BAJETI YA WIZARA YA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA KWA MWAKA 2012 - 2013...


HOTUBA YA WAZIRI WA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA MHESHIMIWA PROF. MAKAME MNYAA MBARAWA (Mb.), WAKATI WA KUWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Peter Joseph Serukamba (Mb.) kuhusu Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa kazi za Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2011/2012 na Malengo ya Wizara katika bajeti ya mwaka 2012/2013. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia pamoja na Taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nitangulize dua zangu kwa Mwenyezi Mungu kuwa azipokee na kuzilaza pema roho za Waheshimiwa Wabunge waliotangulia mbele ya haki tokea mkutano wa Bajeti wa mwaka 2011/2012  ulipofanyika.
Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea na hotuba yangu, naomba uniruhusu kutumia fursa hii kukumbuka tukio zito na la majonzi la tarehe 18 Julai 2012 ambapo Taifa liliwapoteza watu wengi na wengine wengi kujeruhiwa kupitia ajali ya Meli ya Mv Skagit katika eneo la kisiwa cha Chumbe karibu na Bandari ya Malindi, mjini Zanzibar. Ninapenda kuungana na Watanzania wenzangu kuwapa pole wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika ajali hiyo. Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi, Amina.
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kuwapongeza wale wote walioteulewa na Mheshimiwa Rais katika Baraza la Mawaziri kufuatia mabadiliko aliyofanya mwezi Mei, 2012 kama ifuatavyo: Mhe. Dkt. William Augustao Mgimwa (Mb), kuwa Waziri wa Fedha; Mhe. Prof. Sospeter Mwijaribu Muhongo (Mb), kuwa Waziri wa Nishati na Madini; Mhe. Mhandisi Christopher Kajoro Chiza (Mb), kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika; Mhe. Dkt. Harrison George Mwakenyembe (Mb), kuwa Waziri wa Uchukuzi; Mhe. Dkt Fenella Ephraim Mukangara (Mb), kuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo; Mhe. Balozi Khamis Sued Kagasheki (Mb), kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii; na Mhe. Dkt. Abdallah Omari Kigoda (Mb), kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko. Pia, napenda kuwapongeza wote walioteuliwa kuwa Naibu Mawaziri katika Wizara mbalimbali.
Vilevile, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote waliochaguliwa kuiwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki na Bunge la Afrika. Ni matumaini yangu kuwa watatuwakilisha vyema kwa maslahi na manufaa ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, napenda sasa kutumia fursa hii kutoa shukrani zangu za pekee kwa wote walioniwezesha kutekeleza majukumu ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kwa kipindi kilichopita, na ambao wamewezesha kuandaa mpango wa mwaka wa fedha 2012/2013 na kuboresha hoja ambayo naiwasilisha katika hotuba hii. Aidha, namshukuru Mheshimiwa January Yusuf Makamba (Mb.), Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia; Dkt. Florens Martin Turuka, Katibu Mkuu; na Dkt. Patrick James Makungu, Naibu Katibu Mkuu. Vilevile, napenda kuwashukuru watendaji wote katika Wizara, Taasisi na Mashirika yaliyo chini ya Wizara kwa ushirikiano wao katika kufanikisha uwasilishaji wa hotuba hii.

Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru kwa namna ya pekee Waheshimiwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Peter Joseph Serukamba, Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), kwa ushauri wao uliotuwezesha kutekeleza majukumu yetu kwa tija na ufanisi. Aidha, napenda kumshukuru Mhe. Suzan A. Lyimo, Mbunge wa viti maalum (CHADEMA) ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, kwa ushirikiano wake na mchango wake katika kuiboresha hoja hii ninayoiwasilisha katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia inayo dhamana ya kusimamia, kuimarisha na kuendeleza Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ili viweze kuchangia zaidi katika maendeleo ya nchi. Vilevile, Wizara inayo dhamana ya kusimamia na kutoa miongozo kwa Taasisi, Mashirika, Tume na Kampuni ambazo zinafanya kazi chini yake. 

Mheshimiwa Spika, wakati wa kutekeleza majukumu yake katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/2012, Wizara imezingatia miongozo ifuatayo; Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Mwaka 2011/12 – 2015/16 na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010–2015. 

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MIPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2011/2012
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ilitengewa jumla ya Sh. 64,017,516,000. Kati ya fedha hizo, Sh. 23,799,259,000 zilitengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Kati ya fedha hizo za matumizi ya kawaida Sh. 14,765,658,000 zilikuwa ni kwa ajili ya mishahara na Sh. 9,033,601,000 zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi mengineyo. Fedha za maendeleo zilizoidhinishwa zilikuwa Sh. 40,218,257,000 ambapo fedha za ndani zilikuwa Sh. 38,195,679,000 na fedha kutoka nje zilikuwa Sh. 2,022,578,000.

Mheshimiwa Spika, majukumu yaliyotekelezwa na Wizara pamoja na Taasisi zake katika kipindi cha mwaka 2011/12 ni haya yafuatayo:

 MAWASILIANO

 Uwekezaji, Ajira na Ukuaji wa Sekta ya Mawasiliano
 
Mheshimiwa Spika, Mawasiliano ni sekta inayokua kwa kasi hapa nchini na duniani kote na imekuwa ikichangia kikamilifu katika maendeleo ya mataifa mbalimbali na pia imekuwa ikiwezesha sekta nyingine kukua na kuboresha maisha ya wananchi wake. Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi nchini, sekta ya mawasiliano ilikua kwa asiasilia 22 (mwaka 2009), asilimia 21.5 (mwaka 2010), na asilimia 19.0 (mwaka 2011). Hata hivyo, takwimu hizi zilitegemea zaidi takwimu na mahesabu yaliyowasilishwa na watoa huduma wenyewe.

