"Dk. Ulimboka alipopata nguvu alielezea yaliyomkuta alipotekwa jana kuwa ni pamoja na kufungwa kitambaa, kamba mikononi na miguuni na kushushiwa kipigo na baadaye alitupwa porini na kufunikwa na majani. Waliompiga walidhani amekufa hivyo, walimuacha hapo baada ya kupishana wamuue kwa risasi au sindano na kuishia kumtupa porini ambako mwenyewe alijikongoja hadi alipokutana na wasamaria wema na kumuokoa."
Pamoja na hayo hali ya Dk. Ulimboka inaanza kuimarika ambapo leo mchana alianza kuwatambua watu waliomtembelea na kuzungumza huku akilindwa na madaktari nje ya wodi ya wagonjwa mahututi alikolazwa katika Kitengo cha Mifupa cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MOI).
Aidha wakati daktari huyo akipatiwa huduma ya matibabu kupitia jopo la madaktari bingwa, hali ilikuwa tofauti kwa wagonjwa wa kawaida waliofika hospitalini hapo ambao waliishia nje huku wakiambia hakuna huduma kwa kuwa sasa mgomo umeshika kasi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo mchana, Katibu wa Jumuiya hiyo ya Madaktari, Edwin Chitage, alisema madaktari wote nchini wameamua kutokuwa na imani na tume iliyoundwa na Polisi kutokana na mazingira ya tukio lilimpata Dk. Ulimboka.
“Tunaomba kiundwe upya chombo huru kitachokuwa na wajumbe wanaoaminika ambao watachunguza kwa dhati tukio hili na kuja na majibu, hatuna imani na tume hii kwa kuwa mazingira ya kutekwa na kupigwa kwa Dk Ulimboka yanatufanya tusiiamini polisi,” alisisitiza.
Aidha alidai madaktari na hospitali ya Dodoma wamekuwa wakipokea vitisho mbalimbali kwa njia ya simu na kusisitiza kuwa havisaidii kwa kuwa ndio vinazidisha mgogoro huo. “Serikali itambue hakuna njia yeyote ya kutatua mgogoro huu bali ni kwa njia ya kuzungumza kwa dhati,”
Alisema madaktari kwa sasa wamechoshwa na hali mbaya ya sekta ya afya kuanzia mlundikano wa wagonjwa, ufunyu wa vifaa tiba na dawa na kwamba mgomo wao ni ishara ya madaktari nchi nzima kujitolea kutetea sekta hiyo licha ya vitisho.
Dk. Chitage pia alisema Dk. Ulimboka alipopata nguvu alielezea yaliyomkuta alipotekwa jana kuwa ni pamoja na kufungwa kitambaa, kamba mikononi na miguuni na kushushiwa kipigo na baadaye alitupwa porini na kufunikwa na majani.
Alisema waliompiga walidhani amekufa hivyo, walimuacha hapo baada ya kupishana wamuue kwa risasi au sindano na kuishia kumtupa porini ambako mwenyewe alijikongoja hadi alipokutana na wasamaria wema na kumuokoa.
Awali akizungumza na waandishi wa habari Msemaji wa MOI Almas Jumaa, alisema hali ya Dk Ulimboka inaendelea vizuri ikilinganishwa na jana ambapo kwa sasa ameanza kuzungumza vizuri na kutambua watu.
Naye Dk Joseph Kahamba anayemtibia Dk Ulimboka alisema hali ya mgonjwa inatia matumaini na kwamba jopo la madaktari bingwa linamhudumia kuhakikisha afya yake inaimarika.
Dk Ulimboka mwenyewe aliwahakikishia watanzania kuwa anaendelea vizuri ila aliomba apatiwe muda apumzike na kuwataka wagonjwa wanaoenda kumuangalia wapungue.
No comments:
Post a Comment