SERIKALI YAINGILIA KATI KUOKOA MAISHA YA WAGONJWA...


Juhudi zaidi zimechukuliwa na serikali ambapo sasa itatumia pia hospitali binafsi za TMJ, Regency, Aga Khan, Hindu Mandal, CCBRT na Hospitali ya Jeshi Lugalo.
Aidha, nguvu zimeongezwa katika hospitali za Mwananyamala, Amana na Temeke za Dar es Salaam kunakodaiwa hakuna mgomo, ili kutotoa rufaa nyingi kwa wagonjwa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kunakodaiwa kuwa na mgomo. 
Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja alilsema ofisini kwake kuwa, utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu kuhusu kutumia hospitali za Jeshi na madaktari wastaafu limeanza na sasa nguvu imeongezwa kwa kuhusisha hospitali binafsi.
“Pamoja na Lugalo kuwa tayari, tulikuwa katika mazungumzo na hospitali za binafsi ikiwa ni juhudi hizo hizo za Serikali, hospitali kadhaa zimeshakubali ambazo ni CCBRT, Aga Khan, Hindu Mandal, Regency na TMJ na tunaendelea kuzungumza na nyingine,” alisema Mwamwaja.
Pamoja na hilo, Mwamwaja alisema nguvu kubwa pia imeelekezwa katika hospitali za Mwananyamala, Temeke na Amana kuhakikisha kuwa wagonjwa wanatibiwa kikamilifu.
Akifafanua kuhusu namna ya wagonjwa watakavyotibiwa katika hospitali hizo za binafsi, Mwamwaja alisema;” Kutakuwa na fomu maalumu ambayo daktari wa Amana, Mwananyamala au Temeke atakayeona mgonjwa anahitaji tiba zaidi, atamjazia ili apokewe ama kupelekwa katika hospitali hizo”.
Pia alisema wagonjwa watakaohitaji rufaa, kwa utaratibu huo huo, watatibiwa katika Hospitali ya Jeshi la Lugalo ambayo imekuwa tayari muda mrefu ikishirikiana na hospitali nyingine chini yake. 
Alisema mgomo wa awali madaktari walipelekwa Muhimbili kutoa huduma, lakini baadhi ya madaktari wenyeji mgomo wa awali walidaiwa kuwakwamisha makusudi kufanya huduma na Serikali ililiona hivyo na kuona ni bora wagonjwa wapelekwe huko ili kupata tiba vizuri zaidi.
Alisema madaktari wastaafu na wa Wizara kama alivyosema Waziri Mkuu Pinda, ndio watakaohusika Muhimbili. Pinda alieleza hayo bungeni akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliyetaka kujua hatua za Serikali kukabili mgomo huo.
Mlinzi wa MOI ambaye hakufahamika jina, aliwaeleza waandishi kuwa, amepewa agizo kuwa mwandishi yeyote asiingie kupata taarifa za mgomo au za Dk Steven Ulimboka.
Mmoja wa wagonjwa Lydia Rwechungura kutoka Chamwino, Dodoma, akiwa nje ya lango la MOI alisema, alifika hospitalini hapo Juni 25 mwaka huu baada ya kupewa rufaa ya Hospitali ya Mkoa Dodoma na sasa hajui afanyeje.
“Pingili za uti wa mgongo zinasigana, nilikuja wakaniambia nije ili nianze mazoezi, nimeingia humo ndani, mapokezi wameniambia niondoke maana hakuna huduma. Eti niangalie vyombo vya habari mgomo ukiisha ndio nije, sijui niende wapi, kwa nini madaktari hawana huruma jamani,” alisema Rwechungura huku akilia.
Eneo la Hospitali ya Muhimbili tofauti na siku nyingine,  lilikuwa kimya, hakukuwa na pilikapilika za wagonjwa wala wahudumu na baadhi ya wagonjwa walionekana kuingia na kutoka huku wengine wakisikitika kwa kuelezwa kuwa hakuna huduma.