Mheshimiwa Spika, mchango wa sekta kwenye pato ghafi la taifa (GDP) umekuwa ukiongezeka kwa kasi ndogo isiyowiana na kukua kwa sekta yenyewe kama ifuatavyo: asilimia 2.7 (mwaka 2009), asilimia 2.2 (mwaka 2010) na asimilia 2.1 (mwaka 2011).

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania iko katika mchakato wa kuboresha upatikanaji wa takwimu sahihi ikiwemo kufungwa kwa mtambo wa kuhakiki mawasiliano (Traffic Monitoring System - TMS) ambao utatumika pia kupata takwimu zenye uhakika zaidi za mapato yanayotokana na huduma za mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, mchakato wa uwekaji wa mtambo huu ambao unatarajiwa kuanza kutumika katika mwaka huu wa fedha umekwisha anza ambapo tathmini ya makampuni yaliyoonyesha nia ya kujenga mtambo huu ilifanyika mwezi Juni 2012, na Kampuni zilizoonyesha uwezo wa kufanya kazi hiyo zimeombwa kuwasilisha taarifa zao za kitaalamu na kifedha (technical and financial proposals) kwa ajili ya hatua za kupata Kampuni itakayofanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, uwekezaji katika sekta hii ya mawasiliano umeendelea kuongezeka kwa kasi kubwa katika miaka ya hivi karibuni. Uwekezaji huo uko katika maeneo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa minara ya mawasiliano, uwekaji wa vifaa vya mawasiliano na katika ubunifu wa bidhaa mpya za huduma za mawasiliano zikiwemo huduma za kibenki.

Ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, mchakato wa kujenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ni endelevu na unatekelezwa kwa kushirikisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi. Mradi wa ujenzi wa Mkongo wa Taifa umebuniwa kuwa na awamu tano (V). Utekelezaji wa ujenzi wa Mkongo wa Taifa awamu ya I na II umekamilika. Kukamilika kwa awamu ya I na II kunaufanya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kuwa na jumla ya kilomita 7,560 na umeunganisha Makao Makuu ya mikoa ya Tanzania Bara. Aidha, Mkongo huu umeweza kuunganisha baadhi ya wilaya hususan zile zilizo ndani ya Makao Makuu ya Mikoa. Andiko dhana kwa ajili ya awamu ya III itakayohusu kukamilisha kwa uunganishwaji wa Makao Mkauu ya Wilaya zote, ujenzi wa viunganisho muhimu (Missing links, IP-MPLS Service layer) na Vituo Vikubwa vya Kuhifadhi Kumbukumbu (Data Centres) limekamilika. Aidha, awamu ya IV inahusu ujenzi wa mikongo ya mijini (Metro Networks). Ujenzi wa mikongo ya mijini unaendelea kutekelezwa kwa kushirikiana na watoa huduma za mawasiliano na imekamilika katika jiji la Dar es Salaam. Awamu ya V inahusu uunganishaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika maeneo mengine ya matumizi ikiwa ni pamoja na kumfikia mtumiaji wa mwisho (Last Mile Broadband Connectivity) na maandalizi yake yanaendelea.

Mheshimiwa Spika, Aidha, Kimataifa, Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umeunganishwa na mikongo ya baharini ya SEACOM, EASSy na SEAS ambao unaoendelea kujengwa na utatuunganisha na Sychelles. Mkongo Taifa pamoja na ile ya baharini inatoa huduma za maunganisho ya mawasiliano kwa nchi zote za jirani ambazo hazijapakana na bahari na pia kuzipa huduma mbadala nchi zile zilizo na ufukwe wa bahari. Nchi hizi ni pamoja na Rwanda (kupitia Rusumo), Burundi (kupitia Kabanga na Manyovu), Zambia (kupitia Tunduma), Malawi (kupitia Kasumulo), Kenya (kupitia Namanga, Sirari na Horohoro) na Uganda (kupitia Mutukula).

Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia Juni, 2012, Makampuni 18 ya mawasiliano yameunganishwa na mkongo wa Taifa. Kati ya makampuni hayo, makampuni 6 ni ya ndani ambayo ni; TTCL, Airtel, Tigo, ZANTEL, Iffinity Communication na Simbanet. Na makumpuni 12 mengine ni za za nchi za jirani

Mheshimiwa Spika, Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umesaidia kupunguza gharama za mawasiliano nchini, na tunatarajia gharama hizo kuendelea kupungua zaidi kadiri muda unavyoenda. Nitatoa mfano wa jinsi gharama zilivyoshuka za huduma za mawasiliano zitolewazo na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ambayo tayari imeunganishwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Mwaka 2009, kabla ya Mkongo, gharama ya huduma za kifurushi cha Broadband cha Giga Byte 2 kwa ajili ya wateja wadogo wadogo ilikuwa ni TSh 100,000. Hivi sasa gharama ya huduma hiyo ni Tsh.30,000, ikiwa ni unafuu wa asilimia 70. Halikadhalika, gharama za huduma za kifurushi cha Broadband cha Giga Byte 40 kwa makampuni ilikuwa Tsh.1,000,000 mwaka 2009 wakati hivi sasa ni Tsh. 360,000 ambayo ni nafuu kwa asilimia 64. Aidh, gharama kwa huduma ya Dedicated 2 Mega Bits per second (2Mbps) ilikuwa Tsh.12,400,000 mwaka 2009 wakati hivi sasa ni Tsh.3,620,000 ikiwa ni nafuu kwa asilimia 71.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kusafirisha mawasiliano kwa masafa marefu (mkoa moja hadi mwingine) gharama zimeshuka kwa zaidi ya asilimia 98. Kwa mfano, kabla ya kuanza kutumia Mkongo, gharama ya kusafirisha mawasiliano ya kasi ya 2 Mega bits per second (2Mbps) kwa umbali wa Kilomita 451 hadi 500 ilikuwa Dola za Kimarekani 9,410 kwa mwezi wakati hivi sasa ni Dola za Kimarekani 158.7 kwa mwezi ikiwa ni nafuu kwa asilimia 98. Kwa upande wa simu za mkononi, gharama zimepungua kutoka TSh 147 kwa dakika mwaka 2009 hadi kufikia TSh 93 kwa dakika mwaka 2010 na TSh 51 kwa dakika mwaka 2011.

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCAF
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za Serikali kupeleka huduma za mawasiliano hadi vijijini, Serikali imeanzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCAF). Utafiti wa awali umefanyika ambao umebaini maeneo 239 yenye uhitaji mkubwa wa mawasiliano ambayo Mfuko utaanza kuyapatia ufumbuzi. Aidha, mwezi Julai 2011 Mfuko ulipokea taarifa za maeneo ya vijiji 2,175 yasiyo na mawasiliano kutoka kwa waheshimiwa Wabunge. Taarifa hizi zimetoa tathmini halisi ya maeneo yasiyo na mawasiliano. Katika hatua ya awali, Mfuko umepeleka taarifa hizi kwa watoa huduma za mawasiliano ili waweze kuboresha mawasiliano katika maeneo yaliyoainishwa. Mshauri mwelekezi anazifanyia kazi taarifa hizi ili kupata njia bora ya kuwashirikisha watoa huduma za mawasiliano kushiriki kwa ufanisi katika kupeleka mawasiliano katika maeneo hayo.

Mabadiliko ya Teknolojia ya Utangazaji kutoka Analojia kwenda Dijitali
Mheshimiwa Spika, Umoja wa Mawasiliano Duniani (ITU) umeazimia kusitisha matumizi ya teknolojia ya utangazaji ya analojia ifikapo tarehe 7 Juni, 2015 ili kuhakikisha kuwa teknolojia pekee itakayotumika kwa utangazaji ulimwenguni kote ni ile ya dijitali. Aidha, kufuatia uamuzi huo, nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimeamua kusitisha matumizi ya teknolojia ya analojia ifikapo Desemba mwaka 2012.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Tanzania, maandalizi yote muhimu ya kuwezesha mabadiliko haya ya teknolojia yanaendelea. Baadhi ya mambo yaliyokwisha fanyika na yanayoendelea kufanyika ni pamoja na: kufanya mapitio na kuboresha sheria ambapo uandaaji wa kanuni za sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010 inayotambua mabadiliko hayo ulikamilika mwezi Desemba, 2011. Hadi sasa, kampuni tatu (3) za Agape Associates Limited, Basic Transmissions Limited na Star Media (T) Limited zimepewa leseni na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kurusha matangazo ya televisheni katika mfumo wa dijitali. Aidha, ili kuwezesha wananchi wote wanaotumia televisheni kumudu mabadiliko haya, Serikali katika mwaka wa fedha 2012/13 imeondoa kodi kwenye ving’amuzi.

Mheshimiwa Spika, mikoa ambayo tayari imefikiwa na matangazo ya dijitali ni pamoja na Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya, Arusha, Tanga, Kilimanjaro na Dodoma. Kampuni zilizopewa leseni, zinaendelea kupeleka huduma hii katika mikoa mengine nchini, chink ya uratibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ambapo moja ya kigezo ni kuhakikisha kuwa mitambo inayowekwa inakidhi viwango vya ubora. Katika kipindi hichi cha mpito kabla ya Desemba 2012, matangazo ya televisheni yataendelea kutolewa kwa mifumo yote yaani analojia na dijitali.

Anuani za Makazi na Simbo za Posta
Mheshimiwa Spika, Tanzania imeanza kutekeleza mfumo mpya wa Anuani za Makazi na Simbo za Posta. Utekelezaji huo ulianza katika kata 8 za Manispaa ya Arusha ambapo uzinduzi rasmi ulifanyika mwezi Januari 2010. Aidha, utekelezaji pia umefanywa katika kata 7 za Manispaa ya Dodoma. Uzinduzi wa utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi kwa jiji la Dar es Salaam ulifanywa mwezi Novemba 2011 na juhudi zinafanywa kupata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mfumo huu katika jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, ninapenda kulijulisha rasmi Bunge lako Tukufu kuwa Tanzania imepewa heshima kubwa katika suala hili na Umoja wa Posta Duniani ambapo Mhe. Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka (Mb.), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameteuliwa kuwa Balozi Maalum wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Simbo za Posta. Hii inatokana na juhudi kubwa ambazo amekuwa akizifanya katika kuhakikisha kuwa kila mtu ulimwenguni anakuwa na anuani kamili tangu wakati akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi (UN Habitat). 

