yakinifu unaojumuisha uchorongaji miamba kwa lengo la kuthibitisha mashapo zaidi. Hadi mwishoni mwa mwezi Juni, 2012 mashapo yaliyopatikana yalikuwa wakia milioni 2.72 za dhahabu. Kiasi hiki cha dhahabu kina thamani ya Dola za Marekani bilioni 4.35, sawa na Shilingi bilioni 6,963.20 kwa wastani wa bei ya dhahabu ya Dola za Marekani 1,600 kwa wakia. Aidha, katika kipindi hicho STAMICO iliingia ubia wa hisa asilimia 50 kwa 50 na Obtala Resources kwa ajili ya kufungua migodi ya dhahabu yenye ukubwa wa kati kwa ubia na Watanzania wenye leseni na kuendesha vituo vya kununulia dhahabu.
Mheshimiwa Spika, mwezi Oktoba, 2011 STAMICO ilikabidhiwa eneo la Mgodi wa Buhemba. Baada ya kukabidhiwa eneo hilo, STAMICO iliweka ulinzi shirikishi kwa kuwatumia wananchi wa Kata za Buhemba na Mirwa. Vigezo vya kumpata mbia viliandaliwa, ambapo STAMICO, kwa niaba ya Serikali, itabaki na hisa zisizopungua asilimia 40. Vilevile, STAMICO itapata gawio la asilimia 30 la dhahabu itakayozalishwa kutokana na marudio ya mabaki ya uchimbaji wa zamani. Jumla ya kampuni 42 zilijitokeza kuomba ubia na STAMICO na zote zilialikwa kwenye zabuni. Hata hivyo, ni kampuni 11 tu ndizo zilizowasilisha zabuni. Uchambuzi wa zabuni hizo unaendelea chini ya kamati ya wataalamu. 
 WAKALA WA JIOLOJIA TANZANIA – GST
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2011/12 Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) ulipima na kuchora ramani mpya 4 za jiolojia za QDS 194, 212 na 230 zilizoko Chunya na QDS 148 iliyoko Kilindi. Wakala pia ulipima na kuchora ramani mpya 2 za jiokemia za QDS 212 na 230. Aidha, ramani 53 za zamani za mfumo wa QDS zilibadilishwa kutoka kwenye mfumo wa karatasi na kuzifanya kuwa kwenye mfumo wa digital.
Mheshimiwa Spika, Wakala kwa kupitia ufadhili wa African   Array Program ulipata msaada na kufunga vituo viwili vipya vya kupimia matetemeko ya ardhi katika maeneo ya Geita na Mtwara ambavyo vyote vilifungwa pamoja na Differential Global Positioning Systems. Aidha, takwimu za matukio ya matetemeko ya ardhi ziliendelea kukusanywa katika vituo hivyo viwili vipya pamoja na vile vya zamani vilivyoko Dodoma, Kibaya, Kondoa, Babati, Mbeya, Singida na Manyoni. Wakala ulifanya utafiti wa kina wa upatikanaji wa nishati ya jotoardhi (geothermal energy) katika eneo la Ziwa Ngozi na kubainisha maeneo matatu yanayofaa kuchoronga mashimo ya kina kirefu ya kupimia kiasi cha joto katika eneo hilo. Pia, utafiti wa upatikanaji wa madini kwa kutumia Satelite Palsar Radar Images ulifanyika kwa ufadhili wa Japan Oil Gas and Metals Corporation (JOGMEC). Kutokana na matokeo ya utafiti huo, maeneo yatakayopewa kipaumbele kwa ufuatiliaji wa kina ni pamoja na Nachingwea, Kilosa, Mpwapwa na Simbanguru – Mazoka (Manyoni). 

 CHUO CHA MADINI DODOMA - MRI
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2011/12, Chuo cha Madini – Dodoma kiliendelea kutoa mafunzo katika ngazi ya Cheti na Stashahada kwa jumla ya wanafunzi 240 katika fani za Jiolojia na Utafutaji Madini (Geology and Mineral Exploration); Uhandisi Migodi (Mining Engineering) na Uhandisi Uchenjuaji Madini (Mineral Processing Engineering). Jumla ya wanafunzi 55 walihitimu katika fani za Geology and Mineral Exploration (20); Mining Engineering (21); na Mineral Processing Engineering (14). Aidha, Chuo kiliandaa mitaala ya ngazi za stashahada katika fani za Uhandisi na Usimamizi wa Mazingira Migodini; na Jiolojia ya Mafuta na Gesi na kuiwasilisha NACTE kwa ajili ya kupata uhalali na ithibati (accreditation).
Mheshimiwa Spika, mafunzo ya muda mfupi yameendelea kutolewa kwa wataalamu wanaofanya kazi katika migodi mbalimbali nchini, ikiwemo migodi ya dhahabu ya North Mara na Geita. Pia, Chuo kimeendelea kuainisha matatizo ya wachimbaji wadogo katika maeneo ya Nyarugusu, Lwenge na Rwamugaza. Lengo ni kuanza kutoa mafunzo ya umahiri katika Mwaka 2012/13 ili kuongeza uzalishaji. 
Mheshimiwa Spika, Chuo kinakabiliwa na changamoto mbalimbali, hususan madarasa na vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Uzoefu kutoka nchi mbalimbali duniani unaonesha kuwa ili kufanya kazi kwa ufanisi, mtaalamu mmoja anapaswa kufanya kazi na mafundi watano wa kumsaidia (uwiano wa 1:5). Kwa hapa nchini hali hiyo haipo kwa kuwa kuna vyuo vikuu viwili (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Dodoma) vinavyotoa wataalamu wa fani za madini katika ngazi ya shahada ambapo wastani wa wahitimu 180 hutolewa kila mwaka. Ili kufikia uwiano huo, Chuo cha Madini kitaendelea kuboresha miundombinu ili kuwa na uwezo wa kutoa wahitimu wasiopungua 900 kila mwaka. 
SOUTHERN AND EASTERN AFRICAN MINERAL CENTRE – SEAMIC 

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Utafiti na Uendelezaji wa Sekta ya Madini cha SEAMIC kilichopo Kunduchi, Jijini Dar es Salaam kimeendelea kutoa mafunzo na huduma za kitaalamu kwa Sekta za Madini za nchi wanachama na sekta binafsi zinazowekeza katika madini. Nchi wanachama wa SEAMIC ni Angola, Comoro, Ethiopia, Kenya, Msumbiji, Sudan, Tanzania na Uganda. Aidha, kikao cha Mawaziri wa Madini wa nchi wanachama kilifanyika Jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa mwezi Juni, 2012 katika utaratibu wa kila mwaka wa kukutana kutathmini utendaji wa kituo hicho. Katika mkutano huo, Tanzania iliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa kikao cha Mawaziri wa SEAMIC na kupewa jukumu la kusimamia shughuli za kituo kwa kipindi cha Mwaka 2012/13, wakati Sudan ilichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti na kupewa jukumu la kuandaa mkutano ujao wa Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya madini utakaofanyika mwezi Mei, 2013 Jijini Khartoum, Sudan. Kutokana na Kituo hiki wadau wa Sekta ya Madini wananufaika kwa kupeleka sampuli mbalimbali kwa ajili ya kufanyiwa utambuzi wa madini yaliyomo.

AJIRA NA MAENDELEO YA WATUMISHI

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2011/12 Wizara ilidurusu muundo wa utendaji kazi ili kuongeza ufanisi wa shughuli zake. Katika muundo huo, sehemu mbili zimeongezwa ambazo ni Sehemu ya Uongezaji Thamani Madini iliyopo chini ya Idara ya Madini; na Sehemu ya Matumizi ya Gesi iliyopo chini ya Idara ya Nishati.  
Mheshimiwa Spika, katika kuongeza tija na motisha kwa watumishi, katika Mwaka 2011/12 Wizara iliwapandisha vyeo watumishi 80, kuthibitisha kazini watumishi 63 na kuwabadilisha kazi watumishi watatu (3). Aidha, Wizara iliwapeleka mafunzoni jumla ya watumishi 112 katika fani mbalimbali. Kati ya hao, 33 walihudhuria mafunzo ya muda mrefu na 79 walihudhuria mafunzo ya muda mfupi.
Mheshimiwa Spika, kwa kuelewa na kuthamini mchango wa watumishi wanapokuwa na afya njema, Wizara imeendelea kutoa huduma ya lishe, chakula na madawa maalumu kwa watumishi wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (VVU) na wenye UKIMWI kama inavyoagizwa na Waraka wa Utumishi wa Umma Na. 2 wa Mwaka 2006. Wizara itaendelea kutoa huduma hizo ikiwa ni pamoja na huduma ya upimaji wa hiari wa VVU kwa watumishi. Aidha, elimu juu ya masuala ya UKIMWI itaendelea kutolewa kwa watumishi wa Wizara na wachimbaji wadogo katika maeneo mbalimbali.

MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2012/13
Mheshimiwa Spika, Mpango na Bajeti ya Wizara kwa Mwaka 2012/13 umezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011/12 – 2015/16; Malengo ya Taifa ya MKUKUTA II; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2010 - 2015; Mpango Mkakati wa Wizara ya Nishati na Madini 2011/12 – 2015/16; Maagizo ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa kwa Wizara ya Nishati na Madini kwa nyakati tofauti; Mwongozo wa Utayarishaji wa Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2012/13; na ushauri uliotolewa na Bunge pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa nyakati tofauti. 
Mheshimiwa Spika, Mpango na Bajeti ya Wizara kwa Mwaka 2012/13, unatoa mwelekeo wa kukabiliana na changamoto zilizopo katika Sekta za Nishati na Madini. Mpango huu unalenga kutekeleza miradi ya kitaifa ya kimkakati ambayo itakuwa na manufaa katika kipindi cha muda mfupi na wa kati. Hii ni katika kuhakikisha kuwa sekta za nishati na madini zinachangia ipasavyo katika maendeleo ya Taifa na hatimaye kuwezesha juhudi za Serikali katika kupunguza umaskini. Kufikiwa kwa lengo hilo kutarudisha imani ya Watanzania kuhusu utekelezaji wa mipango ya Serikali kwa vitendo chini ya dhana ya uwajibikaji na uwazi katika shughuli za umma.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka 2012/13, Wizara inalenga kuimarisha zaidi usimamizi wa Sekta za Nishati na Madini ikiwa ni pamoja na kuboresha makusanyo yatokanayo na sekta hizo ili kuwezesha utekelezaji wa mipango ya Serikali. 
 Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali

Mheshimiwa Spika, Wizara itaongeza juhudi za ukusanyaji wa mapato ya Serikali kutoka Shilingi 131,266,153,300 zilizokadiriwa kwa Mwaka 2011/12 hadi kufikia Shilingi 193,007,543,000 kwa Mwaka 2012/13, sawa na ongezeko la asilimia 47. Mapato hayo yatakusanywa kwa kutumia mikakati mbalimbali ikiwemo kuendelea kukusanya mauzo ya gesi asili; kuboresha mikataba ya uzalishaji na ugawanaji wa mapato ya mafuta na gesi asili; kuimarisha usimamizi wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Kanuni zake pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu Sheria hiyo; kuongeza kasi ya utoaji wa leseni kwa kuimarisha Mfumo wa Utoaji Leseni za Madini; kuendelea kutoa huduma za ugani kwa wachimbaji wadogo ili kuongeza tija katika uzalishaji madini; kuendelea kuimarisha Ofisi za Madini Kanda na Afisa Mkazi kwa kuzipatia rasilimali watu na fedha; na kuongezeka kwa mauzo ya madini yaliyoongezwa thamani. 
Mheshimiwa Spika, pamoja na mikakati hii, natumia fursa hii kuwakumbusha na kuwahimiza wamiliki wote wa leseni za madini nchini kuhakikisha kuwa wanalipa mrabaha, kodi na tozo mbalimbali kulingana na Sheria za nchi na kuyaendeleza maeneo ya utafutaji na uchimbaji.
 SEKTA YA NISHATI
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2012/13, kazi zilizopangwa kutekelezwa ni pamoja na kupanua na kuboresha miundombinu ya gesi asili na mafuta; kuongeza uwezo wa kufua umeme; ujenzi wa njia za kusafirisha na kusambaza umeme; kuongeza kasi ya kupeleka umeme makao makuu ya wilaya na vijijini; kuhamasisha matumizi ya nishati jadidifu katika ufuaji umeme; kuhamasisha matumizi bora ya nishati; kuendeleza shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asili, kudurusu na kuandaa sera, sheria, mipango na mikakati inayohusu Sekta ya Nishati. 
Kupanua na Kuboresha Miundombinu ya Mafuta na Gesi Asili 
Kujenga Bomba la Kusafirisha Gesi Asili Kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2012/13, Serikali itaanza ujenzi wa mitambo miwili ya kusafisha gesi asili katika maeneo ya Songo Songo Kisiwani na Mnazi Bay na ujenzi wa bomba la gesi asili lenye urefu wa kilometa 532 kutoka Mnazi Bay, Mtwara na Songo Songo Kisiwani (Kilwa) hadi Dar es Salaam kupitia Somanga Fungu. Utekelezaji wa mradi huu utakuwa katika awamu mbili. Awamu ya kwanza ni ujenzi wa bomba la gesi asili lenye kipenyo cha inchi 24 na urefu wa kilometa 25 kutoka Songo Songo Kisiwani hadi Somanga Fungu - Kilwa; na ujenzi wa bomba lenye kipenyo cha inchi 36 na urefu wa kilometa 197 kutoka Somanga Fungu - Kilwa hadi Dar es Salaam. Awamu ya pili, itahusisha ujenzi wa bomba lenye kipenyo cha inchi 36 na urefu wa kilometa 290 kutoka Mnazi Bay, Mtwara hadi Somanga Fungu. Katika Mwaka 2012/13, Serikali imetenga Shilingi bilioni 63 kama sehemu ya mchango kwa ajili ya ujenzi wa mitambo ya kusafisha gesi asili na bomba la kusafirisha gesi asili. Gharama ya mradi huu ni Dola za Marekani milioni 1,225.3, sawa na Shilingi trilioni 1.96.
Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa mradi wa bomba la gesi asili kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam mwishoni mwa Mwaka 2013, kutawezesha mitambo ya umeme kutumia gesi asili badala ya mafuta ambayo ni ghali, na hivyo kuokoa zaidi ya Dola za Marekani milioni 900 kwa mwaka. Vilevile, matumizi ya gesi asili yatapunguza utegemezi wa umeme unaofuliwa kutokana na maji na hivyo kuongeza uwezo wa upatikanaji umeme wa uhakika. Kwa upande mwingine, upatikanaji wa gesi asili ya kutosha katika Jiji la Dar es Salaam kutachochea matumizi zaidi kwenye viwanda, taasisi, magari na majumbani.
Mheshimiwa Spika, ili kuanza utekelezaji wa mradi wa bomba la gesi asili, Serikali imefanya tathmini ya mali kwenye maeneo ambayo bomba litapita. Fidia itaanza kulipwa kwa wananchi husika kuanzia mwezi Agosti, 2012.

   Usambazaji wa Gesi Asili Jijini Dar es Salaam 
Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka 2012/13, Wizara itaendelea na utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa miundombinu ya kusambaza gesi asili kwenye nyumba 30,000, hoteli na taasisi 10, magari 8,000 na vituo vitatu (3) vya kujazia gesi asili kwenye magari Jijini Dar es Salaam. Gharama za mradi zinakadiriwa kuwa Dola za Marekani milioni 35, sawa na takriban Shilingi bilioni 56. Kufuatia mafanikio yaliyopatikana kutokana na mradi wa majaribio katika nyumba 70, magari 45 na kituo kimoja cha kujazia gesi asili kwenye magari, wigo wa usambazaji wa gesi asili utaongezwa ili kuwafikia wateja wengi zaidi. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imetenga Shilingi bilioni 20 kwa kazi hiyo. 
Mheshimiwa Spika, ili kuhamasisha matumizi ya gesi asili kwenye taasisi, majumbani, viwandani na kwenye vyombo vya usafiri, Serikali imeamua kuondoa kodi ya ongezeko la thamani kwenye vifaa vitakavyotumika kwa ajili ya gesi iliyoshindiliwa (compressed natural gas) na vya kujengea mabomba ya kusafirisha gesi asili (piped natural gas) vikiwemo mita za kupimia gesi asili na majiko mahsusi yanayotumia gesi asili tu.  
 Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa nchi inafaidika na rasilimali zilizopo, umiliki wa miundombinu kama mitambo ya kusafisha na kusafirisha gesi asili umeangaliwa upya. Kwa kuzingatia hilo, Serikali kupitia TPDC itamiliki bomba jipya la gesi asili litakalojengwa kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam pamoja na mitambo ya kusafisha gesi katika visima vilivyopo Songo Songo na Mnazi Bay. Aidha, TPDC itakamilisha ufufuaji wa Kampuni ya GASCO ili iweze kusimamia majukumu ya usafishaji na usafirishaji wa gesi asili hiyo. 