Simu za Jumaa Almasi, Ofisa Uhusiano wa MOI ziliita bila majibu na Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, Aminiel Aligaeshi alikataa kuzungumza na waandishi akidai hajui kama mgomo upo au haupo. Alipotafutwa simu haikuwa hewani.
Wakati hali ya huduma ikizorota Muhimbili, Mkoa Mwanza madaktari 63 waliopo kwenye mafunzo kwa vitendo kazini katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando na ya Sekou Toure wametimuliwa kutokana na mgomo na kurejeshwa wizarani.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Dk. Charles Majinge alisema inawarejesha wizarani madaktari 47 baada ya kukataa kurejea kazini.
“Hospitali ya Bugando ina jumla ya madaktari 47 walio katika mafunzo kazini ambao tumewarudisha wizarani wamegoma kurejea katika mafunzo kazini, na sasa kwa kuwa walitoka wizarani kuja hapa kwetu kwenye mafunzo, basi tunawarejesha huko walikotoka,” alisema Dk. Majinge.
Alisema kuwa kuondoka kwa madaktari hao, waliokuwa katika mgomo kutaathiri utendaji wa utoaji huduma, kwa muda mpaka baadaye watakapojipanga na kupata ufumbuzi wa kudumu. 
Kwa upande wa Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure, madaktari 16 waliopo kwenye mafunzo kazini wamesimamishwa pia kwa agizo la Wizara ambao waliamuliwa kuchukua barua zao na kuondoka katika eneo la Hospitali ya Sekou Toure.
Mganga Mkuu wa Mkoa, Valentine Bhangi akielezea kutimuliwa kwa madaktari hao alisema kwa vile madaktari hao waliletwa na wizara hapo kwa ajili ya mafunzo kazini, wamerejeshwa huko walikotoka kwa hatua zaidi.
Madaktari katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma wameingia kwenye mgomo baridi hali ambayo inasababisha wagonjwa kutopata huduma kwa wakati huku wengine wakitaka Serikali itazame hatima ya wananchi wa kipato cha chini ambao hawana uwezo wa kwenda hospitali za kulipia.
Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk Ezekiel Mpuya alisema kuwa hakuna mgomo hospitalini hapo na wanaendelea na kazi kama kawaida.
Hospitalini hapo kulikuwa na msululu mrefu  wa wagonjwa wakiwa kwenye foleni ya kumuona daktari ambapo ni daktari  moja tu alikuwa akitoa huduma huku vyumba vingine vya madaktari vikiwa havitoi huduma yoyote.
Mmoja wa wananchi hao, Zakaria Daudi ambaye ni mkazi wa Chamwino katika Manispaa ya Dodoma alisema kuwa,  hali ya huduma sio nzuri kwani wanalazimika kusubiri kuingia kwa daktari muda mrefu bila ya mafanikio.
“Nimekuwa namleta hapa mke wangu bado hajapata huduma napigwa tu kalenda bila huduma yoyote kama wamegoma waseme ukweli,” alisema.
Kwa upande wake, mkazi wa Nkuhungu, Kunze George alimtaka Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuwa mkweli kuwa kuna mgomo na si kusema hali shwari wakati wananchi wanateseka kwa kukosa huduma.
Wakati huohuo, Chama cha Wauguzi, Tawi la MOI limeiomba Serikali kutatua haraka mgomo huo kwa kuwa wao wanabebeshwa mzigo mkubwa wa huduma na utendaji na wanalaani kitendo hicho.
Mwenyekiti wa chama hicho MOI, Prisca Tarimo alisema kazi kubwa wamekuwa wakiifanya na hivyo wanalazimika kufanya kazi zisizo kuwa zao kuokoa maisha ya watu hivyo Serikali itatue tatizo hilo kwa haraka.
Kuhusiana na afya ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari wanaoongoza mgomo, Dk Steven Ulimboka, Mkuu wa Jopo la Madaktari wanaomtibu daktari huyo, Profesa Joseph Kahamba alibainisha kuwa afya yake inaendelea kuimarika na wanaendelea kumtibu akiwa chini ya uangalizi wao katika kitengo cha wagonjwa mahututi.

No comments: