KUSHOTO: Jermaine Grant akipelekwa mahakamani mjini Nairobi chini ya ulinzi mkali. KULIA: Samantha akiwa na mumewe, Jermain Lindsay ambaye alihusika na milipuko ya London.
'Mjane Mzungu' wa mlipuaji bomu wa London ni mtuhumiwa nambari moja wa shambulio baya la kigaidi nchini Kenya.Samantha Lewthwaite, ambaye mumewe Jermain Lindsay alilipua njia ya treni ya Piccadilly, amekuwa mafichoni tangu Desemba pale polisi walipofichua mpango kamambe wa kulipua hoteli za Magharibi mjini Mombasa.
Maofisa wamesema mama huyo wa watoto watatu kutoka Home Counties alionekana karibu na klabu ya usiku ambayo ni mojawapo ya sehemu zilizolengwa kwenye Hoteli ya Indian Ocean Jumapili usiku.
Bomu lilirushwa ndani ya bustani ya Jericho Beer ambamo kulikuwa na watalii wakitazama mechi kati ya England na Italia, na kuua watu watatu akiwamo kijana mdogo.
Haijafahamika kama Waingereza ni kati ya watu 25 waliojeruhiwa.
Muda mfupi kabla ya shambulio hilo, mwanamke mweupe anayefanana na taarifa za alivyo Samantha alionekana mwenye mashaka na kuuliza maswali kadhaa kuhusu baa hiyo. Alikuwa pamoja na wanaume wawili wenye asili ya Asia.
"Tunashuku Samantha Lewthwaite amehusika kwenye shambulio hili la kigaidi katika klabu," Ofisa wa Polisi wa Kenya amesema.
Mwanamke huyo mwenye miaka 28 ambaye ni mtoto wa askari kutoka Aylesbury mjini Buckinghamshire alishitakiwa Desemba mwaka jana kuandaa mpango wa kuua mamia ya watalii wa Kiingereza mjini Mombasa.
Polisi walikuta silaha na kiwanda cha kutengeneza mabomu katika nyumba yake yenye ulinzi mkali, ambamo pia hupatumia kama benki kwa ajili ya kuhifadhia fedha za magaidi wa Kisomali wa kundi la Al Shabaab.
Samantha aliachiliwa kwa sababu ambazo hazijajulikana na anasemekana aliishi Somalia kama mkimbizi kabla ya kurejea Kenya.
"Polisi wanaamini Samantha amerejea Mombasa na anashiriki kikamilifu kwenye mashambulio ya mabomu ya kutegwa kwa mkono," kilisema chanzo cha ulinzi Kenya.
"Mwanamke mweupe, mwenye kufanana kabisa na taarifa za Samantha, alionekana na wanaume wa Kiarabu wa rika la kati wakiuliza maswali kuhusu baa kabla ya shambulio.
"Hakika si hali ya kawaida kwa mwanamke Mzungu kuwapo hapa na kuvaa mavazi ya Kiislamu."
Watuhumiwa hao watatu pia walionekana jirani na makanisa Katoliki mjini Mombasa.
Samantha ambaye alitimuliwa chuo kikuu amekuwa akiwindwa na CIA, Polisi wa Kenya na Scotland Yard, ambao wametuma askari wa kutosha Nairobi kusaidia uchunguzi.
Kabla ya kukamatwa mwezi Desemba, alikuwa akisafiri Kenya kwa kutumia pasipoti bandia inayomilikiwa na Natalie Faye Webb, nesi wa Essex ambaye hana uhusiano na ugaidi na hajawahi kukanyaga nchi za Afrika Mashariki.
Samantha alizaliwa Ireland ya Kaskazini ambako baba yake, Andrew ambaye alikuwa akitumikia jeshi, alikutana na mama yake, Christine.
Wazazi hao walitengana wakati Samantha akiwa na miaka 11, tukio ambalo marafiki wanasema lilimshawishi kupenda Uislamu, na kuingia rasmi katika dini hiyo akiwa na miaka 15.
Alikutana na mlipuaji wa treni ya King's Cross, Lindsay kwenye chumba cha majadiliano ya Kiislamu wakati akisomea dini hiyo na siasa kwenye Shule ya Oriental and African Studies iliyoko katikati ya London.
Aliolewa na fundi wa kufitisha mazulia mzaliwa wa Jamaica kwenye sherehe za Kiislamu zilizofanyika Aylesbury mwaka 2004.
Wakati mume wake mwenye miaka 19 alipojilipua mwaka 2005 na kukatisha maisha ya watu 26, Samantha alikuwa na ujauzito wa miezi minane wa mtoto wake wa pili, ambaye ni msichana. Tayari alikuwa mtoto wa pili wa kiume ambaye amezaa na mwanaume asiyefahamika mwaka 2009.
Katika familia yake ya mjini Aleysbury, Samantha ni mtoto wa mwisho kati ya watoto watatu, akielezea hawajaonana kwa miaka kadhaa sasa.
Mshirika wake wa tuhuma za kupanga ulipuaji bomu Desemba, Jermaine Grant mwenye miaka 29 kutoka London, yuko mahakamani mjini Mombasa.
Mji wa Bandari na Nairobi imekumbwa na mashambulio ya mabomu tangu vikosi vya Kenya vilipovamia Somalia Oktoba mwaka jana kupambana na wapiganaji wa Kiislamu.
Masaa kashaa kabla ya milipuko ya Jumapili, Ubalozi wa Marekani ulitoa tahadhari kutokea kwa mashambulio ya kujitoa muhanga ndani au kuzunguka Mombasa.
Mkuu wa Polisi, Aggrey Adoli alisema: "Mashambulio yalitokea majira ya Saa 4 usiku, bomu lilitupwa ndani ya baa, lakini wengi kati ya waliojeruhiwa walikuwa nje ya baa kwenye mlango.
"Mmoja kati ya watu waliojeruhiwa anatusaidia kwenye uchunguzi sababu anatoa taarifa za kukanganya. Amekuwa akishikiliwa kama mtuhumiwa."
No comments:
Post a Comment