  Kuongeza Uwezo wa Kufua Umeme

Mitambo ya Kinyerezi I - MW 150 na Kinyerezi II - MW 240

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya Mwaka 2012/13, Serikali itaanza kutekeleza mradi wa Kinyerezi I MW 150. Aidha, Serikali itakamilisha mikataba ya mikopo na benki za JBIC na ABSA ifikapo mwezi Septemba, 2012 kwa ajili ya ujenzi wa mtambo wa Kinyerezi II MW 240. Utekelezaji wa mradi utaanza baada ya kusainiwa kwa mikataba hiyo. Mitambo hii ina uwezo wa kutumia gesi asili au mafuta ya ndege (Jet–A1). Mitambo hiyo itakapokamilika itaongeza MW 390 katika Gridi ya Taifa na itamilikiwa na Serikali kupitia TANESCO. Katika Mwaka 2012/13 Serikali imetenga Shilingi bilioni 18 kama mchango wake katika kutekeleza miradi hiyo. Jumla ya gharama ya miradi hii miwili ni Dola za Marekani milioni 598, sawa na Shilingi bilioni 956.8

Mradi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira MW 200

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2012/13 Serikali kupitia STAMICO itatafuta mbia kwa lengo la kuendeleza mradi wa Kiwira kwa manufaa ya Taifa. Lengo la mradi huu ni kuanza uzalishaji wa umeme wa MW 200 katika Mwaka 2015/16, ambapo MW 50 zitaanza kufuliwa Mwaka 2014/15 na kujenga njia ya umeme ya kV 220 kutoka Kiwira hadi kituo cha kupozea umeme cha Uyole, Mbeya. Utekelezaji wa mradi huu utawezesha kuongezeka kwa umeme wa bei nafuu kwenye Gridi ya Taifa.  Mradi huu unakadiriwa kugharimu Dola za Marekani 400,   sawa na Shilingi bilioni 640. 

 Mradi wa Somanga Fungu MW 320 
 Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2012/13, Kampuni ya Kilwa Energy itaanza ulipaji wa fidia kwa wananchi watakaopisha ujenzi wa mradi na kuanza utekelezaji wa mradi wa Somanga Fungu wa MW 320. Mradi huo utazalisha MW 230 kwa kuanzia, ambapo MW 90 za ziada zitazalishwa baada ya miezi 20. Gharama za mradi huu ni Dola za Marekani milioni 365, sawa na Shilingi bilioni 584.
Mradi wa Murongo / Kikagati MW 16
Mheshimiwa Spika, mradi huu ni wa kujenga miundombinu ya kusambaza umeme katika mji mdogo wa Murongo mkoani Kagera. Lengo ni kuwezesha wakazi wa Murongo/Kikagati kuunganishiwa umeme wa MW 16 utakaozalishwa kutoka katika maporomoko ya maji ya Mto Kagera. Mradi utaendelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda, ambapo kila nchi itapata MW 8. Kazi zilizopangwa kufanyika chini ya mradi ni ujenzi wa njia za kusambaza umeme za msongo wa kV 33 na kV 0.4; ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 33 yenye urefu wa kilometa 194 na kusambaza umeme katika mji mdogo wa Murongo pamoja na vijiji 24. Katika Mwaka 2012/13 Serikali imetenga Shilingi bilioni 12 kwa ajili ya ujenzi wa njia na usafirishaji na usambazaji umeme kwa upande wa Tanzania.

Mradi wa Ufuaji na Usambazaji wa Umeme – Biharamulo, Mpanda na Ngara

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2012/13, utekelezaji wa mradi wa ORIO katika maeneo ya Biharamulo, Mpanda na Ngara utaanza. Mradi huo utahusisha ufungaji wa jenereta za kufua MW 2.5 kwa kila eneo pamoja na usambazaji wa umeme katika maeneo hayo. Mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Kifalme ya Uholanzi. Mradi huo utagharimu Euro milioni 34, sawa na Shilingi bilioni 67.49 na wateja wa awali 100,000 wataunganishwa.

Ukarabati wa Mitambo katika Vituo vya Kufua Umeme
Mheshimiwa Spika, mradi huu unahusu ukarabati  wa mitambo ya vituo vitano vya kufua umeme unaotokana na nguvu za maji. Mitambo hii ni Kidatu, Kihansi, Mtera, New Pangani Falls na Nyumba ya Mungu. Mradi utafadhiliwa kwa msaada wa Serikali ya Norway kwa asilimia 32, kwa Mwaka 2012/13 Serikali hiyo imetoa Shilingi bilioni 2.43. Katika kutekeleza mradi huu, TANESCO itachangia asilimia 68. Mradi huu unatarajiwa kukamilika Mwaka 2013/14. Aidha,  ukarabati wa mitambo ya kituo cha Hale utatekelezwa kwa ufadhili wa Serikali ya Sweden kwa kiasi cha Shilingi bilioni 4.5
Ujenzi wa Njia za Kusafirisha na Kusambaza Umeme
Uboreshaji wa Huduma za Umeme Jijini Dar es Salaam

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya umeme katika Jiji la Dar es Salaam. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na kukarabati vituo vya kupozea umeme katika maeneo ya Ilala, Temeke, Kinondoni Kaskazini na Kinondoni Kusini; kukamilisha ufungaji wa transfoma zenye uwezo mkubwa katika maeneo ya Mbezi Beach, Mbagala, Kigamboni, Gongolamboto, Kurasini na Ubungo; kubadilisha nyaya ndogo na zilizochakaa; kubadilisha nguzo zilizooza za njia za msongo mdogo na mkubwa za umeme; kujenga njia kubwa za umeme za msongo wa kV 33 ili kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika Jijini. Katika Mwaka 2012/13 jumla ya Shilingi bilioni 52 zimetengwa kutumika katika mradi huo. 

 Mheshimiwa Spika, Serikali ya Finland itatoa kiasi cha Euro  milioni 25 kwa ajili ya  ujenzi wa kituo cha kupozea umeme cha kV 132/33/MVA 2x45 city centre; ujenzi wa njia ya umeme chini ya ardhi kutoka kituo cha Ilala hadi kituo kipya cha city centre; ujenzi wa njia ya umeme chini ya ardhi kwa ajili ya kuunga kituo cha Kariakoo – Railway – Sokoine na kituo cha zamani cha city centre; kuanzisha kituo cha kuongozea mifumo ya usambazaji umeme katika msongo wa kV 33 na kV 11 (SCADA); kuanzisha mfumo wa kuangalia na kutoa taarifa za usambazaji umeme katika msongo mdogo wa umeme. Serikali ya Tanzania itachangia Euro milioni 1.5 kwa ajili ya kazi hizo. 

Mradi wa Iringa - Shinyanga kV 400 (backbone) 
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuwezesha na kusimamia utekelezaji wa mradi wa Iringa - Shinyanga kV 400, ambapo kazi zitakazofanyika ni pamoja na ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa njia ya msongo wa kV 400; ujenzi wa vituo vinne (4) vya kupozea umeme katika Mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga; na ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa njia za usambazaji umeme. Vyanzo vya fedha kwa ajili ya mradi huu ni kutoka Benki ya Dunia, JICA, AfDB, NORAD, Sida, Taasisi ya Korea Kusini (ECDF) na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB). Fedha zilizotengwa kwa ajili ya kutekeleza mradi huo kwa Mwaka 2012/13 ni Shilingi bilioni 12.5 na fedha za nje ni Shilingi bilioni 7.5.

Mradi wa Makambako - Songea kV 220           
Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa kufanyika katika Mwaka 2012/13 chini ya mradi huo ni uandaaji wa michoro ya mradi; shughuli za ugani (Aerial flight survey); uandaaji wa zabuni za kumpata mkandarasi; na ulipaji wa fidia kwa wananchi watakaopisha ujenzi wa mradi huo wa njia ya msongo wa kV 220. Katika Mwaka 2012/13, Serikali imetenga Shilingi bilioni 9.5 na fedha za nje ni Shilingi bilioni 7.5 kwa ajili ya utekelezaji wa kazi hizo. 