Mheshimiwa Spika, Utekelezaji wa mfumo wa Anuani za Makazi na Simbo za Posta unafanywa kwa pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Wizara kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imeendelea na utoaji wa elimu kwa wadau mbalimbali. 

Uanzishwaji wa Tume ya Taifa ya TEHAMA
Mheshimiwa Spika, mwezi Juni, 2012, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia imeridhia kuundwa kwa Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT Commission). Uanzishaji wa Tume hii ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2003 inayoelekeza kuundwa kwa chombo mahsusi kitakachoratibu masuala ya TEHAMA. Pamoja na masuala mengine, Tume hii itasimamia na kuratibu maendeleo ya Tehama nchini.

Mradi wa “Video Conferencing”
Mheshimiwa Spika, Huduma hii ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu Serikalini kwa kupunguza gharama. Kwa kutumia teknolojia hii, viongozi/watendaji na wataalam wanaweza kufanya kazi zao kwa kushirikiana na kuwasiliana na wadau wengine wakiwa katika sehemu zao za kazi bila ya kulazimika kusafiri kutoka sehemu zao za kazi na kwenda sehemu zingine na hivyo kupunguza gharama za usafiri, na pia kutopoteza muda wa kusafiri kwenda katika sehemu hizo. Vifaa vya huduma hiyo zinakamilishwa kufunga kwenye ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha na ofisi zote za Maafisa Tawala wa Mikoa hapa nchini. Huduma hii itanza kutumika rasmi kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inasimamia utekelezaji wa Sheria na Kanuni mbalimbali za Mawasiliano ili kuhakikisha kuwa watumiaji wa huduma za Mawasiliano wanapata huduma bora. Ili kufanikisha hili Mamlaka pia inahakikisha kuwa wananchi wanafahamu utaratibu wa kuwasilisha malalamiko yao. Elimu hii hutolewa kupitia semina mbalimbali, vyombo vya habari na machapisho.

Kampuni ya Simu Tanzania
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali imelipa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kiasi cha TSh. 1,774,800,000 na hivyo kumaliza deni la Serikali kwa TTCL kufuatia huduma zilizotolewa na Kampuni hiyo kwa Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali. 

Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, TTCL imeanza kufanya majadiliano na Kampuni ya NEC Corporation ya Japan ili kuingia ushirikiano wa kibiashara kwa lengo la kufikisha mawasiliano kwa watumiaji wa mwisho (last mile connectivity). 

Shirika la Posta Tanzania
Mheshimiwa Spika, Shirika la Posta Tanzania (TPC) limeendelea kuimarika kiutendaji na kiufanisi katika kutoa huduma za kiposta nchini na kimataifa. Tathmini iliyofanywa na Umoja wa Posta Duniani (UPU) mwaka jana kuhusiana na ubora wa huduma imelipa Shirika la Posta cheti cha “Bronze”. Shirika la Post ni moja ya mashirika na makampuni sita (6) Afrika yaliyotunukiwa vyeti hivyo ambavyo vitatolewa kwenye Mkutano wa Umoja huo, Doha Qatar mwezi Oktaba, 2012.

Sayansi na Teknolojia

Mheshimiwa Spika, Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ni moja ya eneo muhimu katika kujenga uchumi imara uliojikita kwenye misingi ya maarifa ambapo Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia imepewa dhamana ya kuiendeleza. Kwa kuzingatia dhamana hii, Wizara imejikita katika kutekeleza masuala kadhaa ya ujumla yanayolenga kujenga uwezo na mazingira mazuri ya kuendeleza matumizi ya sayansi na teknolojia na kuchochea ubunifu ikizingatiwa kuwa eneo hili ni mtambuka.

Mheshimiwa Spika, katika sekta hii, masuala yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na; kuweka mifumo ya utekelezaji na udhibiti, kuandaa sera, mikakati, sheria na kanuni; kujenga miundombinu na kuendeleza utafiti; na kujenga na kusimamia taasisi za udhibiti na taasisi za kuendeleza sayansi na teknolojia, hususan rasilimali watu. Baadhi ya haya nitayatolea maelezo katika hotuba hii.

Kutenga asilimia 1.0 ya pato ghafi la Taifa (GDP) kwa ajili ya utafiti na maendeleo(R&D)

Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kutenga asilimia 1.0 ya pato ghafi la Taifa (GDP) kwa ajili ya utafiti na maendeleo. Katika mwaka wa fedha 2011/2012 Serikali ilitenga jumla ya shilingi 25,768,769,000 kwa ajili ya kuendeleza shughuli za utafiti na maendeleo, maeneo yaliyofaidika na fedha hizi ni: (i) Kujenga uwezo wa watafiti; (ii) kukarabati miundombinu ya utafiti; (iii) kugharimia utafiti; (iv) kuhawilisha teknolojia; na (v) kufanya usimamizi na utawala, hususan ufuatiliaji na tathmini ya shughuli zilizofadhiliwa na fedha za utafiti.

Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia Desemba 2011 Tume ya Sayansi na Teknolojia ulikuwa unagharimia mafunzo ya wataalamu 195 katika ngazi ya Shahada ya Uzamili (MSc) na 100 katika Uzamivu (PhD) kwenye Vyuo Vikuu 5.

Kuishirikisha sekta binafsi katika kuchangia maendeleo na matumizi ya teknolojia kwenye uzalishaji mali na utoaji huduma
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Sheria ya Public Private Partnership ya mwaka 2010 pamoja na kanuni zake za mwaka 2011. Kwa mfano, kupitia ushirikiano baina ya sekta binafsi na Serikali, muungano wa kampuni tatu za watoa huduma za mawasiliano (Airtel, Tigo na Zantel) wameweza kujenga na kukamilisha njia za mkongo wa mawasiliano katika Jiji la Dar es Salaam (metro networks) na hivyo kuongeza fursa za kutoa huduma bora zaidi za mawasiliano. 

Mheshimiwa Spika, Tanzania Private Sector Foundation imechangia maendeleo ya Teknolojia kwenye Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Mbeya kwa kutoa vifaa vya maabara. Majadiliano yanaendelea kati ya HUAWEI na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela.

Kuandaa Programu Mahsusi ya wataalamu wa kada mbalimbali za sayansi na teknolojia katika kuyafikia malengo ya dira
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2011/2012, Serikali kupitia Wizara hii imeendelea kupanua Taasisi zinazotoa mafunzo katika fani mbalimbali za sayansi na teknolojia. 

MASUALA YA UJUMLA KATIKA WIZARA

Uendelezaji wa Rasilimali Watu

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kusimamia sheria, kanuni na taratibu na kuendeleza Rasilimali watu, watumishi 20 wa kada mbalimbali wamepandishwa vyeo baada ya kukidhi vigezo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuhamasisha watumishi kujikinga na kuepuka maambukizi mapya ya UKIMWI, matumizi ya dawa za kurefusha maisha kwa waishio na virusi vya UKIMWI na kupunguza maambukizi mapya ya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma
Mheshimiwa Spika, ukaguzi wa matumizi ya fedha za Wizara na Taasisi zilizo chini yake umeendelea kufanywa kwa lengo la kuongeza ufanisi, matokeo mazuri na tija kwa Taifa. Taarifa za ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na pia Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi katika Sekta ya Umma (PPRA) umethibitisha hilo. 

Sera na Miongozo Mbalimbali Katika Sekta
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea na jukumu lake la uandaaji wa Sera mbalimbali na Utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha 2010-2015. Aidha, Wizara imehuisha Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia (Communication, Science and Technology Strategic Plan).

Umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi katika Sekta ya Mawasiliano
Mheshimiwa Spika, umuhimu wa sensa ya watu na makazi katika sekta ya mawasiliano ni jambo lililo dhahiri lisilohitaji ufafanuzi wa ziada kwa sababu huwezi kupanga kwa usahihi jinsi ya kuimarisha miundombinu ya mawasiliano bila kujua idadi ya watu na mtawanyiko wao. Kwa hivyo Wizara inatoa wito wa kipekee kwa watanzania wote kujitokeza kuhesabiwa na kutoa taarifa sahihi.

TAASISI ZA MAFUNZO
 
Taasisi ya Sayani na Teknolojia ya Mbeya
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia upandishwaji hadhi wa Taasisi ya Sayani na Teknolojia ya Mbeya kuwa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia. Tayari Taasisi imeshapata ithibati ya muda kwa ajili ya kuendesha programu zake kama Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya. Aidha, imekamilisha ujenzi wa mabweni mawili ya wanafunzi yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 800. Pia, taasisi inaendelea kukarabati na kuboresha vyumba vitakavyotumika kama maabara za kufundishia.

Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Teknolojia Mbeya (MIST) imeendelea na upanuzi wa udahili na uanzishaji wa Programu mpya kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Katika mwaka wa masomo wa 2011/2012 Taasisi imefikisha jumla 2,591, ikilinganishwa na wanafunzi 1,757 kwa mwaka wa masomo 2010/2011.
Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT)
Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imeendelea na upanuzi wa udahili na uanzishaji wa Programu mpya kwa ajili ya kukidhi mahitaji na maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Katika mwaka wa masomo wa 2011/2012 Taasisi ilikuwa na jumla ya wanafunzi 2,583 ikilinganishwa na wanafunzi 1,578 katika mwaka wa masomo 2010/2011. Aidha, imeendelea na ujenzi wa DIT Teaching Tower na usimamizi wa kituo Mahiri cha TEHAMA. 

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, inaendelea kuimarisha Kampasi mpya ya Mwanza ijulikanayo kama Tanzania Institute of Leather Technology (TILT), kampasi hii inaendelea kutoa Programme za muda mfupi kwa wajasiriamali wa kusindika na kutengeneza bidhaa za ngozi. Lengo ni kuendesha Programu za muda mrefu. 

Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela

Mheshimiwa Spika, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa
Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Ilifanya udahili kwa mara ya kwanza mwezi Oktoba 2011, ambapo wanafunzi 83 walianza masomo. Kati ya wanafunzi hao 83, wanawake 15 na wanaume 78. Aidha, kati ya wanafunzi hao, wanafunzi 53 wamedahiliwa katika masomo ya shahada ya uzamili na wanafunzi 30 wamedahiliwa katika masomo ya shahada ya uzamivu. Aidha, taratibu za kuzindua rasmi Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Nelson Mandela zinaendelea kufanywa na inatarajiwa kuwa Taasisi hii itazinduliwa rasmi mwezi Oktoba 2012.