Mradi wa North - West Grid  kV 220 
Mheshimiwa Spika, lengo la mradi ni kujenga njia ya umeme ya msongo wa kV 220 kutoka Geita kwenda Nyakanazi – Kigoma – Mpanda – Sumbawanga hadi Mbeya. Lengo ni kuipatia mikoa hiyo umeme wa gridi. Gharama za mradi ni Dola za Marekani milioni 792.9, sawa na Shilingi bilioni 1,268.64, ambapo Benki ya Exim ya China itagharimia asilimia 85 na Serikali itachangia asilimia 15. Katika Mwaka 2012/13 Shilingi bilioni 5 zimetengwa kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi.

Kuendeleza Usambazaji Umeme katika Makao Makuu ya   Wilaya na Vijijini

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, 2010 – 2015, Ibara ya 63(c), Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) itaendelea na kazi ya kupeleka umeme katika Makao Makuu ya Wilaya za Nanyumbu, Mkalama, Kakonko, Uvinza, Mlele, Kalambo, Nyasa, Buhigwe, Momba, Itilima, Busega, Ikungi, Chemba na Kyerwa. Aidha, upelekaji umeme Makao Makuu ya Wilaya za Mbogwe na Bukombe zitaendelea kutekelezwa chini ya mradi wa Electricity V unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Makao Makuu ya Wilaya mpya ya Nyang’hwale utatekelezwa chini ya mradi wa Millenium Challenge Corporation (MCC) ya Serikali ya Marekani. 

Mheshimiwa Spika, upelekaji umeme katika wilaya hizo utahusisha ufungaji wa transfoma na usambazaji umeme kwenye njia zenye msongo wa kV 11 na 33, na ujenzi wa njia ya usambazaji zenye msongo wa kV 0.4. Kutekelezwa kwa kazi hizo kutawezesha kuunganisha wateja wa awali wapatao 80,000. Aidha, Wakala kwa kushirikiana na TANESCO utaendelea na kuwezesha utekelezaji wa mradi kabambe katika mikoa 16. Katika Mwaka 2012/13, mbali na vyanzo vingine vya fedha, Wakala umetengewa jumla ya Shilingi bilioni 150, zikiwemo Shilingi bilioni 16.6 fedha za nje ili kutekeleza awamu ya pili ya Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini ikiwa ni pamoja na kupeleka umeme kwenye Makao Makuu ya wilaya mpya. 
Usambazaji Umeme katika Mikoa ya Lindi na Mtwara
Mheshimiwa Spika, kwa takriban miaka mitano Mikoa ya Lindi na Mtwara imekuwa ikipata huduma ya umeme kutoka kwa Kampuni ya Artumas iliyokuwa inamiliki mitambo ya MW 18 iliyopo Mtwara. Kutokana na mdororo wa uchumi, Kampuni ya Artumas ilishindwa kutoa huduma hiyo na kuamua kuuza mitambo hiyo kwa Kampuni ya Wentworth, ambayo baadaye nayo iliiuzia Serikali kupitia TANESCO mwezi Machi, 2012. Katika Mwaka 2012/13 TANESCO itaendelea kutoa huduma za usambazaji umeme na uboreshaji miundombinu ya umeme katika Mikoa ya Mtwara na Lindi, ambapo Shilingi bilioni 5 zimetengwa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini. Katika zoezi hilo jumla ya vipozea umeme 48 vitafungwa na kuwezesha kuunganisha wateja wa awali 2,400.
Mikakati ya Kupunguza Gharama za Kuunganisha Umeme kwa Wateja
Mheshimiwa Spika, moja kati ya vikwazo vinavyokwamisha jitihada za Serikali za kuhakikisha kuwa huduma ya umeme inawafikia wananchi wengi zaidi na kwa kasi kubwa ni gharama kubwa za kuunganisha umeme na kipato cha wananchi wengi wanaohitaji kupata huduma ya umeme. Gharama hizo zimekuwa ni kikwazo katika azma ya Serikali ya kutimiza lengo la asilimia 30 ya wananchi watakaounganishiwa umeme ifikapo Mwaka 2015. 

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia changamoto hizo, Serikali kupitia TANESCO imedhamiria kupunguza gharama za kuunganisha umeme wa njia moja (single phase) kwa wateja wadogo mijini na vijijini kwa wastani wa kati wa asilimia 30 na 77. Kwa kufanya hivyo, wateja wengi watamudu gharama na hatimaye kuongeza kasi ya kuunganisha umeme. 
Mheshimiwa Spika, kutokana na uamuzi huo wa Serikali, gharama za uunganishaji umeme zitakuwa kama ifuatavyo: kwa wateja watakaojengewa njia moja (single phase) kwenye umbali usiozidi mita 30 bila kuhitaji nguzo, katika maeneo ya vijijini watalipa Shilingi 177,000 na wa mijini watalipa Shilingi 320,960 badala ya Shilingi 455,108 zinazolipwa na wateja hao  kwa sasa. Punguzo hili ni sawa na asilimia 61.11 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 29.48 kwa wateja waishio  mijini. 

Mheshimiwa Spika, kwa wateja watakaojengewa njia moja (single phase) na kuwekewa nguzo moja, katika maeneo ya vijijini watalipa Shilingi 337,740 na wa mijini watalipa Shilingi 515,618 badala ya Shilingi 1,351,884 zinazolipwa na wateja hao kwa sasa. Punguzo hili ni sawa na asilimia 75.02  kwa wateja waishio vijijini na asilimia 61.86 kwa wateja waishio  mijini. Aidha, kwa wateja watakaojengewa njia moja na kuwekewa nguzo mbili katika maeneo ya vijijini watalipa Shilingi 454,654 na wa mijini watalipa Shilingi 696,670 badala ya Shilingi 2,001,422 zinazolipwa na wateja hao kwa sasa. Punguzo hili ni sawa na asilimia 77.28  kwa wateja waishio vijijini na asilimia 65.19 kwa wateja waishio  mijini. Viwango hivyo vya gharama vitaanza kutumika mwezi Januari, 2013. 

Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeanzisha utaratibu wa kugharimia miundombinu ya kuwafikishia umeme wateja kwa miradi inayopata ruzuku kutoka Mfuko wa Nishati Vijijini (REF). Utaratibu huu utatumika kwa wateja watakaokuwa wamefunga nyaya za umeme kwenye nyumba zao katika maeneo ya miradi husika. Mpango huo utapunguza gharama za kuunganishiwa umeme kwa wastani wa asilimia 80 kulingana na idadi ya nguzo na mfumo utakaotumika (yaani Single au three phase). Idadi ya wateja wa awali watakaounganishiwa umeme kupitia mpango huo ni 100,000. 

Mradi wa Uendelezaji wa Umeme Utokanao na Maporomoko Madogo ya Maji 
Mheshimiwa Spika, lengo la mradi ni kufanya utafiti na kuendeleza miradi midogo ya maporomoko ya maji (mini hydro) kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa maeneo yaliyo nje ya Gridi ya Taifa. Kazi zilizopangwa kufanyika Mwaka 2012/13 ni kumpata Mshauri kwa ajili ya kufanya tafiti kwenye vyanzo vilivyobainishwa; na kuwezesha ununuzi wa mitambo ya uzalishaji na kujenga kwenye vyanzo vitakavyoonekana vinafaa kuendelezwa. Kiasi cha Shilingi bilioni 4.5 zimetengwa kwa ajili ya kazi hizo. 

Kuendeleza Shughuli za Utafutaji wa Gesi Asili na Mafuta

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TPDC itatangaza maeneo mapya ambayo hayajapata wawekezaji kwa ajili ya utafutaji mafuta na gesi asili. Zabuni ya awamu ya nne (4th Off-shore Licensing Round) kwa ajili ya kunadi maeneo mapya ya uwekezaji  inatarajiwa kutangazwa mwezi Septemba, 2012 Jijini Houston, Marekani. 