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia

Mheshimiwa Spika, Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ni chombo cha kusimamia na kuratibu tafiti za Sayansi na Teknolojia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika kuhakikisha shughuli za Tume ya Sayansi na Teknolojia zinatekelezwa vyema Tanzania Bara na Tanzania Visiwani, Tume hiyo imefungua ofisi yake mjini Zanzibar. Baadhi ya majukumu ya Tume katika uendelezaji wa sayansi na teknolojia ni katika maeneo ya uboreshaji wa miundombinu ya utafiti na vitendea kazi katika taasisi za utafiti na maendeleo. Aidha, Tume imejielekeza katika uhamasishaji wa matumizi ya matokeo ya utafiti na uhawilishaji wa teknolojia kwa wajasiriamali.

Uhamasishaji wa matumizi ya matokeo ya utafiti na uhawilishaji wa teknolojia kwa wajasiriamali.

Mheshimiwa Spika, Wizara, kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia, ilitoa kiasi cha Tsh. 80,000,000 kwa ajili ya shughuli za Atamizi ya TEHAMA ya Dar es Salaam (DTB), ambapo wadau wengine ni INFODEV (World Bank) na Vodacom Tanzania. Atamizi hiyo imeweza kuhudumia wajasiriamali ambao wameweza kuendeleza juhudi zao za ujasiriamali katika nyanja za TEHAMA ikiwa ni pamoja na kupatia ufumbuzi wa masuala ya ununuzi wa bidhaa kwa mtandao n.k. Aidha, kwa kutambua umuhimu wa shughuli za ugunduzi na ubunifu, jumla ya Tsh.134,894,950 zimetumika kwa ajili ya kuwahudumia wagunduzi na wabunifu kwa kuwapatia tuzo na vitendea kazi ili kuboresha shughuli zao. Pia Wizara kupitia Tume ilitoa kiasi cha Tsh. Million 500 kutoka Mfuko wa Ubunifu kwa ajili ya kubiasharisha teknolojia zilizopo kwenye kongano (clusters) za taasisi za TEMDO na Mzinga.

Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzani
Mheshimiwa Spika, Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imepewa dhamana ya kusimamia na kuendeleza matumizi salama ya nguvu za atomiki, eneo hili ni muhimu sana katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Miongoni mwa shughuli zilizotekelezwa na Tume hii ni pamoja na kuendeleza na kudhibiti matumizi salama ya nguvu za atomiki.

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imekuwa ikishiriki katika kuandaa mipango na taratibu za kuendeleza na kusimamia matumizi ya nguvu za atomiki hapa Tanzania. Kwa upande wa udhibiti, Tume imekuwa mstari wa mbele katika kusimamia matumizi salama ya mionzi katika hospitali, vituo vya huduma za afya, viwandani, kwenye migodi na shughuli za tafiti mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, juhudi za kuendeleza matumizi salama ya nguvu za atomiki zimehakikisha kuwa matumizi ya nguvu za atomiki zinaboresha maisha ya wananchi wa Tanzania ikiwa ni pamoja na: (i) utoaji wa huduma za tiba ya saratani, (ii) uboreshaji wa mazao ya kilimo na mifugo, (iii) kutokomeza mbung’o katika visiwa vya Unguja na Pemba, (iv) kusimamia na kukagua uwepo wa mionzi kwenye vyakula na pembejeo za kilimo n.k. Katika kuhakikisha kuwa shughuli za usimamizi wa matumizi ya nguvu za atomiki zinafanywa vyema zaidi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume imefungua ofisi yake mjini Zanzibar hivi karibuni.

Uchimbaji wa Madini ya Urani
Mheshimiwa Spika, kiwango kikubwa cha madini ya Urani kimegundulika hapa Tanzania na hasa katika maeneo ya Namtumbo, Bahi na Manyoni. Juhudi kubwa zimeelekezwa katika kuhakikisha kuwa uchimbaji utakapoanza, masuala ya usalama wa wananchi na madini hayo unapewa kipaumbele kikubwa.

CHANGAMOTO ZILIZOJITOKEZA WAKATI WA UTEKELEZAJI WA MIPANGO YA WIZARA KWA MWAKA 2011/12
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, Wizara imekabiliwa na changamoto kadhaa ambazo zilichangia katika kutofikiwa malengo kulingana na mpango. Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na:

(i) Uhaba wa wataalamu wa kutosha katika nyanja mbalimbali za Sayansi, 
Teknolojia na Ubunifu,
 (ii) Kuongeza uelewa wa umuhimu wa Sayansi na Teknolojia ili kuendana na dhana ya kuwa na jamii inayoongozwa na maarifa,
(iii) Uhaba wa miundombinu ya kuendeleza sekta ya Mawasiliano Sayansi na Teknolojia,

 (iv) Kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu na manufaa ya Mkongo kwa jamii, unachangia katika uharibifu wa nyaya za Mkongo unaofanywa na wananchi katika baadhi ya maeneo. 

 (v) Shughuli za Utafiti na Maendeleo (Research and Development – R&D) kutotengewa fedha za kutosha: Serikali kwa kutambua tatizo hili, imeendelea kutenga fedha kulingana na uwezo wake. Katika kutimiza azma hii, Serikali katika Bajeti yake ya Mwaka wa Fedha wa 2011/2012 ilitenga Sh. 25,768,769,000 kwa ajili ya shughuli za utafiti. 