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu shughuli za utafutaji mafuta na gesi asili na kuhakikisha kuwa shughuli hizo zinafanyika kulingana na mpango kazi uliyoainishwa kwenye mkataba. Natoa rai kuwa, Serikali haitasita kufuta mikataba kwa kampuni zitakazoshindwa kutekeleza mpango kazi kwa muda uliopangwa kwa mujibu wa sheria. 
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia TPDC itaendelea kujenga uwezo wa kufanya ukaguzi ili kuhakikisha kuwa kampuni zote zinazofanya utafiti na uzalishaji wa gesi asili na mafuta zinatekeleza kazi zake kwa mujibu wa mikataba iliyopo. Aidha, Serikali itadurusu mikataba iliyopo na kufanya uchambuzi wa kina kabla ya kuingia mikataba mipya ya uzalishaji na ugawanaji mapato ya mafuta na gesi asili ili kuhakikisha kuwa maslahi ya Taifa yanazingatiwa. 

Uboreshaji wa Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2012/13, Kanuni za Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja zitapitiwa na kuboreshwa ili kuondoa upungufu uliojitokeza. Aidha, muundo na upatikanaji wa wajumbe wa Bodi ya Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PIC) utapitiwa upya ili kuboresha ufanisi wa mfumo huo. 
Kuwezesha Kampuni ya Mafuta (COPEC)
Mheshimiwa Spika, kufuatia azma ya Serikali ya kuihuisha Kampuni ya Mafuta ya Taifa (COPEC) ambayo ni kampuni tanzu ya TPDC, mwezi Agosti, 2011 EWURA ilitoa leseni kwa Kampuni hiyo kuanza biashara ya uagizaji na usambazaji wa mafuta nchini. Katika Mwaka 2012/13 Serikali itatafuta njia bora ya kuiwezesha COPEC kuanza utekelezaji wa jukumu hilo, ikiwa ni pamoja na kuidhamini COPEC kuweza kukopa kutoka katika benki za ndani na kuiwezesha kupata mafuta ya mkopo yenye masharti nafuu kutoka nchi zinazozalisha mafuta duniani. Lengo ni kuwa na uhakika wa upatikanaji (security of supply) wa mafuta nchini.
Sera, Sheria, Mipango na Mikakati inayohusu Sekta ya  Nishati 
Durusu ya Sera ya Taifa ya Nishati, 2003
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Nishati imeendelea kukua kwa kasi kubwa hali inayohitaji kuwepo kwa sera madhubuti, inayozingatia ukuaji huo pamoja na changamoto zilizopo. Hivyo, pamoja na jitihada za kudurusu Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2003, Serikali imelazimika pia kuandaa sera nyingine katika sekta hiyo zikiwemo sera za gesi asili, nishati vijijini, biofuel na nishati jadidifu. Katika Mwaka 2012/13, Wizara itakamilisha durusu ya Sera ya Nishati ya Mwaka 2003. 

 Kuandaa Sera, Sheria na Mpango Kabambe wa Matumizi ya Gesi Asili 

Mheshimiwa Spika, wadau wengi wakiwemo Waheshimiwa Wabunge wamekuwa na shauku kubwa ya kuona kuwa Sera, Sheria na Mpango Kabambe wa Matumizi ya Gesi Asili vinakamilishwa haraka ili utekelezaji wake uweze kuanza. Hata hivyo, utayarishaji wa Sera, Sheria na Mpango Kabambe unahitaji uchambuzi wa kina na ushirikishwaji mpana wa wadau. Lengo ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na usimamizi bora wa matumizi ya rasilimali hii kwa manufaa ya Taifa. 

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2012/13, Wizara itakamilisha Sera, Sheria na Mpango Kabambe wa Matumizi ya Gesi Asili. Sera na Sheria ya Gesi Asili zitakazoandaliwa zitazingatia uhamasishaji wa ushiriki wa Watanzania wakiwemo wenyeji wa mikoa ambayo shughuli za gesi na mafuta zinafanyika; kuongeza kiwango cha mrabaha; kuwezesha TPDC kushiriki zaidi katika uwekezaji; mgawanyo wa majukumu ya wadau wa sekta ndogo ya gesi na mafuta; na mwekezaji kulipa kiasi cha fedha kisichorudishwa (signature bonus) wakati wa kusaini mkataba.Kuhamasisha Matumizi ya Nishati Jadidifu katika Uzalishaji Umeme
Uendelezaji wa Rasilimali ya Joto Ardhi 
Mheshimiwa Spika, lengo la Wizara ni kuweka mazingira wezeshi katika uendelezaji wa nishati ya jotoardhi (geothermal) nchini.  Shilingi bilioni 1.0 zimetengwa katika Mwaka 2012/13 kwa ajili ya kuwezesha tathmini na kuchoronga visima vya majaribio kwenye eneo la Ziwa Ngozi (Mbeya). Maeneo mengine yenye viashiria vya kuwepo jotoardhi ni pamoja na Songwe (Mbeya); Ziwa Eyasi, Manyara na Natroni (Manyara); Mto Luhui - Rufiji (Pwani); na Kisaki (Morogoro). Mafanikio ya uchorongaji huo yatawezesha kubainisha uwepo wa joto la kutosha kwa ajili ya ufuaji umeme, hivyo kuongeza wigo wa vyanzo vya kufua umeme nchini. 

Uendelezaji wa Nishati kwa Kutumia Tungamotaka 
Mheshimiwa Spika, katika eneo hili Wizara inalenga kuhamasisha matumizi ya majiko banifu, mabaki ya mazao ya mashambani na taka salama za viwandani katika kuzalisha umeme na biogas kwa kupikia. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na kuwezesha ujenzi wa mitambo ya biogas katika Kanda ya Ziwa kwenye shule na zahanati; kuhamasisha matumizi ya majiko banifu kwenye taasisi mbalimbali kama magereza na shule. Kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya kazi hizo katika Mwaka 2012/13 ni Shilingi milioni 261

Uendelezaji wa Biofuel 
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2012/13 jitihada zitaelekezwa katika kuweka mazingira wezeshi ya kisera, kisheria na kitaasisi ili kuendeleza biofuel nchini. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na kukamilisha sera ya biofuel; kuandaa mkakati wa kutekeleza sera; kujenga uwezo wa taasisi za Serikali katika kusimamia masuala ya biofuel; na kuandaa sheria ya biofuel. Jumla ya Shilingi bilioni 2.19 zikiwemo Shilingi milioni 50, fedha za ndani zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza kazi hizo. 

Matumizi Bora ya Nishati 

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi bora ya nishati kupitia mradi wa Low Carbon Energy Efficient and Climate Change Mitigation. Mradi huo ni wa miaka minne na unalenga kusaidia upatikanaji na kuhamasisha matumizi endelevu ya nishati kwa wananchi wengi, hususan, maeneo ya vijijini. Mradi huo pia utahamasisha Halmashauri za Wilaya kuweka kipaumbele katika kuendeleza miradi ya nishati jadidifu (renewable energies) na matumizi bora ya nishati (energy efficiency) kwa kutenga fedha za miradi hiyo katika mipango yao. Mradi unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Serikali. Ili kutekeleza mradi huu, kwa Mwaka 2012/13 UNDP imetoa Shilingi bilioni 1.33
SEKTA YA MADINI

Utoaji na Usimamizi wa Leseni za Madini

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2012/13, Wizara itaendelea kuboresha Mfumo wa Utoaji na Usimamizi wa Leseni, hususan kuongeza kasi ya mawasiliano ya mfumo huo kwa kutumia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano; kuongeza idadi ya watumishi wenye ujuzi wa kutumia mfumo huo; kuboresha kanzidata (database); na kuendelea kuongeza vitendea kazi kwenye ofisi zote zinazotumia mfumo huo.
 Kuendeleza Uchimbaji Mdogo wa Madini
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kukamilisha taratibu za kisheria za kutenga na kugawa maeneo kwa ajili ya uchimbaji mdogo. Maeneo hayo ni pamoja na Nyakunguru, Goronga, Gibaso na Mogabiri (Tarime); Kapalamsenga (Mpanda); Ilagala (Kigoma Vijijini); Ibaga na Mpambaa (Mkalama); Isenyela (Chunya); na Makanya (Same). Maeneo yote haya yana jumla ya hekta 105,163 zinazoweza  kutolewa leseni  takriban 10,516 za uchimbaji mdogo zenye ukubwa wa hekta 10 kila moja.

Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 8.9 kwa ajili ya kuwaendeleza wachimbaji wadogo ikiwa ni pamoja na kuwapa mikopo kwa Mwaka 2012/13. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 2.5 ni fedha za ndani na Dola za Marekani milioni 4, sawa na Shilingi bilioni 6.4, ni fedha za nje kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali za Madini (SMMRP) unaofadhiliwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia. Kutolewa kwa fedha hizo kutawezesha wachimbaji wadogo kufanya kazi zao kwa kutumia nyenzo za kisasa hivyo kuongeza tija na ufanisi na hatimaye kusaidia katika juhudi za kupunguza umaskini wa kipato kama ilivyoelekezwa katika Malengo ya MKUKUTA II.

Mheshimiwa Spika, vilevile Wizara itaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo kuhusu biashara na masoko ya madini, masuala ya afya, usalama na utunzaji mazingira katika shughuli za uchimbaji madini ili waweze kuzingatia Sheria na Kanuni za Madini. 

Uongezaji Thamani Madini

Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha usimamizi na uratibu wa shughuli za uongezaji thamani madini nchini, Wizara imeanzisha Sehemu ya Uongezaji Thamani Madini. Katika Mwaka 2012/13, Sheria ya Uongezaji Thamani Madini itaandaliwa. Vilevile, Wizara itashirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha mbinu bora za uchenjuaji madini kwa ajili ya kunufaisha wachimbaji wadogo wengi zaidi. Kwa kufanya hivyo, ni matarajio ya Serikali kuwa kiasi cha madini yanayoongezwa thamani kitaongezeka kutoka asilimia sifuri hadi asilimia 70 ya tani 30,000 ya shaba ghafi zinazozalishwa na wachimbaji wadogo na wa kati kwa mwaka kwa sasa; na kutoka asilimia 35 hadi asilimia 50 ya kilo milioni 1.3 za vito zinazozalishwa kwa mwaka kwa sasa.
Uimarishaji wa Soko la Madini ya Vito

Mheshimiwa Spika, kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika Maonesho ya Kwanza ya Kimataifa ya Vito na Usonara, Wizara itaandaa maonesho ya pili yanayotarajiwa kufanyika tarehe 18 hadi 22 Aprili, 2013 mjini Arusha kwa kuhakikisha kuwa yanafanikiwa zaidi na kuboresha mfumo wa soko la madini, uhamasishaji uongezaji thamani; na uendelezaji tasnia ya uchimbaji wa madini ya vito nchini. Aidha, Serikali itaendelea kusimamia tasnia ya almasi na vito hapa nchini kwa kutambua, kuchambua na kuthamini madini hayo kupitia Kitengo cha TANSORT.

Kuimarisha Afya, Usalama na Utunzaji wa Mazingira  Migodini

Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kusimamia Sheria zote zinazohusu Afya, Usalama na Utunzaji wa Mazingira migodini kwa kuimarisha kaguzi katika migodi mikubwa, ya kati na midogo. Aidha, katika kuhakikisha kuwa migodi ya wachimbaji wadogo wa madini wa Kitalu B kilichopo Mererani Wilayani Simanjiro, haiathiriki na mafuriko kutokana na mvua, Serikali imeanza ujenzi wa mtaro katika eneo la D’souza. Kazi hii inatarajiwa kukamilika katika Mwaka 2012/13 na imetengewa Shilingi milioni 500.
 Mheshimiwa Spika, mipango ya ufungaji  migodi (mine closure plans) ya Geita, Tulawaka, Bulyanhulu, Buzwagi, Williamson Diamond na TanzaniteOne itaboreshwa na kukamilishwa katika Mwaka 2012/13. Baada ya mipango hiyo kupitishwa, migodi husika itaanzisha mifuko ya ukarabati wa mazingira. 
Maandalizi ya Sheria ya Baruti 
Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka 2012/13, Wizara itadurusu Sheria ya Baruti ya Mwaka 1963 ili iendane na mazingira na teknolojia ya sasa. Aidha, Wizara itaendelea kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo kuhusu utunzaji, usafirishaji na utumiaji wa baruti; na kutoa mafunzo kwa wakaguzi wa baruti ili waweze kwenda na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Utekelezaji wa Shughuli za TEITI 

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka 2012/13, Kamati Tekelezi itaendelea kuandaa Sheria ya TEITI pamoja na kujenga uwezo juu ya uendeshaji wa TEITI kwa wajumbe wa Kamati na Sekretarieti. Kamati pia imepanga kuelimisha na kuhamasisha wachimbaji wadogo kushiriki katika utoaji wa takwimu za malipo katika uandaaji wa ripoti ya tatu ya TEITI itakayohusisha hesabu za kipindi cha Mwaka 2010/11. Lengo ni kubaini mchango wa sekta ndogo ya uchimbaji madini kama ilivyo kwa kampuni kubwa ili kuwezesha Serikali kupima maendeleo ya ukuaji wa sekta hii mwaka hadi mwaka. 

Kuongeza Fungamanisho la Sekta ya Madini na Sekta Nyingine za Uchumi
Mheshimiwa Spika, mojawapo ya njia ya kuongeza fungamanisho la Sekta ya Madini na sekta nyingine za uchumi ni kuhakikisha kuwa kampuni zinazojihusisha na shughuli za madini nchini zinatumia kwa wingi huduma na bidhaa za ndani kadri zinavyopatikana. Hii ni katika kutekeleza Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ambayo inasisitiza kampuni za madini kutumia huduma na bidhaa zinazopatikana hapa nchini kama vifaa vya ofisi, chakula na vinywaji, ushauri wa kisheria, ulinzi, utunzaji wa mazingira na chokaa. Katika kufikia azma hiyo, Serikali itaendelea kuweka mkazo kwa kampuni za madini kutumia bidhaa na huduma za hapa nchini ili kuhakikisha kuwa Watanzania wananufaika na shughuli za uchimbaji madini. 
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa, migodi mikubwa ya dhahabu nchini imenunua bidhaa na huduma za ndani zenye thamani ya takriban Dola za Marekani bilioni 3.5, na nje Dola za Marekani bilioni 4.3 katika kipindi cha kuanzia Mwaka 2001 hadi 2011. Kwa takwimu hizo, ununuzi wa ndani ni asilimia 44.8 na wa nje ni asilimia 55.2. Serikali bado hairidhishwi na kiwango hicho cha ununuzi wa ndani. Hivyo, wamiliki wa migodi wanatakiwa kutoa kipaumbele kwa kununua bidhaa za ndani ambazo zinakidhi viwango.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2012/13, Wizara itaanzisha utaratibu wa kubainisha mahitaji muhimu ya huduma na bidhaa zinazohitajika kwenye kampuni za madini. Utaratibu huu utakuwa ni msingi wa kuwahamasisha na kuwawezesha Watanzania kukidhi viwango vya huduma na bidhaa zinazohitajika migodini. Lengo ni kuongeza kiwango cha ununuzi wa bidhaa na huduma za ndani ili kuleta manufaa zaidi kwa Watanzania.

Ujenzi na Uboreshaji wa Ofisi za Madini

Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka 2012/13 Wizara itaanza ujenzi wa Ofisi ya Madini ya Kanda ya Magharibi (Mpanda), Kanda ya Kusini (Mtwara) na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi (Dodoma). Aidha, ukarabati wa Ofisi ya Madini Kanda ya Kati - Magharibi (Shinyanga) na Ofisi ya Madini ya Kanda ya Kaskazini (Arusha) utakamilishwa.
Mheshimiwa Spika, ili kuwa na usalama zaidi katika kazi zinazofanywa na Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na Kitengo cha TANSORT, Wizara imeona ni vyema taasisi hizo ziwe na jengo la kudumu na kuepusha gharama kubwa za ukodishaji wa majengo ya ofisi. Katika Mwaka 2012/13 Wizara itaanza maandalizi ya ujenzi wa jengo hilo. Mbali na matumizi ya ofisi, jengo hilo litakuwa ni kituo cha kimataifa cha biashara ya madini nchini. 
Mheshimiwa Spika, kituo hicho kitatoa huduma mbalimbali zikiwemo ukaguzi na uhakiki wa madini hususan dhahabu, almasi na vito; utambuzi na uthamini wa madini ya almasi na vito; vyumba maalumu vya kuuzia na kununulia madini ya dhahabu, almasi na vito; vyumba vya kuhifadhi madini; na utoaji wa vibali kwa ajili ya kusafirisha madini nje ya nchi. Pia, Kituo kitakuwa na sehemu salama ya kufanyia biashara ya madini, kuongeza makusanyo yatokanayo na biashara ya madini na kuwapatia soko wafanyabiashara wa madini nchini.

WAKALA WA UKAGUZI MADINI TANZANIA - TMAA

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2012/13, Serikali itaongeza kasi ya ukaguzi na udhibiti wa shughuli za uzalishaji na biashara ya madini nchini kupitia TMAA ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inaleta manufaa zaidi kwa Taifa. Ukaguzi utakaofanyika utahusisha migodi mikubwa, ya kati na midogo kwa madini yote. Pia, Wakala utaendelea kujenga uwezo kwa watumishi wake katika kubainisha maoteo ya mapato ya Serikali kutoka kwenye Sekta ya Madini kwa kutumia mfumo wa kisasa (revenue forecasting model) ili kuwa na takwimu za uhakika za mapato ya Serikali kutoka sekta hiyo na kuzitumia katika kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali. Wakala pia utaendelea kuboresha maabara yake ili iweze kupata usajili katika Shirika la Viwango vya Kimataifa (ISO 17025) na hivyo kujiendesha kibiashara.
Migodi Kulipa Kodi ya Mapato
Mheshimiwa Spika, ili nchi yetu iweze kunufaika zaidi na shughuli za uchimbaji mkubwa wa madini nchini, mikakati iliyopo ni pamoja na kuhakikisha kuwa migodi inaendelea na mingine inaanza kulipa kodi ya mapato na gawio kwa migodi ambayo Serikali ina hisa. Kabla mgodi haujaruhusiwa na Serikali kujengwa, wamiliki wake wanawajibika kuwasilisha taarifa za upembuzi yakinifu zinazoonesha gharama za uwekezaji, muda wa mgodi kurudisha gharama na muda wa kuanza kulipa kodi ya mapato. Kimsingi, taarifa hizo ndizo zinazotumiwa na Serikali kufikia uamuzi wa kuingia mkataba wa uendelezaji mgodi na kampuni husika.   
Mheshimiwa Spika, bei ya dhahabu katika soko la dunia imeendelea kupanda kwa kiwango kikubwa, ukilinganisha na kiwango cha nyuma wakati migodi hiyo inaanzishwa. Hali hiyo inawezesha muda wa urejeshaji gharama za uwekezaji kupungua na hivyo kuanza kulipa kodi ya mapato mapema. Hata hivyo, licha ya kupanda kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia baadhi ya migodi haijaanza kulipa kodi ya mapato kwa madai kwamba haijarudisha gharama za uwekezaji. Hivyo, Serikali kupitia Wakala wa Ukaguzi wa Madini kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato (TRA) itaendelea kukagua na kuhakiki gharama za uwekezaji na uendeshaji kwenye migodi mikubwa na ya kati ili kuhakikisha kodi hizo zinalipwa mapema.  
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa rai kuwa migodi yote ianze kulipa kodi ya mapato bila kuleta visingizio kuwa hawajarudisha gharama au wanapata hasara pamoja na muda  walioonesha  kwenye taarifa za upembuzi yakinifu kufika. Bei zilizoainishwa kwenye taarifa za upembuzi yakinifu kwa wakati huo ni ndogo mara tano ya bei ya sasa, hali inayoashiria kuwa migodi imerudisha gharama za uwekezaji mapema kuliko inavyokadiriwa kwani gharama za uendeshaji haziwezi kupanda sawa na bei ya dhahabu inavyopanda. Ni matumaini yangu kuwa kama mwekezaji ameendelea kuchimba kwa muda wa miaka mitano hadi saba ameishapata faida na kurejesha gharama zake.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia hali hiyo, kupitia Bunge lako Tukufu, naagiza kampuni zote zilizochimba madini kwa miaka mitano na kuendelea, zianze kulipa kodi ya mapato bila kuleta visingizio. Na kama Kampuni bado inapata hasara na haiwezi kuchangia katika uchumi wa Taifa kwa kulipa kodi ya mapato, ifunge mgodi wake na kuondoka kwa kuwa madini hayaozi. Haiwezekani kukaa miaka saba unaendelea kupata hasara lakini upo. Serikali itaendelea kushirikiana na Kampuni zilizo tayari kuanza kulipa kodi ya mapato kwa wakati bila masharti. 

SHIRIKA LA MADINI LA TAIFA – STAMICO
Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa kutekelezwa na STAMICO katika Mwaka 2012/13 ni kuendelea kusimamia kwa karibu upembuzi yakinifu unaofanyika kwenye mradi wa dhahabu wa Buckreef; kufanya majadiliano na kuingia mkataba wa ubia na kampuni itakayoibuka mshindi kwa ajili ya kuliendeleza upya eneo la Mgodi wa Buhemba; na kuanzisha uzalishaji wa dhahabu kutokana na mabaki ya uchimbaji wa zamani katika eneo hilo. Uzalishaji huo pamoja na huduma mbalimbali utatoa ajira ya Watanzania wasiopungua 120. 
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) itaendelea kuwatambua wachimbaji wadogo kwa kuanzisha kanzidata (database) itakayokuwa na taarifa na takwimu zote muhimu zinazowahusu; kufanikisha upatikanaji wa mikopo, mitambo, vifaa na zana za uchimbaji; kutoa elimu na huduma za ushauri katika utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji na uingiaji wa mikataba. Kazi zote hizi zitafanyika kwa kushirikisha idara na taasisi zote ambazo zimekuwa zinatoa huduma kwa wachimbaji wadogo. Taasisi hizo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM); Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT); Shirika la Uendelezaji Viwanda Vidogo (SIDO); Chuo cha Ufundi Stadi (VETA); kampuni na taasisi binafsi.
WAKALA WA JIOLOJIA TANZANIA – GST

 Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2012/13, Wakala wa Jiolojia Tanzania utafanya upimaji na uchoraji wa ramani tano za jiolojia na jiokemia (QDSs 280, 281, 282, 283 na 284) katika Wilaya za Kilwa, Lindi, Liwale na Ruangwa. Wakala pia, utafanya kazi ya ukusanyaji wa takwimu za jiofizikia kwa kutumia ndege (High Resolution Airborne Geophysical Survey – Gravity, Magnetic, Radiometric and Elecromagnetic) katika QDSs 34 katika Mikoa ya Dodoma, Manyara, Mbeya, Morogoro, Pwani, Singida na Tanga. Zoezi hili litagharimiwa kwa pamoja kati ya Serikali na Benki ya Dunia, ambapo Serikali itachangia Shilingi milioni 750 na Benki ya Dunia itatoa mkopo wa Dola za Marekani milioni 11.55. Aidha, ramani 60 za zamani zitabadilishwa kutoka kwenye mfumo wa karatasi na kuziweka kwenye mfumo wa digital.
Mheshimiwa Spika, Wakala pia umepanga kufanya ukarabati mkubwa kwenye kituo cha kupimia matetemeko ya ardhi kilichopo Dodoma ili kiweze kunakili moja kwa moja kwenye mfumo wa kompyuta (server) taarifa za matetemeko mara yanapotokea (real time seismic station). Aidha, ukusanyaji wa takwimu za matukio ya matetemeko ya ardhi kutoka kwenye vituo kumi vya kupimia matetemeko ya ardhi vilivyoko nchini (Babati, Dodoma, Geita, Kibaya, Kondoa, Mahale, Manyoni, Mbeya, Mtwara na Singida) utaendelea ikiwa ni pamoja na kuchakata takwimu hizo na kuandaa taarifa za matukio hayo. Wakala utaendelea kuboresha miundombinu, vitendea kazi na rasilimali watu ili kuongeza ufanisi na tija.
 CHUO CHA MADINI DODOMA - MRI

Mheshimiwa Spika, katika Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2012/13, Chuo cha Madini kitaendelea kutoa mafunzo katika ngazi ya Cheti na Stashahada katika fani za Jiolojia na Utafutaji Madini, Uhandisi Uchimbaji Madini na Uhandisi Uchenjuaji Madini. Pia, kwa kutambua umuhimu wa kuwa na wataalamu wa kutosha katika sekta ndogo ya mafuta na gesi asili nchini, Chuo kitaanzisha kozi mpya za Jiolojia ya Mafuta na Gesi; na Uhandisi na Usimamizi wa Mazingira Migodini katika ngazi ya Cheti na Stashahada. Aidha, watumishi wa Chuo wataendelezwa kitaaluma na kitaalamu ili waweze kutoa mafunzo yaliyokusudiwa. 
Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zitakazofanyika ni uendelezaji wa miundombinu kwa kuanza ujenzi wa jengo la taaluma lenye vyumba vya mihadhara vyenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 100 kila kimoja na ukumbi wa mikutano wenye uwezo wa kuchukua watumiaji 500 kwa wakati mmoja. Lengo ni kupanua wigo wa mafunzo na kudahili wanafunzi wengi zaidi.
AJIRA NA MAENDELEO YA WATUMISHI