MALENGO YA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/13
 ​Mawasiliano

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Wizara itatekeleza yafuatayo:
(i) Itakamilisha mchakato wa kuanzisha Tume ya TEHAMA,
(ii) Itaratibu utekelezaji wa Mradi wa Kitaifa wa Anuani za Makazi na Simbo za Posta,
 (iii) Itaratibu utekelezaji wa mabadiliko ya Teknolojia ya utangazaji kutoka Analojia kwenda dijitali hadi ifikapo Desemba 2012,
(iv) Itaratibu na kusimamia utendaji kazi wa Kampuni ya Simu (TTCL), Shirika la Posta Tanzania (TPC), Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCAF),
(v) ​Itaratibu Ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kufikisha huduma zake hadi Wilaya zote nchini pamoja na kuunganisha Taasisi zote za Umma kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano,
(vi) Itaratibu mradi wa kuunganisha katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, shule za msingi, sekondari, shule/vyuo vya afya pamoja na taasisi zilizoainishwa kwenye mradi wa Tanzania Beyond Tomorrow,
 (vii) Itaratibu uwekaji wa viwango vya mifumo, vifaa, mitambo na huduma za TEHAMA nchini na kuandaa mwongozo kuhusu usalama wa mitandao ya TEHAMA.

Sayansi, Teknolojia na Ubunifu

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Sayansi na Teknolojia, Wizara itatekeleza mambo yafuatayo:
(i) Kuratibu mahusiano ya kikanda na kimataifa katika masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu,
(ii) Itakamilisha Andiko la Programu ya Matumizi ya Teknolojia za Nyuklia,
(iii) Itaratibu utekelezaji wa Programu ya Mageuzi ya Sayansi, Tekonolojia na Ubunifu,

MASUALA YA UJUMLA
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Wizara itatekeleza mambo yafuatayo:
(i) Itawapandisha vyeo watumishi 11 wenye sifa,
(ii) Itawapeleka kwenye mafunzo watumishi kumi na sita (16) katika maeneo ya Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano,
(iii) Itaendelea kusimamia na kuimarisha Sekta ya TEHAMA, Sayansi na Teknolojia,
(iv) Itaendelea kusimamia miongozo ya Serikali inayohusu matumizi sahihi ya Fedha na Mali zote za serikali.
(v) Itaratibu uandaaji na uhuishaji wa Sera na Sheria mbalimbali zinazosimamiwa naWizara,
 (vi) Itaendelea kusimamia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Wizara wa Miaka Mitano (2012/2013-2016/2017),

 USIMAMIZI WA TAASISI ZILIZO CHINI YA WIZARA

 Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam

 Mheshimiwa Spika, Wizara itatekeleza yafuatayo kupitia Taasisi Teknolojia Dar esSalaam:
(i) Itadahili wanafunzi 1,505 katika programu mbalimbali,
 (ii) Itaanza kufundisha kozi mpya ya Shahada ya Uzamili ya Uhandisi (Master of Engineering in Maintenance Management),
(iii) Itaanzisha mradi wa majaribio wa Matibabu Mtandao (Telemedicine) utakaounganisha DIT, Hospitali za Muhimbili, Amana, Temeke, Mwananyamala, Tumbi na Bagamoyo, na
(iv) Itaendelea na ukarabati wa majengo na miundombinu ya Kampasi ya Mwanza (kilichokuwa Chuo cha Ngozi Mwanza)

Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Mbeya
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Mbeya itatekeleza mambo yafuatayo:
(i) Itaongeza udahili wa wanafunzi kutoka wanafunzi 2,591 hadi kufikia wanafunzi 3,000, ikiwa ni ongezeko la asilimia 16,
(ii) Itaendelea na ujenzi wa jengo la maktaba litakalokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,500 kwa wakati mmoja,
(iii) Itaendelea na ujenzi wa jengo la maabara ili kukabiliana na uhaba wa vyumba vya maabara katika Taasisi.

Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Taasisi ya Nelson Mandela itatekeleza mambo yafuatayo:
(i) Itadahili wanafunzi wapatao 100 katika ngazi za uzamili za uzamivu kwa mwaka 2012/2013,
(ii) Itajenga Kituo cha TEHAMA,
(iii) Itanunua vifaa vya kujifunzia na kufundishia, na
(iv) Itakamilisha uandaaji wa Mpango wa Matumizi ya Ardhi (Land Use Plan) wa eneo la Taasisi lililopo Karangai.

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Tume ya Sayansi na Teknolojia itatekeleza mambo yafuatayo:
(i) Itaendelea kuratibu shughuli za utafiti nchini,
(ii) Itaendelea na kuratibu shughuli za uhawilishaji wa teknolojia mbalimbali nchini,
(iii) Itaanzisha atamizi ya biashara na kilimo (Agri-business Incubator) ili kukuza ujasiliamali katika sekta ya kilimo, hususan usindikaji wa mazao,
(iv) Itasimamia ujenzi wa kijiji cha kisasa cha mawasiliano ICT Technology Park ambacho kitachangia sana katika kuleta makampuni makubwa ya kimataifa na hatimaye kuweza kukuza uchumi wa maarifa (knowledge economy).

Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania itatekeleza mambo yafuatayo:
(i) Itaendeleza zoezi la upimaji wa viwango vya mionzi kwa wafanyakazi 1,300wanafunzi 83 wanaotumia vifaa vya mionzi katika vituo mbalimbali (Personnel Dosimetry Service),
 (ii) Itatoa elimu kwa wananchi waishio maeneo yenye madini ya Urani kwa nia ya kuongeza uelewa na kuweka tahadhari pale panapostahili,
(iii) Itaanzisha Ofisi ya kanda katika mkoa wa Ruvuma (Namtumbo) ili kusogeza huduma ya kupima mionzi karibu na migodi ya urani.

Shirika la Posta Tanzania
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2012/2013, Shirika la Posta Tanzania litatekeleza mambo yafuatayo:

 (i) Litaendeleza, kuongeza na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika huduma zitolewazo na Shirika ikiwa ni pamoja na kuunganisha ofisi za Posta za Mikoa na Wilaya katika Mtandao wa Ki-Elektroniki wa Posta kutoka ofisi 65 za sasa hadi 95;

(ii) Litafanyia matengenezo katika majengo mbalimbali nchini.


Kampuni ya Simu Tanzania
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Kampuni ya Simu litatekeleza mambo yafuatayo:
(i) Kuongeza tija na ufanisi wa Kampuni kwa kuboresha mapato kutoka Sh. 89 bilioni mwaka 2011 hadi Sh. bilioni 110 mwaka 2012,
 (ii) Itapanua Mtandao wa intaneti (Fixed and Wireless Broadband Services) kwenye miji mikubwa 8 Tanzania bara na visiwani kwa kuongeza vituo vya mitambo (BTS). 

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania utatekeleza mambo yafuatayo:
(i) Itaendelea na kuratibu utekelezaji wa mfumo mpya wa utangazaji wa digitali (Digital Broadcasting) kwa kutoa elimu kwa umma na watoa huduma za mawasiliano kulingana na kanuni na Sheria husika;
(ii) Itaendelea kusimamia na kudhibiti ubora wa huduma za mawasiliano kwa kufanyia kazi ukaguzi makampuni yaliyosajiliwa ili kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa zinakidhi viwango vilivyowekwa kwenye leseni zao.

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013 Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCAF) utatekeleza mambo yafuatayo:
 (i) Utasimamia utekelezaji wa makubaliano na watoa huduma za mawasiliano ya kupeleka huduma katika maeneo yaliyoainishwa kulingana na mikataba baina ya pande hizi mbili,
(ii) Utaendelea kutathmini mahitaji ya huduma za mawasiliano katika maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara na kuanzisha miradi itakayohakikisha mawasiliano yanafika kwenye maeneo hayo.


MAAZIMIO NA MWELEKEO WA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/13

Malengo katika mpango wa muda wa kati na mrefu

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine kutoka sekta ya umma na sekta binafsi inaazimia kutekeleza Mpango wa Muda wa Kati na Muda Mrefu ambao umetilia mkazo katika maeneo yafuatayo:

 MAWASILIANO

 (i) Kukamilisha mabadiliko ya mfumo wa utangazaji, kutoka Analojia kwenda Dijitali,
 (ii) Kutekeleza Mfumo wa Anuani za Makazi na Simbo za Posta (Physical Addressing and Post Code System),
(iii) Kuimarisha usimamizi wa masuala ya mawasiliano na haki za watumiaji wa huduma;
(iv) Kuboresha utoaji wa huduma za simu hadi katika sehemu zisizo na mvuto wa kibiashara,
(v) Kuendeleza ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (The National ICT broadband Backbone Infrastructure) katika awamu ya III.

 SAYANSI NA TEKNOLOJIA NA UBUNIFU

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, Wizara imeazimia kutekeleza yafuatayo:
(i) Kuratibu utekelezaji wa Programu ya Mageuzi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu,
 (ii) Kuratibu uboreshaji na upanuaji wa taasisi za sayansi na teknolojia nchini na
 (iii) Kuweka na kusimamia utaratibu wa usajili na kulinda haki miliki za matokeo ya ubunifu kwa watafiti na wagunduzi

SHUKRANI
Mheshimiwa Spika, naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa nchi rafiki, mashirika ya kimataifa, na taasisi za fedha kwa misaada yao ambayo imeiwezesha Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kutekeleza baadhi ya malengo yake muhimu. Wahisani hao ni pamoja na Serikali za Marekani, Sweden, Norway, Finland, Uholanzi, Japan, Italia, Afrika Kusini, Jamhuri ya Korea, China na India. Mashirika wahisani ni pamoja na Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Madola, Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki, KOICA, UNESCO, UNCTAD, UPU na ITU. Mashirika ya fedha ni pamoja na Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika pamoja na Benki ya Exim ya China. Aidha, naishukuru sana sekta binafsi kwa mchango wao katika kuendeleza sekta ya mawasiliano, sayansi na teknolojia.
MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
Mheshimiwa spika, makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia katika mwaka wa fedha 2012/13 yamekadiriwa kuwa sh. 70,107,712,000. 

Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kutekeleza mipango yake iliyojiwekea katika mwaka wa wa fedha 2012/13, sasa naliomba bunge lako tukufu lipokee, lijadili na kuidhinisha matumizi ya jumla ya Sh 70,107,712,000 kwa mchanganuo ulioelezwa.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa napenda kukushukuru wewe binafsi, Naibu Spika, Wenyeviti wa Kamati za Bunge pamoja na Bunge lako Tukufu kwa kunisikiliza wakati nikiwasilisha Hotuba yangu. Hotuba hii itapatikana pia katika tovuti ya Wizara ambayo ni  www.mst.go.tz

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

1 comment:

Anonymous said...

Hey there! I know this is kinda off topic but I was wondering which blog platform are
you using for this website? I'm getting fed up of Wordpress because I've
had problems with hackers and I'm looking at alternatives for another platform. I would be great if you could point me in the direction of a good platform.
Look into my web blog free conferencing