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2012/13 Wizara itaajiri jumla ya watumishi 267 wa kada mbalimbali. Kati ya hao watumishi 65 ni kwa ajili ya Wizara, TPDC 51, REA 16, MRI 33, STAMICO 30, TMAA 15 na GST 57. TANESCO itaendelea kuajiri watumishi kulingana na taratibu zilizounda Shirika hilo. Aidha, ili kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa Sekta za Nishati na Madini, Wizara imepanga kuwajengea uwezo jumla ya watumishi 206 kwa kutoa mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi. Mbali na fani za mafuta na gesi asili, kipaumbele kitatolewa katika maeneo maalumu yakiwemo energy economics; geothermal; uranium; mineral economics; diamond valuation and sorting; na contracts negotiations and management in energy and mineral sectors. 
Mheshimiwa Spika, kufuatia ugunduzi mkubwa wa gesi asili nchini, Wizara imeanzisha Mpango wa Uendelezaji Rasilimali Watu (Marshall Plan on Capacity Building and Development in Oil and Gas Industry 2012 – 2016). Mpango huu utawezesha Watanzania kati ya 30 hadi 50 kupata elimu katika ngazi ya shahada na shahada za uzamili kwenye fani za mafuta na gesi asili. Maeneo yatakayopewa kipaumbele ni pamoja na petroleum geosciences, petroleum geophysics, petroleum geochemistry, petroleum engineering, energy modelling, oil and gas economics, oil and gas accounting and auditing, oil and gas legal regimes na contract negotiations. Mpango huu utatekelezwa na Wizara kwa kushirikiana na TPDC kupitia  fedha za uendelezaji rasilimali watu zinazotokana na mikataba ya uzalishaji na ugawanaji wa mafuta na gesi asili pamoja na Washirika wa Maendeleo. 
Mheshimiwa Spika, ili kufikia lengo hilo, katika Mwaka 2012/13 Wizara imeamua kusomesha wanafunzi 10  waliofanya vizuri kidato cha sita katika masomo ya physics, chemistry na mathematics na wenye nia ya kuchukua shahada ya kwanza katika fani ya mafuta na gesi asili katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Vilevile, Wizara itachangia gharama za masomo kwa wanafunzi 15 watakaochaguliwa kujiunga katika ngazi ya cheti na Stashahada katika Chuo cha Madini, Dodoma (MRI). Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeanza kutayarisha mitaala ya shahada ya uzamili katika fani ya gesi na mafuta na wanafunzi watakaogharimiwa na Wizara yangu wataanza masomo katika Mwaka 2013/14. Pia, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) inatayarisha mitaala ya stashahada/shahada kwenye fani hii.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mpango wa Serikali wa kupunguza matumizi ya fedha za umma, hasa katika ununuzi wa magari yenye gharama kubwa, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba Wizara yangu itatekeleza kwa dhati agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu la kudhibiti matumizi ya magari ya aina hiyo kuanzia Mwaka 2012/13. Katika utekelezaji huo, viongozi waandamizi wa Wizara wakiwemo Makamishna na Wakurugenzi waliokuwa wanahudumiwa na magari ya gharama kubwa wataanza kutumia magari ya kawaida, ambayo ujazo wa injini hautazidi sentimita za ujazo (CC) 3,000 kwa utaratibu wa kukopeshwa. Mpango huo utawezesha Wizara kuokoa zaidi ya Shilingi bilioni 1.4 kwa mwaka. Fedha hizo zitatumika katika shughuli nyingine za maendeleo. Aidha, mpango huo utapunguza matumizi ya magari ya Serikali baada ya saa za kazi na siku ambazo siyo za kazi.

USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Mheshimiwa Spika, Wizara ilinufaika na itaendelea kupata misaada na ushirikiano kutoka kwa washirika mbalimbali wa maendeleo kwa kipindi cha Mwaka 2012/13. Kwa niaba ya Serikali napenda kutoa shukurani kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, hususan katika kuwezesha kupatikana kwa mkopo wa masharti nafuu wa mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la gesi asili kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Aidha, natoa shukurani kwa Serikali za nchi za Brazil, Canada, Finland, Marekani, Norway, Sweden, Trinidad na Tobago, na Urusi. Vilevile, natoa shukurani kwa Benki ya Exim ya China, Benki ya Maendeleo ya Afrika Kusini (DBSA), Benki ya HSBC, Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Benki ya BADEA, Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB), Umoja wa Ulaya (EU), pamoja na taasisi na mashirika ya AFD (Ufaransa), CIDA (Canada), DANIDA (Denmark), ECDF (Korea Kusini), FINIDA (Finland), JICA (Japan), MCC (Marekani), NORAD (Norway), OFID (Saudi Arabia), ORIO (Uholanzi) na Sida (Sweden), GEF, GVEP, IDA, IFC, UNDP, UNEP, UNIDO, UNICEF na Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola.

E.  SHUKURANI

Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kuwashukuru Naibu Mawaziri wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhe. George Boniface Simbachawene, Mbunge -  Jimbo la Kibakwe, anayesimamia masuala ya nishati; na Mhe. Stephen Julius Masele, Mbunge - Jimbo la Shinyanga Mjini, anayesimamia masuala ya madini, kwa kunisaidia kwa kiasi kikubwa na kwa dhati kabisa katika kutekeleza majukumu yangu. Aidha, nawashukuru Mawaziri wote walionitangulia katika kuongoza Wizara ya Nishati na Madini. Napenda kumshukuru Katibu Mkuu Bw. Eliakim C. Maswi kwa uchapakazi wake mahiri na ushirikiano alionipa katika kipindi hiki kifupi tangu niteuliwe kuwa Waziri wa Nishati na Madini.  Vilevile, nawashukuru Makamishna wote, Wakuu wa Idara na Vitengo, Viongozi wa Taasisi na Bodi zilizo chini ya Wizara kwa ushirikiano wao katika kufanikisha maandalizi ya bajeti hii. Mwisho lakini sio kwa umuhimu, nawashukuru watumishi wote wa Wizara na Taasisi zilizo chini yake kwa michango yao iliyowezesha kuandaliwa kwa mpango na bajeti hii. Natumia fursa hii kuwakumbusha watumishi wote wa Wizara kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia viapo tulivyojiwekea siku ya tarehe 21 Mei, 2012 tulipokutana kwa mara ya kwanza. Kipekee naomba nimshukuru sana mke wangu Bertha Muhongo, wanangu Godfrey Chirangi, Musuto Chirangi, Dkt. Bwire Chirangi na Rukonge Muhongo pamoja na familia yangu kwa ujumla kwa msaada mkubwa wanaonipa.

HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Mwaka 2012/13 inalenga kutatua matatizo ya kutopatikana kwa umeme wa kutosha na wa uhakika nchini; na kuimarisha usimamizi wa Sekta za Nishati na Madini ili kuongeza mchango wake katika kukuza uchumi wa Taifa, kuongeza ajira hasa kwa vijana na kupunguza umaskini nchini. 
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa liidhinishe bajeti ya jumla ya Shilingi 641,269,729,000 kama ifuatavyo:

Bajeti ya maendeleo ni Shilingi 531,190,861,000, sawa na asilimia 82.83  ya  bajeti  yote  ya Wizara. Kati ya fedha hizo, Shilingi 431,190,861,000 ni fedha za ndani, sawa  na  asilimia 81.17  ya  fedha za maendeleo na Shilingi 100,000,000,000 ni fedha za nje, sawa na asilimia 18.83; na

Matumizi ya Kawaida ni Shilingi 110,078,868,000, sawa na asilimia 17.17 ya bajeti yote ya Wizara. Kati ya fedha hizo Shilingi 17,292,347,000 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Wizara, Mashirika na Taasisi zake (sawa na asilimia 2.70 ya bajeti yote ya Wizara) na Shilingi 92,786,521,000, sawa na asilimia 14.47 ya bajeti yote ya Wizara, ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (O.C).

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments: